Na Francisca Swai, Mahakama-Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya jana tarehe 27 Octoba, 2022
aliendelea na ziara yake ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama
katika Wilaya ya Tarime ambapo amewaasa watumishi wilayani humo kuzingatia
maadili kwani utumishi bora unalipa.
Akizungumza kwenye kikao
kilichojumuisha watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini na Mahakama ya
Wilaya Tarime, Mhe. Mtulya waliwataka watumishi hao kujenga mazingira ya
kuheshimiana, kupendana, kuthaminiana na kufanyakazi kwa bidii kwani mchango wa
kila mmoja wao unakamilisha jukumu la Mahakama la utoaji haki kwa wote na kwa
wakati.
Jaji Mfawidhi huyo, ambaye
ameambatana na viongozi mbalimbali wa Mahakama Kanda ya Musoma, aliwasihi
watumishi wote kuwa waadilifu na kuishi kulingana na vipato vyao na kutumia
njia halali za kujipatia vipato nje ya mshahara kulingana na fursa
zinazopatikana katika maeneo yanayowazunguka.
Mhe. Mtulya aliwapongeza
watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini kwa kasi nzuri ya umalizaji wa
mashauri licha ya uchache wao ukilinganisha na wingi wa mashauri katika kituo
hicho.
Aidha, akawapongeza
watumishi wanaotumia majengo ya Mahakama za Mwanzo zilizokarabatiwa hivi
karibuni ambazo ni Ngoreme iliyoko Serengeti na Mtana iliyoko Tarime kwa usafi
na utunzaji mzuri wa mazingira. Aliwasisitiza kuendelea na juhudi hizo na kuhakikisha
mipaka ya maeneo yao inalindwa ili kuepuka uvamizi.
Katika ukaguzi huo, msafara
wa Jaji Mfawidhi ulitembelea pia Mahakama ya Mwanzo Mtana ambayo ilifungwa
mwaka 2000 kutokana na wananchi wa eneo hilo kusuluhisha matatizo yao kimila,
hivyo Mahakama kukosa mashauri.
Mahakama hiyo imeanza
kufanya kazi tarehe 1 Agosti 2022 baada ya Mhe. Mtulya kuelekeza ikarabatiwe kutokana
na kukua kwa kijiji hicho, ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi, hivyo
wananchi kuhitaji uwepo wa huduma za kimahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma,
Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama) akiongea na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo
Tarime Mjini pamoja na Mahakama ya Wilaya Tarime.
Muonekano wa Mahakama ya Mwanzo Mtana (juu) kabla ya ukarabati. Muonekano wa Mahakama ya Mwanzo Mtana (chini) baada ya ukarabati.
Muonekano wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme (juu) kabla ya ukarabati Muonekano wa Mahakama ya Mwanzo Ngoreme (chini) baada ya ukarabati.
Picha ya pamoja ya viongozi wa Kanda ya Musoma, viongozi wa Mahakama ya Wilaya Tarime na watumishi wa Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo Tarime Mjini.










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni