Na Lusako Mwang’onda-Mahakama Kuu, Iringa.
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Iringa hivi karibuni ilifanya tamasha kubwa ambalo lilihusisha bonanza
katika michezo mbalimbali, lengo likiwa kuisogeza Mahakama karibu na wananchi
ili kufahamu shughuli inazofanya na kuitumia ipasavyo kama chombo chao cha
usimamizi wa haki hapa nchini.
Bonanza hilo ambalo lilipewa jina la Mahakama
Mtaani, ambapo kauli mbiu yake ilikuwa ni “Njoo Tuongee Kimtaani” lilifanyika baada
ya kufanya utafiti na kugundua kuwa wananchi wengi na hasa wa ngazi ya chini
wanaigopa Mahakama.
Kutokana na hali hiyo, uongozi
wa Mahakama katika Kanda hiyo kwa kushirikisha wadau uliona ni vyema kuandaa
bonanza hilo, ambalo lilishirikisha michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa Miguu,
Mpira wa Pete, Riadha, Kuvuta Kamba, Kucheza rede, Kukuna nazi, Kukimbiza kuku
pamoja na mashindano ya kura na kunywa.
Bonanza hilo la Mahakama
Mtaani lenye dhima kubwa ya kutoa elimu kuhusu maswala mbalimbali ya kimahakama
na kisheria kwa ujumla lilifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ipogolo,
ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa huku mgeni wa heshima akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Mhe Halima Dendego.
Akizungumza na wananchi
waliofurika kwenye tamasha hilo, Jaji Utamwa alisema kuwa lengo kubwa la
bonanza hilo ni kuisogeza Mahakama mtaani na kuwafikia wananchi wa kawaida ili
waijue kama chombo chao kikuu cha usimamizi wa haki.
Mhe. Utamwa alisisitiza
kuwa bonanza hilo limelenga zaidi kutoa elimu katika masuala ya kisheria,
ikiwemo Mirathi, Ndoa, Talaka, Ardhi na Haki Jinai hasa kwa makundi mengi
mtaani ambayo yapo kwenye hatari ya ama kufanya au kufanyiwa makosa ambayo
yatawapelekea wao kuletwa mahakamani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Iringa aliushukuru uongozi wa Mahakama wa Kanda hiyo kwa kubuni tukio hilo
ambalo limekuwa na faida kwa wananchi waliofika kwenye viwanja hivyo. Aliuomba
uongozi huo kuendeleza mabonanza kama hayo ili kuwaongezea wananchi uelewa wa
masuala mbalimbali ya kimahakama na kisheria kwa ujumla.
Mbali na michezo hiyo
katika tamasha hilo, kulikuwa na burudani kutoka kwa wanamziki na vikundi
mbalimbali vya ngoma za asili waliotumbuiza siku hiyo.
Tamasha hilo
lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Mahakama wakiwemo TAKUKUKURU, Chama cha
Wanasheria (TLS), Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, na wengine
ambao wote walishiriki kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria katika
mabanda yao.
Mabingwa wa Mpira wa Miguu Timu ya City Center toka mitaa ya Ipogolo Manispaa ya Iringa wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mahakama baada ya kukabidhiwa Kombe na Ng'ombe dume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni