Na Mary Gwera, Mahakama-Morogoro
Mkurugenzi Msaidizi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa
Mashauri- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Agness Mchome ametoa rai kwa Watumishi wa
Mahakama mpya za Wilaya kuwa wabunifu na uwezo wa kufanya kazi zaidi ya zile za
taaluma zao ‘multitasking’ ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.
Akiwasilisha Mada ya Usimamizi na Uratibu wa
Mashauri kwa njia ya Kieletroniki (JSDS) kwa watumishi hao jana tarehe mosi
Desemba, 2022 mkoani Morogoro, Mhe. Agness alisema ubunifu ni muhimu hususani
katika kipindi hiki ambacho Mahakama inaendelea kuboresha huduma zake.
“Napenda kutoa rai kwenu Watumishi wenzangu kila
mmoja kwa nafasi yake, tafuteni namna ya kuwahusisha hata Madereva, walinzi na
watumishi wa kada nyingine kuingia kwenye mfumo wa JSDS ili kuendana na
mabadiliko ya ki-TEHAMA,” alisema Mhe. Agness.
Aliongeza kwa kueleza umuhimu wa kujua kazi zaidi
ya moja husaidia pia kuziba changamoto ya upungufu wa watumishi, kuokoa muda na
vilevile kuongeza tija katika kazi.
Akiwakumbusha Watumishi hao kuhusu matumizi ya
‘JSDS’, Mhe. Mchome amewasisitiza pia kuwa makini katika usajili ya mashauri na
matumizi mengine yanayohusiana na mfumo huo muhimu kwa Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa
TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Allan Machella akiwasilisha Mada ya Matumizi
bora na sahihi ya Vifaa, Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA amewaasa Washiriki wa
Mafunzo ya Huduma kwa Mteja kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia kwa
kuwa kila siku kuna kitu cha kujifunza katika eneo hilo.
Kadhalika Mkurugenzi huyo amewakumbusha kutunza
vifaa, mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika
kuwezesha utekelezaji wa shughuli za Mahakama.
“Ulimwengu wa sasa ni ulimwengu wa kidijitali
‘digital transformation’, hivyo Watumishi mnapaswa kujua kwamba teknolojia
imekuwa ni sehemu ya Maisha yenu ya kila siku na mnatakiwa kujifunza mambo
mapya kila siku ili msipitwe na mabadiliko ya Teknolojia yanayojitokeza kila
wakati,” alisisitiza Bw. Machella.
Naye Mwezeshaji wa Mafunzo, Bw. Godfrey Wawa
aliyewasilisha mada ya Jinsi ya kukabiliana na Msongo amewaeleza washiriki wa
mafunzo kuwa wanatakiwa kuwa makini kwa kutoongozwa na hisia pindi wanapotaka
kufanya uamuzi wowote katika maisha yao ya kiutumishi na maisha binafsi.
Aidha; katika siku ya nne (4) ya mafunzo hayo
ilitolewa pia Mada kuhusu Matumizi na Utunzaji wa majengo ya Mahakama pamoja na
Vifaa vyake ambapo Maafisa kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Majengo cha Mahakama
ya Tanzania wamewaasa Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya kuyatunza majengo
na kutoa taarifa kwa wakati endapo kuna hitilafu/dosari yoyote.
Leo tarehe 02 Desemba, 2022 ni siku ya mwisho ya Mafunzo kwa sehemu ya Watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya 18 kutoka Gairo, Songwe, Mkinga, Kilombero na Mvomero. Mafunzo kwa Watumishi wengine wa Mahakama za hizo mpya yataendelea kutolewa mfululizo kwa Watumishi wake ambapo yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Desemba, 2022.
Tarehe 25 Novemba,
2022 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma alizindua Mahakama ya Wilaya Busega iliyowakilisha
Mahakama nyingine mpya za Wilaya mpya 17, Mahakama hizo zilizojengwa kwa
ufadhili wa Benki ya Dunia ni pamoja na; Butiama, Rorya, Songwe, Gairo,
Mkinga, Mvomero, Kilombero, Mbogwe, Nyang'hwale, Kyerwa, Itilima, Missenyi,
Kaliua, Uvinza, Buhingwe, Kakonko na Tanganyika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni