Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili wapya aliowaapitisha kutumia
fursa ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama hapa nchini kufungua ofisi
karibu na Mahakama za Wilaya 20 zilizofunguliwa hivi karibuni.
Mhe. Prof. Juma ametoa
wito huo leo tarehe 2 Disemba, 2022 katika Viwanja vya Karimjee jijni Dar es
salaam wakati wa Sherehe za 67 za kuwakubali na kuwaingiza kwenye daftari
Mawakili wapya 358 na kufanya Tanzania kufikisha Mawakili 11,442 wa
kujitegemea.
“Pelekeni huduma
za Mawakili maeneo yote ya Tanzania, Mahakama ya Tanzania inaendelea na juhudi
thabiti za kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na wananchi,” alisema.
Jaji Mkuu alisema kuwa
tangu mwaka 2015 Mahakama ya Tanzania imejenga majengo ya kisasa kutoa huduma
za Mahakama katika mikoa yote ya Tanzania.
Alisema majengo 20
ya Mahakama za Wilaya ambayo ameyazindua katika Wilaya za Mwanga, Same, Busega,
Itilima, Butiama Rorya, Songwe, Gairo, Mkinga, Mbogwe, Nyang’hwale, Kyera,
Missenyi, Kaliua, Uvinza, Buhigwe, Kakonko, Tanganyika, Kilombero na Mvomero ni
fursa kwao katika utoaji wa huduma za uwakili kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mhe. Prof. Juma
alisema baadhi ya Wilaya hizo ni mpya na zina fursa za kutosha kwa Mawakili na zipo
fursa nyingi za kiuchumi ambazo wanaweza kuzitumia ili kujipatia kipato na
kujiendelea kimaisha.
Aliwashauri baada
ya kuapishwa na kuingia katika daftari la Mawakili ni vema wakahama kutoka
mijini na majiji ambako soko la uwakili lina ushindani mkubwa hasa kwa Mawakili
ambao bado hawajapata uzoefu wa kutosha na kwenda vijijini ambako kuna fursa ya
kuwawezesha kujijengea uwezo wa kuendelea katika kazi yao.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisema
kumekuwepo na tabia ya baadhi ya Mawakili kujisahaulisha au kutoutendea haki
wajibu wao wa kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi ya haki kwa wakati.
Alisisitiza kuwa
hiyo siyo tu jambo jema lisilo na maadili, bali pia linawaondolea baadhi hadhi
ya kuwa Maafisa wa Mahakama wanapotekeleza wajibu kwa wateja wao.
Mhe. Dkt. Feleshi
alisema ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi Mawakili ambao watashindwa
kujiendeleza ipo hatari kwao kujikuta wakinukuu Sheria ambayo imeshafanyiwa
mabadiliko na haitumiki tena.
“Kwa mfano, Wakili
anapoamua kufanya rejea kwenye uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu au Mahakama ya
Rufani, anapaswa kusoma uamuzi wote na kuuelewa na siyo kutumia aya moja ya
uamuzi huo hivyo kuipotosha Mahakama pamoja na kwamba Mahakama nayo inalo
jukumu la kuusoma ili kujiridhisha na usahihi wa hoja kwa mujibu wa uamuzi
rejewa,” alisisitiza.
Kwa
upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Prof. Edward
Hoseah aliwataka Mawakili wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili
yaliyopo katika viapo vyao ili waweze kuepuka kujiingiza katika matatizo ya
ukiukaji wa maadili ambayo yanaweza kuwasababishia kukosa sifa ya kuendelea na
utoaji wa huduma hiyo.
Alisema
watakaobainiki kukiuka maadili watachukuliwa hatua kwa mujibu na taratibu na
Sheria zinazolinda viapo vyao kama Maafisa wa Mahakama na kuna uwezekano wa
kuondolewa katika daftari la Mawakili.
Prof.
Hoseah aliongeza kuwa TLS inaendelea kupambana na vishoka ambao wamekuwa
wakiendesha vitendo haramu na visivyo vya kimaadili ya kiutendaji kazi za
uwakili na kuchafua taaluma hiyo muhimu kwa maendeleo ya Nchi.
Alisema
vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha kushuka kwa hadhi ya taaluma ya Uwakili na
kusababisha kutoaminika na Serikali na wadau mbalimbali katika jamii.
“Kuna
baadhi ya watu wanaofanya kazi za uwakili ingawa wao sio mawakili, watu hawa
wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali za kiuwakili kama vile kuandaa na kuthibisha
nyaraka na kushuduhia viapo. Wahalifu wa vitendo viovu ni watu wanaojifanya ni
Mawakili lakini sio Mawakili, tunaendelea kupambana nao,” alisisitiza.
Mwakili wapya wakila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni