Na Mary Gwera, Mahakama-Morogoro
Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba amewaasa Watumishi
wa Mahakama mpya za Wilaya nchini kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake
wafanye kazi kwa ari na weledi ili wananchi wanaokuja kupata huduma katika
Mahakama hizo wapate huduma zilizo bora.
Akizungumza
wakati wa kuahirisha Mafunzo ya Huduma kwa Mteja kwa Watumishi wa Mahakama hizo
jana tarehe 02 Desemba, 2022, Mhe. Chaba ambaye alimuwakilisha Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro alisema kuwa, ana imani kwamba, mafunzo
yaliyotolewa na wawezeshaji yamegusa maeneo muhimu na kutoa uelewa wa namna ya
kupambanua changamoto za kiutendaji na mabadiliko ya kifikra katika maeneo
mbalimbali.
“Nina imani
kuwa kufanyika kwa mafunzo haya kutakuwa chachu ya kuboresha huduma
zitakazotolewa na Mahakama pamoja na wadau katika Mahakama hizi za Wilaya ili
uwekezaji uliofanyika kwenye ujenzi wa majengo hayo ulete tija katika Mahakama
hizo,” alisema Jaji Chaba.
Aliongeza kwa
kuwasisitiza kuwa na ushirikiano miongoni mwa watumishi kwa watumishi pamoja na
wadau wanaoshirikiana nao katika mnyororo wa Huduma za Haki ili
kuzidi kuimarisha imani ya wananchi na wadau kutokana na uboreshaji wa huduma
za Mahakama.
Kadhalika,
aliwakumbusha watumishi hao walioshiriki katika Mafunzo ya huduma kwa mteja
kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya utendaji kazi bora katika maeneo yao ya
kazi na kuziishi vyema jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania katika
uboreshaji wa huduma za haki ili kuweza kuifikia dira yake ya kutoa Haki
sawa kwa wote na kwa wakati.
Akitoa neno la
shukrani, naye Mwakilishi wa Washiriki wa Mafunzo ambaye ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama mpya ya Wilaya ya Songwe, Mhe. Augustine Lugome amesema
wamefurahishwa na mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi vitendo ili kusudi
lilikusudiwa na Mahakama lifikiwe kwa mafanikio.
“Katika kipindi cha siku tano (5) cha mafunzo haya
tumejifunza mambo mengi yenye tija kupitia mada mbalimbali zilizotolewa na
wawezeshaji ambazo ni pamoja na; Maadili ya watumishi, Huduma bora kwa mteja,
Matumizi ya masjala na Serikali mtandao, Mradi wa uboreshaji wa Huduma za
Mahakama, Matumizi sahihi ya TEHAMA na vifaa vya kielektroniki, Kushinda msongo
wa mawazo na namna ya kupambana na sonona, Saikolojia na namna ya kuwianisha
Maisha ya kazi na nje ya kazi na kadhalika. Hivyo tuwahakikishi tutayaishi yote
tuliyofunzwa,” alisema Mhe. Lugome.
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 28
Novemba, 2022 na kuhitimishwa tarehe 02 Desemba, 2022 yametolewa kwa sehemu ya
Watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya 18 kutoka Gairo, Songwe, Mkinga, Kilombero
na Mvomero. Mafunzo kwa Watumishi wengine wa Mahakama za hizo mpya yataendelea
kutolewa mfululizo kwa Watumishi wake katika vituo vya Kigoma, Bukoba na Musoma na mafunzo haya yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe
23 Desemba, 2022 lengo likiwa ni kuwakumbusha watumishi mbinu na namna
bora ya kutoa huduma kwa wananchi.
Mafunzo haya yanafanyika kufuatia uzinduzi wa Mahakama
mpya 18 za Wilaya zilizozinduliwa tarehe 25 Novemba, 2022 na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Mahakama
zilizozinduliwa ni ;- Butiama, Rorya, Songwe, Gairo, Mkinga,
Mvomero, Kilombero, Mbogwe, Nyang'hwale, Kyerwa, Itilima, Missenyi, Kaliua,
Uvinza, Buhingwe, Kakonko na Tanganyika.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akiwatunuku vyeti baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya Huduma kwa Mteja yaliyotolewa kwa sehemu ya Watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni