Alhamisi, 29 Desemba 2022

DIVISHENI YA MAKOSA YA RUSHWA, UHUJUMU UCHUMI YAFUNGUA UKURASA MPYA USIKILIZAJI MASHAURI

 

Na Faustine Kapama-Mahakama

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo tarehe 29 Disemba, 2022 imeendesha mafunzo maalumu kwa ajili ya kuwaandaa watumishi wa Mahakama hiyo kuanza kusikiliza mashauri bila kutumia karatasi (paperless proceedings) kuanzia mwezi ujao.

Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Divisheni hiyo, Mhe. Godfrey Isaya aliwataka watumishi hao kutambua kuwa wanapaswa kufahamu fikapo tarehe 1 Januari, 2023 wataanza kusikiliza mashauri bila kutumia karatasi ikiwa ni utekelezaji wa maagizo kuelekea matumizi kamili ya Mahakama Mtandao (e – judiciary).

“Matumizi ya teknolojia hii mahakamani yatawezesha uharakishaji wa utoaji haki kwa wananchi kwa wakati,” Mhe. Isaya aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa siku moja kwenye Ukumbi wa Maktaba wa Divisheni hiyo mkoani Dar es Salaam chini ya wawezeshaji mahiri waliotoka katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.

Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni iliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ni Mahakama ya mfano katika matumizi ya mtandao kwenye usikilizaji wa mashauri bila kutumia karatasi.

Naye Mtendaji wa Divisheni hiyo, Bi. Masalu Kisasila, akizungumza katika hafla hiyo ya ufunguzi, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa watumishi wa kada zote katika Divisheni hiyo.

Amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kupata uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji kwa vitendo wa safari kuelekea matumizi kamili ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika usikilizaji wa mashauri bila kutumia karatasi (paperless) kuanzia tarehe 1 Januari, 2023 katika Divisheni hiyo.

Hivyo, aliwasihi watumishi hao wakati wa mafunzo hayo kuwa wasikivu na wasisite kuuliza maswali pale watakapoona hawajaelewa ili kuleta tija kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuwa Mahakama ya Tanzania ilishafanya uwekezaji mkubwa kwenye eneo hilo.

Mtendaji wa Mahakama hiyo aliwaahidi wawezeshaji kuwa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itakuwa ya mfano wa kuigwa ukiondoa ya Kigamboni, ambapo Mahakama zingine zitafika kujifunza kuhusu matumizi ya mfumo huo.

Mmoja wa wawezeshaji katika mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Is–haq Bakari Kuppa, akizungumza wakati anawasilisha mada katika mafunzo hayo alieleza kuwa tafsiri rahisi na nyepesi ya maana ya “paperless” katika usikilizaji wa mashauri ni “mtu mmoja anaongea na mwingine anachapa maelezo ya mzungumzaji.”

Hivyo, aliwasilihi watumishi hao kutokuwa na hofu wakati watakapoanza rasmi matumizi ya “paperless”. Naye mwezeshaji mwingine, ambaye ni Msaidizi wa Kumbukumbu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Bw. Oscar Maiseli aliwapitisha watumishi wenzake kwenye mfumo halisi wa mtandao.

Bw. Maiseli aliwaonesha hatua zote kuanzia usajili wa shauri kwa mfumo na kuongeza nyaraka mbalimbali za kimahakama, mfano maelezo ya mashahidi, vielelezo na mwenendo wa shauri hadi kuweka nakala ya hukumu kwenye mfumo.

Kadhalika, alieleza kuwa matumizi ya “paperless” yanakwenda sambamba na uwepo wa jalada gumu kwa kuhifadhi nyaraka ngumu zilizochapwa kwenye mfumo kwa ajili ya rejea (backup file). “Jalada hili halina “handwritten proceedings” yaani mwenendo wa shauri ulioandikwa kwa mkono,” alisema.

 Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Godfrey Isaya  akizungumza wakati anafungua mafunzo maalumu kwa ajili ya kuwaandaa watumishi wa Mahakama hiyo kuanza kusikiliza mashauri bila kutumia karatasi. Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 29 Disemba, 2022  kwenye Ukumbi wa Maktaba wa Divisheni hiyo jijini Dar es Salaam.

Wawezeshaji wa mafunzo ya "paperless" ambao ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Is-haq Bakari Kuppa (aliyesimama kulia) na Msaidizi wa Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Bw. Oscar Maiseli (aliyeinama) wakiandaa mada za kuwasilisha kwa watumishi wa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Is-haq Bakari Kuppa (aliyesimama kulia)akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Sehemu ya watumishi kutoka Divisheni hiyo (juu na chini) ikifuatilia kwa makini uwasilishaji huo wa mada.








 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni