Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka maafisa wa Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) kuboresha matumizi ya teknolojia hiyo mahakamani
ili kuwezesha uharakishaji wa utekelezaji
wa jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Prof.Ole Gabriel alitoa wito huo leo
tarehe 27 Desemba 2022 wakati akifungua mkutano wa Maafisa TEHAMA kutoka mikoa
mbalimbali hapa nchini unaofanyika katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki (IJC) Dodoma.
“Mifumo ikikaa vizuri itasaidia
kupunguza mapungufu yaliyojitokeza katika utendaji kwa mwaka uliopita. Naomba
mboreshe mifumo yenu, tunahitaji kuona TEHAMA inapewa nafasi katika utendaji
kazi za Mahakama wa kila siku,"alisema Mtendaji Mkuu huyo.
Aliwaeleza Maafisa hao kuwa
uimarishaji wa matumizi ya TEHAMA mahakamani utachochea pia ongezeko wa ufanisi
na tija katika utoaji wa haki kwa wananchi wengi kwa gharama nafuu.
Prof Ole Gabriel alifafanua zaidi ya
kuwa mkutano huo ni muhimu kwa watumishi hao kupata nafasi ya kubadilisha
uzoefu wa baadhi ya mambo, hivyo ni heshima ya kipekee kwao kwa sababu Mahakama
inakwenda kubadilika katika matumizi ya TEHAMA.
Alisema msukumo walionao ni
kuimarisha zaidi matumizi ya TEHAMA kwa ngazi zote za Mahakama ambapo hadi sasa
asilimia 99 ya mashauri yanafunguliwa kwa njia ya mtandao ili kuwarahisishia
wananchi upatikanaji wa huduma katika mazingira nafuu.
Aidha, Prof. Ole Gabriel alisema
zaidi ya asilimia 70 ya mashauri yanatoka kwenye Mahakama za Mwanzo na kusema
kuwa ni vema wakaweka nguvu katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika
Mahakama hizo ili wananchi wengi nao waweze kufikiwa na huduma hizo.
Wakati huo huo Mtendaji Mkuu huyo wa
Mahakama ya Tanzania alisema hivi sasa wameanzisha huduma mbalimbali kwa ajili
ya kuwawezesha wananchi kutoa maoni yao na kuuliza maswali pale wanapoona
hawakutendewa haki ili wapate ufafanuzi sahihi kwa kutumia mifumo mbalimbali.
Alitaja huduma zinazoendelea ni
Kipindi cha Sema na Mahakama cha kila siku ya Jumanne kuanzia saa 12.30 jioni
hadi saa 1.30 usiku kupitia Runinga ya ITV na kile cha Shirika la Utangazaji la
Tanzania (TBC) cha siku ya Alhamis kuanzia saa 12.00 jioini hadi saa 1.00
usiku.
Prof. Ole Gabriel aliongeza kuwa
njia nyingine ambayo imeanzishwa na Mahakama ni kutoa maoni au kuuliza maswali
kupitia Kituo cha Taarifa cha Mahakama ya Tanzania (Call Center) kwa namba
0752500400 au namba ya bila malipo ya 0800750247.
“Kadhalika tumefungua laini ya
kushugulikia ndoa na mirathi pekee. Mikakati iliyopo ni kuboresha miundombinu
ya TEHAMA na matumizi ya Mahakama mtandao hivyo tunakwenda kuwekeza zaidi
kwenye eneo hili,” alisisitiza.
Prof. Ole Gabriel aliwaomba wananchi
kutumia mifumo mbalimbali iliyoanziswa na Mahakama ya Tanzania kupata majawabu
ya maswali na kero zao badala ya kusafiri na kutumia fedha nyingi kwa jambo
ambalo suluhu yake wangeipata wakiwa nyumbani.
Aliongeza kuwa hivi sasa Mahakama ya
Tanzania ipo kwenye hatua za mwisho za majaribio ya matumizi ya mfumo wa akili bandia ambao
utakuwa ukitafsiri mambo mbalimbali na kuandika nakala za hukumu.
Prof. Ole Gabriel aliwataka Maafisa
TEHAMA kubadilika na kufikiria nje ya boksi ili waweze kuendana na kasi ya
utendaji wa Mahakama kupitia kiongozi wao ambaye ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya
TEHAMA(DICT), Bw. Enock Kalege akizungumza katika hafla hiyo alisema Maafisa
hao wanakutano ili kutathimini utekelezaji wao wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya
Tanzania na kuboresha maeneo ambayo hawakufikia malengo. Alisema mkutano huo unajumuisha Maafisa
TEHAMA 49 kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara.
Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel(katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Maaafisa TEHAMA kutoka Mahakama Kuu Divisheni mbalimbali baada ya ufunguzi wa Mkutano wao.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama ya
Tanzania)
Asante kwa taarifa mna mpango wa kuajiri lini mafisa TEHAMA maana mwezi wa Saba hamukuajili TEHAMA
JibuFuta