Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 29 Disemba, 2022 ameongoza
timu ya kwanza ya watumishi kuhamia katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania lililopo jijini hapa ambapo inategemewa kuwa hadi kufikia mwisho wa
mwaka huu wa fedha awamu zote za watumishi wanaotakiwa kuhamia Dodoma zitakuwa
zimekamilika.
Akizungumza akiwa ofisini kwake
katika jengo hilo jipya na la kisasa, Prof. Ole Gabriel amemshukuru Jaji Mkuu
wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa uongozi wake mahiri ambao umewezesha
mpango wa kuanza kuhamia katika Makao Makuu ya Mahakama tarehe 29 Disemba, 2022
kufanikiwa kama ulivyopangwa. Amesema hatua hiyo imefanya Mhimili wa Mahakama
kuanza kuungana na Mihimili Mingine (Serikali Kuu na Bunge) ambayo imeshahamia
Dodoma.
Mtendaji Mkuu amesema kuwa mradi wa ujenzi
wa jengo hilo hadi kukamilika kwakwe utagharimu jumla ya shilingi bilioni 129.7
za Kitanzania. Amesema jengo hilo lina ukubwa wa mita za mraba 60,000, hivyo
kulifanya liwe la sita kwa ukubwa duniani kwa Makao Makuu za Mahakama. Prof.
Ole Gabriel akabainisha kuwa kazi kubwa iliyopo sasa ni kuweka samani na kazi
zingine za nje ili kunadhifisha mazingira na jengo lenyewe. Amesema baada ya
hatua hizo taratibu za uzinduzi wa jengo hilo zitafanyika kwa itifaki stahiki.
Aidha Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama
aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo mkubwa katika
mradi huo ambao umeiwezesha Mahakama ya Tanzania nayo kuwa na Makao Makuu yake
na jengo la hadhi ya juu.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Beatrice Parick, akizungumza katika
halfa hiyo fupi alisema watumishi wamefurahi kuhamia Dodoma kwa kuwa wamepata mazingira
mazuri ya kufanyia kazi ambayo yatawasaidia katika kuongeza ufanisi wa utoaji
wa huduma za haki kwa wananchi.
Aliongeza kuwa uwepo wa viwanja vya
michezo mbalimbali katika eneo hilo utatoa fursa kwa watumishi wa Mahakama ya
Tanzania Makao Makuu kufanya mazoezi ambayo yatawasaidia kujikinga na magonjwa
yasiyo ya kuambukizwa.
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa
Kampuni ya Arqes Africa Architects and Interior Designers Ltd, Bi. Rose Nestory,
akizungumza wakati wa kukabidhi jengo hilo alisema hivi sasa watumishi wa
Mahakama wanaruhusiwa kuanza kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwani kazi
zilizobakia hazitaathiri utendaji wao wa kazi. Bi. Rose ameshukuru uongozi wa Mahakama
kwa kuwaamini kama wabunifu wa jengo na pia Mkandarasi CRJE ambaye amefanya
kazi ya ujenzi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akipokea hati ya matumizi ya sehemu ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania kutoka kwa Mshauri Elekezi wa Kampuni ya Arqes Africa Architects and Interior Designers Ltd, Msanifu Rose Nestory (katikati).
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni