Na Stanslaus Makendi-Mahakama Kuu, Dodoma
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt Gerald
Ndika hivi karibuni aliambatana na wadau mbalimbali wa Mahakama na kumtembelea
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel katika ofisi
yake iliyopo kwenye jengo la Makao Makuu ya Mahakama lililopo jijini hapa.
Jaji Ndika na wadau hao wa Mahakama wanakuwa miongoni mwa
wageni wa awali kutembelea jengo hilo ikiwa ni siku chache tangu watumishi wa
Mahakama kuanza kuhamia rasmi Dodoma. Wageni hao wa Mtendaji Mkuu walipata
fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za jengo hilo la Makao Makuu ya Mahakama pamoja
na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Majaji unaoendelea kutekelezwa kwa
kasi katika eneo la Iyumbu.
Akizungumza wakati anatoa neno la ukaribisho kwa wageni hao,
Prof. Ole Gabriel amemshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma na viongozi wengine ndani ya Mhimili wa Mahakama kwa usimamizi thabiti
ambao umewezesha mpango wa kuanza kuhamia katika Makao Makuu ya Mahakama
kutekelezwa kama ilivyopangwa.
Mtendaji Mkuu alibainisha kuwa mradi huo wa ujenzi wa jengo lenye
vifaa na vitendea kazi vya kisasa ambalo litakuwa la sita kwa ukubwa duniani
baina ya majengo ya Makao Makuu ya Mahakama, utagharimu takribani shilingi
bilioni 129 za Kitanzania hadi kukamilika kwake.
Tayari jengo hilo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
lililopo katika eneo la Tambukareli limeanza kutumika tangu tarehe 29 Disemba,
2022.
Prof. Ole Gabriel alibainisha pia kuwa ujenzi wa nyumba za Majaji
utawezesha viongozi hao kuwa na makazi ya uhakika na ya kisasa pindi
watakapohamia Dodoma.
Kwa upande wake, Jaji Ndika alimpongeza Jaji Mkuu wa
Tanzania na Mtendaji Mkuu kwa kuwa chachu na mstari wa mbele katika kuhakikisha
mradi huo unakamilika kwa wakati na kuwezesha Mahakama kuhamia Dodoma.
Mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali, Mhe. Ndika alisifu
uzuri wa kipekee wa jengo hilo, hivyo anaamini sehemu hiyo itakuwa kama motisha
kwa watumishi kufanya kazi katika mazingira mazuri. “Sehemu nzuri na salama kwa
kazi ni motisha kwa watumishi, motisha siyo fedha pekee” alisema Jaji Ndika.
Naye Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatmah Khalfan aliwapongeza viongozi wa Mahakama kwa hatua
hiyo ya kuanza kuhamia Dodoma sambamba na kuipongeza Serikali kwa uwezeshaji wa
ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya kisasa.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatmah Khalfan (aliyesimama) akitoa neno la shukrani kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa mapokezi mazuri ya ugeni huo na kumkaribisha jijini Dodoma mara baada ya ofisi yake kuhamia katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni