Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Mkurugenzi Msaidizi
wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Allan Machela amewahimiza watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe,
Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika kwenda sambamba na madadiliko yanayoendelea
hivi sasa mahakamani, hasa katika matumizi ya teknolojia mpya katika shughuli
za utoaji haki kwa wananchi.
Akiwasilisha mada
kuhusu Matumizi ya Vifaa vya TEHAMA katika siku ya tatu ya mafunzo ya huduma
bora kwa mteja yanayofanyika katika Kituo cha Kigoma, Bw. Machela amesema watumishi
wa Mahakama hizo hawana budi kuendelea kujifunza juu ya mabadiliko hayo kwa
kuwa wanaenda kuhuduma katika majengo mapya ambayo yamefungwa vifaa na mifumo
ya kisasa.
“Msilale usingizi,
msijisahau kwenye matumizi ya TEHAMA kwa sababu TEHAMA ipo kila mahali,
ukilala, ukiamka, ukitembea ni TEHAMA. Kwa hiyo ukilala, umeachwa. Naomba
muendelee kujifunza na kujikumbusha mara kwa mara, kimbieni kwa mwendo huu wa
madadiliko ya teknolojia hasa kwenye shughuli za kimahakama, hakuna kulala,”
alisema.
Amewaeleza
watumishi hao kuwa wanatakiwa kuwa na bidii ya kujifunza ili waweze kuwa na matumizi
bora, salama na sahihi ya vifaa hivyo kwa sababu wanaenda kuingia kwenye
majengo mapya ambayo yamejengwa kisasa na kufungwa mifumo ya teknolojia mpya.
“Vifaa hivi ni vya
kisasa na teknolojia inabadilika kila siku, ulichokutana nacho mwaka jana au
mwaka juzi sicho utakachokutana nacho leo, kwa hiyo ni lazima kwenda na
mabadiliko haya ya teknolojia ili wote twende pamoja. Niwaambie tu kwamba
matumizi ya TEHAMA kwa sasa mahakamani hayana mbadala,” alisema.
Bw. Machela
aliwaambia washiriki hao kuwa TEHMA katika Mahakama ina jukumu muhimu katika
kuhakikisha kwamba dira, dhamira na mpango mkakati unatekelezwa vyema kupitia
uboreshaji wa kisasa na uendeshaji wa shughuli za kimahakama kwa kutumia miundombinu
halisi na ile ya kwenye mtandao.
Alibainisha kuwa TEHAMA
ni chombo muhimu katika uboreshaji wa shughuli za Mahakama au mfumo wa Mahakama,
lakini inaweza kubaki kuwa zana ikiwa hawataitumia kwa ustadi, badala yake
inaweza kuvuruga juhudi za uboreshaji unaotarajiwa.
Kwa mujibu wa
Naibu Mkurugenzi huyo, teknolojia ya habari hutengeneza fursa na changamoto
ambazo zinahitaji kueleweka vizuri na kusimamiwa kikamilifu, ikiwa Mahakama ya
Tanzania italazimika kufaidika kikamilifu na kile ambacho Teknolojia ya Habari
inatoa.
Mahakama ya
Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi
watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki
ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo
ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga
kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi
zinazoendana na uzuri wa majengo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni