Na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa, Mahakama ya Tanzania
kupitia awamu ya pili (II) ya Mradi wa Uboreshaji huduma wa mwaka 2021-2025 unaofadhiliwa
na Benki ya Dunia (WB) imetenga jumla ya Dola milioni 6 katika
eneo la
kuongeza mafunzo ya kuongeza Ujuzi (Skills) na Maarifa (knowledge) kwa watumishi wa Mahakama sambamba
na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA).
Akizungumza na Wahitimu wa Astashahada na Stashahada
ya Sheria pamoja na wageni waalikwa katika Mahafali ya 22 ya Chuo hicho leo
tarehe 07 Desemba, 2022, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, lengo ni kuhakikisha Chuo hicho kinachotoa
elimu na mafunzo kwa wanafunzi wake na kwa watumishi wa Mahakama kwa njia ya
TEHAMA.
“Kutengwa kwa kiasi hicho kikubwa cha
fedha katika Mradi huu
wa pili ni
ushahidi
kuwa, Chuo kinatakiwa kuhama kutoka ‘analogue’ hadi kidijitali katika utoaji wa mafunzo. Fedha
zilizotengwa sio za Semina na Makongamano, ni za Maboresho ambayo yatatoa
matokeo, yatakayopimika na yatakayotathminiwa (evaluated) na Serikali ya
Tanzania na Maafisa wa Benki ya Dunia, hivyo ni muhimu kuchangamkia nafasi hii,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, Chuo
cha Uongozi wa Mahakama kinatakiwa kitengeneze Jukwaa la Ki-elektroniki ‘e-learning platform’
litakalotumia
akilibandia (Artificial
Intelligence) kwa ajili ya kufundishia, na wanafunzi kupata mafunzo kwa njia ya
mtandao.
Ameongeza kuwa, jukwaa hilo linatakiwa liwe la kisasa na lenye
ubora, na liweze kutumika kutoa elimu na mafunzo sio tu kwa wanafunzi wa
Stashahada na Astashahada ya Sheria, bali pia litumike kutoa masomo na mafunzo
Elekezi na Endelevu kwa Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Watendaji, Mahakimu
na Watumishi wa kada zote.
“Ni mategemeo yetu kuwa, Jukwaa hilo
litasheheni taarifa na mambo yote muhimu ambayo wanafunzi, wahadhiri na watumiaji
wengine watajisomea na kujiendeleza: “Support for the launch of the IJA’s
e-learning platform and courses and for the use of AI tools for state
of-the-art trainee experience and use by judges, 11 magistrates, and newly
employed Judges, Magistrates, Registrars, Administrators and Staff.” Baada ya
kuwekeza katika Jukwaa (e-learning platform) Chuo hiki hakitakuwa kisiwa,
kitapata wanafunzi dunia nzima
na kuwawezesha
watumishi walio kazini kuendelea na kazi huku wakisoma,” ameeleza Jaji Mkuu.
Amesema kuwa, Jukwaa la
Ki-elektroniki litakalotengenezwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa ajili ya
kutoa mafunzo (e-learning platform), litasaidia kuokoa muda kwakuwa litatumika kutoa mafunzo
katika majengo Jumuishi yaliyojengwa na yatakayojengwa na Mahakama na ambayo
yatatumika pia kama vituo vya mafunzo kwa njia ya teknolojia kwa watumishi na
wadau bila kusafiri hadi IJA Lushoto.
Amewasihi Wahadhiri, Wakufunzi na Watumishi wote wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto, kujitayarisha na matumizi ya Jukwaa la Ki-elektroniki
(e-learning platform) kutoa mafunzo na elimu sio tu kwa wale waliopo ndani ya
Kampasi hiyo,
bali hata wale walio nje ya Kampasi Chuo. “Mkifanikiwa
kutekeleza matarajio ya Mradi wa Maboresho ya Mahakama kwa kusanifu upya
Stashahada ya Sheria, Astashahada ya Sheria, na mafunzo Elekezi na Endelevu,
mtakuwa mmetoa mchango mkubwa katika kuboresha Elimu ya Sheria Tanzania,” amesisitiza.
Kwa upande wa Wahitimu, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma
amewaeleza kuwa, Watanzania wa leo wanaishi katika dunia
inayosukumwa na Teknolojia yenye nguvu kubwa ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th Industrial Revolution). Hivyo, wahitimu wote wenye elimu ya
ngazi au daraja lolote ni lazima wahakikishe kuwa elimu waliyopata kutoka Chuo
cha Uongozi wa Mahakama haitoshi na
ni
lazima waiboreshe kila siku ili ilingane na mahitaji ya ushindani mkubwa katika
Karne ya 21.
Mbali na kuweka msisitizo kwenye TEHAMA, Mhe. Prof.
Juma aliyekuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali ya Chuo hicho, amewaasa Wahitimu wote
kuwa waadilifu, nidhamu ya kweli na sio ya woga, bidii na wenye ujuzi wa
kutosha, uwezo wa kiuongozi
kuanzia ngazi ya familia hadi kitaifa na kuwa wanajamii wema na kuitumikia vyema jamii.
“Nawaomba wahitimu wote kutambua kuwa
siku zote elimu uliyonayo huwa haitoshi. Kasi ya maboresho na Mabadiliko ya
Elimu inatakiwa ilingane na Kasi ya Mabadiliko ya Mahitaji ya Jamii husika kwa kuzingatia uadilifu na nidhamu ya kweli katika
kazi,” amesema Jaji Mkuu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya
Rufani (T), Mhe. Dkt. Gerald Ndika amesema kuwa, Chuo hicho kimepata mafanikio
makubwa ikiwa ni pamoja na kukamilisha utayarishaji wa Mwongozo wa Ufundishaji
wa ajili ya Watunza Kumbukumbu wa Mahakama kuhusu Uendeshaji wa mashauri ya
Watoto (Training Guide for Record Management Assistants on Handling Juvenile
Cases).
Mhe. Dkt. Ndika ameongeza kuwa, Chuo hicho kimeweza kufanya
mafunzo elekezi kwa Majaji wa ngazi zote pamoja na kwa watumishi wapya wa kada
zote za Mahakama kitu ambacho ni hatua kubwa katika kujenga uwezo katika
utendaji kazi.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa
Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ameeleza kwamba, katika mahafali
hayo jumla ya wanafunzi 574 wamehitimu masomo yao, ambapo kati yao 289 ni wa
kike na 286 ni wa kiume. Wahitimu wa Astashahada ya Sheria (NTA Level 4) ni 348
na wa Stashahada ni 226. Idadi hii inafanya jumla ya wahitimu wa Chuo hicho
kufikia leo kuwa 1,148.
Kabla ya kushiriki katika mahafali hayo, Jaji Mkuu,
Mhe. Prof. Juma alizindua bweni la wavulana wanaosoma katika chuo hicho. Wageni
wengine waliohudhuria katika mahafali hayo ni Mhe. Dkt. Benhajj Masoud, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa
Vitendo (LST), Mhe. Dkt. Juliana Masabo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Moshi, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Frederick Manyanda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto, Wahadhiri na Watumishi cha Chuo cha IJA, wazazi pamoja na wageni wengine waalikwa.
Sehemu ya wahitimu wakiwa katika hafla ya Mahafali ya 22 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni