Jumatano, 7 Desemba 2022

MWANASAIKOLOJIA ATOA MWELEKEO

·Ahimiza uaminifu, uvumilivu kazini

·Ataka mwenye yake abaki nayo mwenyewe

 Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma

Mwanasaikolojia, Bi. Sadaka Gandi amewasihi watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika kuwa waaminifu na wavumilivu wanapotekeleza majukumu yao ili kujenga taswila njema ya Mahakama ya Tanzania kwa wananchi.

Bi. Gandi ametoa wito huo leo tarehe 7 Disemba, 2022 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Uaminifu, Uvumilivu na Saikolojia mahali pa kazi kwa watumishi kutoka Mahakama hizo wanaohudhuria mafunzo ya siku tano ya huduma bora kwa mteja katika Kituo cha Kigoma.

“Kwa Mahakimu, kuweni makini sana, kosa lako dogo tu linaharibu taswila nzima ya taasisi kwa watu mnaowahudumia. Mwagalie yule bibi anayekuja mbele yako akiwa amedhulumiwa haki yake ya mirathi, lakini kumbe wewe unajuana na wale wa upande wa pili na ukamyima haki yake, kilio cha huyu bibi kitakutafuna wewe na kizazi chako,” alionya Mwanasaikolojia huyo.

Alieleza kuwa uaminifu unaonyesha uungwaji mkono wa dhati kwa taasisi na husaidia kupunguza msuguano, huleta hali ya kutegemewa kusaidia kwa muda mrefu katika kufikia mafanikio na kwamba waajiri wanahitaji wafanyakazi waaminifu ili kuwasaidia kukua pamoja kupitia ushindani ili waendelee kuishi.

Mwanasaikolojia huyo aliwaambia washiriki hao wa mafunzo kuchuja nafsi zao kwa sababu wanafanyia kazi maisha ya watu wengine. Hivyo, amewaomba mara zote kukumbuka kuwa kila wanachokifanya ni kwa faida ya wateja wanaowahudumia, ambao ni wananchi.

Bi. Gandi amesema anatambua kila binadamu anakabiliana na changamoto mbalimbali katika safari ya maisha, lakini akatanabaisha kuwa wao kama watumishi hawatakiwi kupeleka vurugu zao za kimaisha kazini.

“Pambana na vurugu zako ukiwa huko nje. Hakikisha ubinadamu wako upo pale kumlinda mwajiri wako, mfumo wa mzima wa Mahakama na wateja wako, ambao ni hao wananchi wanaokuja mbele yako kila siku kupata huduma. Ukiwa muumini wa kile Mahakama inachoamini utakuwa mwanifu na mzalendo,” alisema.

Kadhalika, Bi. Gandi amewaomba watumishi hao kuvumiliana wawapo kazini kwa kuzingatia kuwa kila binadamu ana mapungufu yake, ana mitizamo na akili tofauti na aina tofauti ya utendaji kazi.

“Ni muhimu kuvumiliana katika mazingira ya kazi. Uvumilivu ni muhimu na jifunze kutowafanyia wengine kile ambacho wewe usingependa kufanyiwa. Jifunze kuvaa viatu vya wengine, ila usiingize miguu yako mahali ambapo hapakuhusu,” Mwanasaikolojia huyo aliwaambia watumishi hao.

Bi. Gandi amewaomba washiriki hao wa mafunzo kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa moyo na uaminifu kwa vile anaamini hakuna miongoni mwao kama binadamu aliyeumbwa na Mungu akiwa na tabia mbaya.

“Hakuna mtu aliyezaliwa na hasira. Hakuna ambaye ameumbwa na Mungu ana hasira wala kiburi. Mambo haya yote tunajifunza na kuyatengeneza wenyewe. Kila mtu na achukue nafasi yake, usikubali kubadili mtizamo wako kwa sababu ya mtu mwingine,” alisema.

Amewashauri watumishi hao kujikubali, kujitambua na kujiona wao ndiyo sura ya Mahakama, hivyo wanapaswa kuacha kufanya uamuzi kwa hisia bila kupima matokeo yake kwa wale wanaowahudumia katika mnyororo mzima wa utoaji haki.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.


Mwanasaikolojia, Bi. Sadaka Gandi akisisitiza jambo alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya huduma bora kwa mteja ambayo yamewaleta pamoja watumishi wa Mahakama za Wilaya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika kwenye Kituo cha Kigoma.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo (juu na chini) ikimsikiliza kwa makini Mwanasaikolojia huyo.

Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo hayo (juu na chini) ikimsikiliza kwa makini Mwanasaikolojia huyo wakati anawasilisha mada yake.


Washiriki wengine wa mafunzo hayo ( picha mbili juu na moja chini) ikimsikiliza kwa makini Mwanasaikolojia  Sadaka Gandi wakati anawasilisha mada yake.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni