Jumanne, 6 Desemba 2022

WITO MUHIMU KWA WATUMISHI MAHAKAMA ZA WILAYA MPYA

Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma

Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika wamehimizwa kutunza miundombinu watakayoitumia kwenye maeoneo yao ili iweze kukidhi matarajio ya Mahakama ya Tanzania ya kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi katika mazingira bora na wezeshi.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 6 Disemba, 2022 na Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama, Mhe. Edward Mpabansi alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Tathmini ya Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho wa Mahakama ya Tanzania kwenye mafunzo ya huduma bora kwa mteja yanayotolewa katika Kituo cha Kigoma kwa watumishi kutoka Mahakama hizo.

“Mahakama na Serikali zimetumia nguvu, muda na rasilimali fedha nyingi katika kuhakikisha huu uboreshaji unapatikana.Tumetengeneza mifumo ya kuweza kurahisisha umalizaji wa mashauri, tumetengeneza majengo kuhakikisha kwamba kuna mazingira bora ya kufanyia kazi kwa Mahakimu na watumishi wengine. Kwa hiyo, ni jukumu lenu kuitunza miundombinu hii,” alisema.

Amewasisitiza watumishi hao kuwa wanapokwenda kuanza kutoa huduma katika Mahakama hizo mpya lazima wajitahidi kusimamia zile rasilimali walizonazo, kwa maana ya majengo na kila kitu ambacho wamekabidhiwa, ili yaweze kuhudumia watu wengi kuanzia kizazi cha sasa na kijacho.

“Kwa sasa unakabidhiwa miundombinu mipya, isipotunzwa haiwezi kuleta matokeo ambayo yamekusudiwa, kwa maana kupatikana kwa haki kwa wakati na inayofikika. Matarajio haya ya Mahakama hayawezi kufikiwa kama hatutatunza miundombinu hiyo”, Mhe. Mpabansi alisema.

Amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa maendeleo yanayoonekana kwa sasa ndani ya Mahakama yamewatesa watu wengi kwa miaka mingi, wamefanya tafiti mbalimbali, wametumia rasimimali fedha nyingi, akili nyingi na viongozi wametumia pia muda mwingi kufanikisha uboreshaji huo.

“Tutakuwa hatutendi haki kama hatuwezi kuenzi na kulinda uboreshaji huu. Kwa hiyo, sadaka kubwa kama watumishi mnao wajibu wa kulinda uboreshaji huu ili uweze kuleta matokeo ambayo yamekusudiwa, ikiwemo kutoa haki kwa wakati na bila upendeleo,” alieleza.

Aidha, Mhe. Mpabansi aliwakumbusha watumishi hao kuwa uboreshaji wote unaofanyika mahakamani unamlenga mwananchi ambaye ndiye mlipa kodi na anastahili kuhudumiwa na mtumishi bila kinyongo cha aina yoyote kwa vile yeye ndiye mhusika mkuu wa yote wanayofanya.

“Mlengwa mkuu wa kila kitu tunachofanya ni mwananchi. Mwananchi akija mahakamani lazima apewe kipaumbele. Nawaomba mzingatie kanuni inayosema mteja hakosei, hata kama amekuudhi na mteja kwetu ni mwananchi. Tukifanya haya tutakuwa tunatimiza nguzo ya tatu ya kuimarisha imani kwa mwananchi na kushirikisha wadau katika huduma tunazotoa,” alisema.

Awali, watumishi hao walipitishwa kwenye mada nyingine kuhusu Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula. Katika wasilisho lake, Mkurugenzi huyo aliwaeleza mambo mbalimbali, ikiwemo utaratibu wa kufungua na utunzaji wa majalada kwa mujibu wa taratibu zilizoelezwa kwenye Mwongozo wa Masjala katika ofisi za umma.

Alisema kuwa baadhi ya taasisi za umma zimekuwa haziutekelezi kikamilifu Mwongozo huo. Bw. Manyambula alisisitiza kuwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kila Idara au Kitengo inatakiwa kuwa na majalada yanayohusu kazi zao.

“Watumishi wa masjala tu ndio wanaofungua majalada kwa kufuata utaratibu unaotumika serikalini ambao umeelezwa kwa ufasaha kupitia Mwongozo wa Masjala kwa Taasisi za Umma. Watumishi wengine ndani ya taasisi hawaruhusiwi  kufungua majalada,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliwaeleza washiriki hao wa mafunzo baadhi ya madhara ya kutozingatia mwongozo wa kufungua na kutunza majalada, ikiwemo kuchelewesha utoaji wa uamuzi au kutoa  uamuzi usiosahihi, menejimenti kutokuwa na ufahamu wa kutosha wa kazi za taasisi na uvujaji wa siri za Serikali.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.

Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama, Mhe. Edward Mpabansi akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kwenye mafunzo ambayo yamewaleta pamoja watumishi kutoka Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika ambayo yanafanyika katika Kituo cha Kigoma.
Mnatunza wapi nyaraka katika Mahakama zenu? Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula akiuliza alipokuwa anawapitisha washiriki wa mafunzo hayo katika mada kuhusu utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo (juu na chini) ikifuatilia mada mbalimbali.

Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo (juu na chini) ikifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa.


Sehemu nyingine ya tatu ya washiriki wa mafunzo (picha mbili juu na moja chini) ikifuatilia mada mbalimbali.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni