Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Mafunzo ya huduma kwa mteja kwa watumishi
wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika yameingia
siku ya pili leo tarehe 6 Disemba, 2022 huku Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Sharmillah Sarwatt akiwataka washiriki hao kutoa huduma bora kwa wananchi
wanapotekeleza majukumu yao mahali pa kazi.
Akiwasilisha mada kuhusu Wajibu na Majukumu
ya Watumishi katika Mahakama za Chini, Mhe. Sarwatt aliwaambia washiriki hao wa
mafunzo kuwa matarajio ya wananchi ni makubwa, hivyo wanahitaji kutimiza wajibu
wao kwa kiwango kitakachowafanya wajisikie wapo mahala salama au peponi.
“Tunajua hakuna miongoni mwetu anayejua
peponi kuna nini, lakini itoshe tu kusema tunategemea hali ya juu ya maadili
kutoka kwenu. Hata kama tuna changamoto zetu, bado hazitupi kibali cha kumhudumia
vibaya mwananchi. Tunahitaji kutoa huduma bora kwa mwananchi, na hili ndilo
tegemeo letu,” alisema.
Msajili wa Mahakama Kuu huyo aliwaeleza
watumishi hao sababu kadhaa za kujengwa Mahakama watakazohudumu kwa muundo kama
unavyoonekama, ikiwemo kuandaa njia ya kupata haki kwa wote kama Mahakama inavyotarajia,
kuwa na mtindo mpya wa kufanya kazi kwa uwazi na matumizi ya teknolojia.
“Labda niwaambie ndugu zangu, kwa namna
tunavyokwenda kwa sasa, matumizi ya teknolojia katika shughuli za kimahakama
hayana mbadala, ukipenda utatumia na usipopenda utatumia. Anzeni kutumia teknolojia
kuendesha shughuli za Mahakama mkifika kwenye vituo vyenu vya kazi, hili halina
mjadala,” Mhe. Sarwatt alisisitiza.
Naye Afisa Utumishi Mwandamizi wa
Mahakama, Bw. Jumanne Muna, akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa Huduma kwa
Mteja, aliwaomba washiriki hao wa mafunzo kutambua kuwa wanalojukumu kubwa la
kutangaza mema ya Mahakama kupitia huduma wanazozitoa kwa wamanchi.
Akiwasilisha mada hiyo kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice
Patrick, Bw. Muna alieleza kuwa watumishi wakitoa huduma bora kwa wananchi watapeleka
taswila njema kwa jamii na jamii itatambua kuwa mahakamani ni mahala salama
kuliko pengine katika muktadha mzima wa utoaji wa haki nchini.
“Mahakama ni sehemu ya kutoa huduma. Lazima
kama sisi watumishi tujiulize tunatoa huduma za namna gani na kwa wakati gani. Lazima
tujue huduma wanazohitaji wateja wetu. Wateja wetu wanamatarajio makubwa sana
kutoka kwetu. Kwa hiyo, inatulazimu sasa kuwahudumia vizuri kwa vile bila wao
hatutakuwa na stahiki yoyote ya kuendelea kuwa sehemu zetu za kazi,” alisema.
Bw. Muna amewakumbusha watumishi hao
baadhi ya huduma ambazo wanapaswa kuzitoa kwa wateja, ikiwemo kutoa kalenda ya
shughuli za Mahakama; kutoa ratiba ya kusikiliza mashauri; kupokea, kusajili na
kusikiliza mashauri; kutayarisha na kusoma uamuzi; kutoa na kuthibitisha nyaraka mbalimbali za kimahakama na kutekeleza, kukaza hukumu, amri na uamuzi
wa Mahakama.
“Hatuna budi kutekeleza majukumu ya Mahakama
na kuhakikisha kuwa tunazingatia viwango vilivyobainishwa na kutoa huduma kwa
ubora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya mteja. Tuna jukumu la kuijenga
taswira ya Mahakama na kurudisha imani kwa wananchi,” alisema.
Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya
huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za
Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye
vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia
ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa
majengo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni