Na Catherine Francis – Mahakama Kuu Songea
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Dkt.
Yose Mlyambina aliyetunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD) hivi karibuni amewaahidi
Watumishi wa Kanda hiyo kuwa, atatumia elimu aliyoipata kwa manufaa na kwamba itakuwa
chachu kwa maendeleo ya Kanda hiyo na Taasisi kwa ujumla.
Akizungumza na Watumishi hao hivi karibuni katika hafla (surprise party) aliyofanyiwa na Watumishi wa Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Mlyambina ambaye alionesha kufurahishwa na hafla hiyo aliyoandaliwa kwa upendo, aliwahakikishia kuwa amemaliza shule, lakini safari ya kukitumikia cheti alichokipata ndio imeanza hivyo hana budi kuhakikisha haki inatolewa kwa weledi.
“Natamani kuona elimu niliyoipata iweze kuwa hamasa
kwa wote kuweza kuendelea mbele kielimu wasiishie hapo walipo kwakuwa, hakuna
linaloshindakana yote yanawezekana ukiwa na nia ya kufanya jambo fulani na
kuandaa utayari katika kulitekeleza,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Mhe. Dkt. Mlyambina aliwashukuru Watumishi hao pamoja
na Wadau wa Mahakama waliokuwa wamekusanyika pamoja kumpongeza kwa mafanikio
hayo aliyoyapata. Pia aliwasisitiza kuwa na upendo na ushirikiano huo usianzie
na kuishia kwake tu bali waendelee kuishi kindugu na upendo na kushirikiana kwa
kila jambo na kwa kila mmoja wao.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Mlyambina alisema kwamba,
anatamani elimu aliyoipata iweze kuleta manufaa kwa Taifa hivyo anaandaa andiko
(kitabu) ambacho kitasaidia katika kuleta mbadiliko ya kimaendeleo kwakuwa ili
Taifa lipate kufanikiwa ubunifu wa hali juu unahitajika katika kuendeleza nchi,
hivyo atajikita zaidi kwenye ubunifu wa kutatua changamoto za kisheria
zilizopo.
Katika hafla hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha alinukuu neno kutoka kwenye Biblia ili
likapate kumuongoza vyema Mhe. Dkt. Mlyambina ambalo linatoka; Hesabu 17:8
“Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushindi; na
tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa
kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi na kuchanua maua; na
kuzaa malozi mabivu”.
Mhe. Madeha alifafanua neno hilo akisema kuwa “PhD”
aliyoipata Mhe. Dkt. Mlyambina itaendelea kukua na kuleta matunda chanya kwa Kanda kwakuwa
imewahamasisha wengine kujiendeleza zaidi kimasomo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina akifurahia keki ya pongezi aliyoandaliwa na Watumishi wa Kanda hiyo baada ya kutunukiwa Shahada la Uzamivu hivi karibuni.
Mhe. Dkt. Mlyambina akimlisha keki Inspekta Chodas kwa niaba ya Wadau wa Mahakama.
Zawadi maalum aliyokabidhiwa Mhe. Dkt. Mlyambina kama pongezi ya kuhitimu masomo yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni