Jumatatu, 5 Desemba 2022

‘UNHCR’ YAIUNGA MKONO MAHAKAMA YA TANZANIA MATUMIZI YA TEHAMA

Na Amani Mtinangi, Mahakama Kuu-Tabora 

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imepokea vitendea kazi vya TEHAMA kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kama sehemu ya kuanzisha ushirikiano wake na Mahakama hiyo kuunga mkono juhudi za Mahakama za kuboresha matumizi ya Mahakama Mtandao.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo hivi karibuni, Afisa Hifadhi Mshirika-UNHCR, Bi. Rehema Msami alisema kuwa, lengo la ziara yao ni ya kupanua shughuli zao na kwamba kwa kuanzia wametoa Kompyuta za kisasa za mezani mbili, ‘UPS’ mbili na printa mbili.

Bi. Rehema alisema kuwa, kwa siku za baadaye Shirika hilo litajielekeza pia kwa wadau wa Mahakama kadri ya upatikanaji wa fedha, huku akiongeza kwamba, kwa upande wa Kigoma programu hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wadau kama Polisi, Uhamiaji, Ustawi wa Jamii ni miongoni mwa Taasisi zinazofaidika na program hiyo.

Kwa pande wake Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadiru Juma aliishukuru UNHCR kwa kutoa vifaa na kusema kuwa wadau wengine ambao ni muhimu kufikiwa ni Mabaraza ya Ardhi ambayo mara nyingi husahaulika.

Kadhalika, Kaimu Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa wazo la UNHCR la kuisaidia Mahakama kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kufanya mafunzo kuhusu ukimbizi ni zuri kwa kuzingatia kuwa katika vyuo vingi nchini masomo ya wakimbizi sio ya lazima hivyo kuwafanya wanafunzi kutokuwa na ufahamu wa kina juu ya sheria za wakimbizi.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe alilishukuru Shirika hilo (UNHCR) kwa kuunga mkono juhudi za Mahakama ya Tanzania za kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa sababu kwa sasa TEHAMA ni nguzo muhimu katika utendaji wa shughuli za Mahakama.

 Aidha, Mhe. Mwakatobe alieleza pia wadau mbalimbali wa Mahakama wanakabiliwa na changamoto za vifaa hivyo hususani Magereza nyingi hazina vifaa hivyo au vilivyopo ni vichache ukilinganisha na mahitaji halisi, Gereza Kuu Uyui linalohudumia Wilaya za Tabora, Uyui na Sikonge lina seti moja ya vifaa vya Mahakama Mtandao jambo ambalo linakwamisha juhudi za usikilizaji wa Mashauri kwa njia ya mtandao panapotokea uhitaji wa Jaji au Hakimu zaidi ya mmoja wanapotaka kusikiliza mashauri kwa wakati mmoja.

Aliongeza kwamba, hali hiyo pia ipo katika Wilaya ya Kaliua ambayo haina Gereza na inatumia Gereza la Wilaya ya Urambo akasisitiza kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo ni muhimu sana.

Bi. Rehema Msami, Afisa Hifadhi Mshirika-UNHCR (wa mbele kushoto) akionesha hati za uhamisho wa mali baada ya makabidhiano ya vifaa vya TEHAMA kufanyika, kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadiru Juma akifafanua jambo wakati wa ugeni wa UNHCR.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe akisikiliza kwa makini maelezo ya Bi. Rehema Msami, Afisa Hifadhi Mshirika (hayupo katika picha) wakati wa ziara ya ugeni wa UNHCR.

Utiaji saini Hati ya Uhamisho: Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon (kulia) pamoja na Maafisa kutoa UNHCR wakielezana jambo kabla ya kusaini hati hiyo nyuma ni Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Niku Mwakatobe.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni