Jumatatu, 5 Desemba 2022

MSAJILI MKUU AHIMIZA WATUMISHI KUZINGATIA MAADILI POPOTE WALIPO

Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewataka watumishi wa Mahakama, hususani kutoka Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ili kujenga au kuongeza imani ya Mahakama kwa Umma na kuleta amani, utengamano kwa taifa na kukuza uchumi endelevu.

Mhe. Chuma ametoa wito huo leo tarehe 5 Disemba, 2022 wakati anawasilisha mada kuhusu Maadili ya Watumishi wa Umma na Maafisa wa Mahakama kwenye mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku tano kwa watumishi kutoka Mahakama hizo yanayofanyika kwenye Kituo cha Kigoma.

“Maadili katika kazi yana umuhimu mkubwa sana katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa wananchi. Maadili pia huongeza tija na, au ubora wa huduma, hulinda taswira ya Mahakama, hujenga na kuimarisha au kukuza mahusiano miongoni mwa watumishi na humwezesha mtumishi kutekeleza vema jukumu la utoaji haki,” alisema.

Msajili Mkuu huyo amewaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa kuzingatia maadili na kuwa waadilifu wakati wote kwa kuwahudumia wananchi kwa sababu wanawajibika kwao kwa vile wao ndio wanaofanya wawe katika maeneo yao ya kazi. “Tubadilike kifikra na kimtazamo. Tusifanye kazi kwa mazoea,” Mhe. Chuma alisisitiza.

Kwa mujibu wa Msajili Mkuu, Afisa wa Mahakama na yule asiye wa Mahakama anapaswa kuwa muandilifu katika kutelekeza majukumu yake na pia kuishi maisha yasiyokuwa na mashaka kimaadili.

Alisema kuwa eneo hilo la maadili ya watumishi wa umma na maafisa wa kimahakama ni suala mtambuka ambalo linalogusa maisha ya kila mtumishi wa umma ambapo Hakimu au Hakimu Mkazi pia ni mtumishi wa umma awapo kazini au nje ya kazi yake.

“Kutokana na sababu hiyo kuna haja ya kuielewa dhana ya neno maadili kwa upana wake. Hivyo, ni vema mtumishi wa kada yoyote akazingatia maadili ya kazi na hii inasaidia kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama,” alieleza.

Mhe. Chuma alifafanua kuwa maadili ni silaha ya kupambana na rushwa wakati wa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya utoaji haki, ambapo mtoa haki (Hakimu) anapaswa kuwa na tabia njema mbele ya jamii na hata awapo mwenyewe.

Alisema Hakimu hapaswi kuwa mvunja sheria kwa vile ni kioo cha jamii, uzingatiaji wake wa miiko na maadili ya kazi yake ni elimu tosha kwa jamii, hivyo anapaswa kufanya kazi ya uhakimu kwa kufuata maadili ya hali ya juu.

“Hakimu hatafuata au kuzingatia matakwa ya watu wachache au ahadi alizopewa katika utekelezaji wa jukumu la msingi la utoaji haki na Hakimu hataogopa kushutumiwa au kupoteza kazi ili mradi tu ametenda kazi yake vizuri kwa uadilifu,” Msajili Mkuu alisisitiza.

Kwa muktadha huo, Mhe. Chuma aliwahimiza watumishi hao kuepuka matendo au mwenendo unaoashiria vitendo vya rushwa, ikiwemo kuchelewesha usomaji wa hukumu na kusikiliza shauri upande mmoja bila kutoa sababu za msingi.

Kadhalika aliwaasa watumishi wasio maafisa wa Mahakama kuepuka matendo au mwenendo unaoashiria vitendo vya ukiukaji maadili na kuwa waadilifu katika kuwahudumia wananchi.

“Mnapaswa kuzingatia miiko na maadili ya kazi na kuwahudumia wananchi kwa kutumia lugha nzuri na bashasha (customer care) na mnawajibika kuwahudumia wateja wa Mahakama kwa wakati na bila kupendelea,” Mhe. Chuma alisema.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku tano kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika. Mafunzo hayo yameanza kutolewa leo tarehe 5 Disemba, 2022 kwenye Kituo cha Kigoma.
Sehemu ya watumishi kutoka Mahakama za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika (juu na chini) wakimfuatilia kwa makini Mhe. Chuma (hayupo kwenye picha) wakati akiwasilisha mada yake.

Sehemu nyingine ya watumishi kutoka Mahakama za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika (picha juu na mbili chini) wakimfuatilia kwa makini Mhe. Chuma (aliyesimama kushoto) wakati akiwasilisha mada yake.



Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jumanne Muna (aliyeshika tama) pamoja na watumishi wengine, akiwemo Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe Jovin Bishanga (aliyeshika mdomoni), wakifuatilia mada hiyo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni