Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha amewataka watumishi wanaohudhuria mafunzo
ya huduma kwa mteja katika Kituo cha Kigoma kutekeleza majukumu yao kwa ari
mpya ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kufikia malengo ambayo imejiwekea.
Akizungumza wakati anatoa neno la ufunguzi wa mafunzo ambayo yamewaleta pamoja watumishi 34 kutoka Mahakama za Wilaya tano za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika leo tarehe 5 Disemba, 2022 katika Kituo hicho, Mhe. Mlacha aliwahimiza washiriki hao kuwa wasikivu kwa vile yote watakayoelezwa na wawezeshaji ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Mahakama.
“Ni imani yangu na Mahakama kwa ujumla mtatoka
mkiwa watu wapya, ari mpya na uwezo mkubwa wa kufanya mambo ambayo yatakuwa
tofauti yatakayoiwezesha Mahakama ya Tanzania kuvuka na kufikia malengo ambayo imejiwekea,”
alisema.
Jaji Mfawidhi huyo alibainisha kuwa miongoni
mwa malengo na mbinu za kufanikisha utekelezaji wa Dira na Dhima ya Mpango
Mkakati wa Mahakama awamu ya pili 2020/2025 ni kuwajengea watumishi uwezo wa
kufanya kazi zao vizuri. Akaeleza kuwa ndio maana ikaamuliwa kabla ya kuanza
majukumu yao rasmi watumishi wa hizo Mahakama mpya wapewe mafunzo maalumu.
“Ni matarajio yangu baada ya mafunzo haya
kila mshiriki atakuwa ameiva kwa kubadilika kifikra, kimtazamo na weledi na
hivyo kuachana na utendaji wa kimazoea ambao ulichangia wananchi kukosa imani
dhidi ya huduma zetu,” alisema.
Mhe. Mlacha aliishushukuru Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha kupitia mkopo wa
Benki ya Dunia ili kugharamia uboreshaji wa huduma za Mahakama, yakiwemo
mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi watakaofanya kazi kwenye majengo ya
Mahakama mpya za Wilaya.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Wilbert chuma, akizungumza katika hafla hiyo fupi ya ufunguzi wa mafunzo
hayo katika Kituo cha Kigoma, amewahimiza watumsishi hao kuwa mabalozi na nuru
katika utendaji kazi.
Amesema mafunzo watakayopewa yakawe chachu
kwao katika kuleta mabadiliko chanya na yenye tija kifikra na kimtazamo, hivyo
kuacha kufanya kazi na kuwahudumia wananchi kwa mazoea.
“Uzuri wa majengo kama mlivyoyaona
unapaswa kusaili ubora wa huduma zetu, kwa maana huduma mnazotoa ziendane na
uzuri wa jengo. Haitoishi tu kuhudhuria mafunzo, elimu mtakayoipata muitumie
kubadilisha mitazamo,” Mhe. Chuma alisema.
Alibainisha kuwa uboreshaji wa miundombinu
unaoendelea hivi sasa ndani ya Mahakama ni utekelezaji wa nguzo ya kwanza ya Mpango
Mkakati wa Mahakama ambao unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi.
Msajili Mkuu alifafanua kuwa utekelezaji huo
unakutana na nguzo ya pili ya upatikananji wa haki, yaani utoaji wa huduma za
haki inayofikika na wananchi kupata huduma kwenye maeneo bora na wezeshi.
“Tunatambua uwepo wa matumizi ya Tekonolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yanarahisisha utoaji na upatikanaji wa
huduma. Usogezaji huo unaendana na huduma bora na zenye tija kwa wananchi, hivyo
kusaili nguzo ya tatu ya kurudisha au kujenga imani kwa umma,” alisema.
Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya
huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za
Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye
vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia
ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa
majengo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni