Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya
huduma kwa wateja ya siku 20 yenye lengo linaloelezewa kama ‘kuwabatiza’ upya watumishi
watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki
ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
tarehe 25 Novemba, 2022.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum mjini hapa
leo tarehe 5 Novemba, 2022, Mkurugenzi Msaidizi Mafunzo wa Mahakama ya
Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaandaa na
kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana
na uzuri wa majengo. Amesema mafunzo hayo yatatolewa kwenye Vituo vya Morogoro,
Kigoma, Bukoba na Musoma.
"Tayari tumeshaanza kutoa mafunzo
hayo kwenye Kituo cha kwanza cha Morogoro ambacho kimejumuisha watumishi 51
kutoka Mahakama za Wilaya tano za Gairo, Mvomero, Songwe, Kilindi na Kilombero.
"Leo tunaendelea na mafunzo haya
kwenye Kituo cha Kigoma ambayo kama ilivyokuwa Morogoro yatachukua siku tano
hadi Ijumaa tarehe 9 Disemba, 2022. Kituo hiki kina watumishi 34 ambao wametoka
katika Mahakama za Wilaya tano za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na
Tanganyika," alisema.
Kwa mujibu wa Bi. Ngungulu, baadaye
wataendelea kutoa mafunzo hayo kwenye Kituo cha tatu cha Bukoba kuanzia tarehe
12 hadi 16 Disemba, 2022 ambacho kina watumishi takribani 36 kutoka kwenye
Mahakama za Wilaya nne ambazo ni Misenyi, Kyerwa, Nyang'wale na Mbogwe.
Amesema mafunzo katika Kituo cha nne na
cha mwisho yatafanyika /’Musoma kuanzia tarehe 19 hadi 23 Disemba, 2022.
Mkurugenzi Msaidizi huyo amesema Kituo hicho kinachojumuisha Mahakama za Wilaya
nne za Busega, Itilima, Rorya na Butiama zenye watumishi wanaozidi 35.
"Tuna wawezeshaji wetu mahiri kutoka
ndani na nje ya Mahakama ambao wamebobea katika maeneo mbalimbali ambao
watawapitisha watumishi hawa katika mada kadhaa, ikiwemo Maadili na Kanuni za
Maadili katika Mahakama; Huduma kwa Mteja; Wajibu na Majukumu ya Mahakama za
Wilaya; Utamaduni wa Mahakama; Utii na Uvumilivu katika Mahala pa Kazi;
Mabadiliko maeneo ya Kazi na Uboreshaji wa Huduma za Mahakama," amesema.
Mada zingine zitakazowasilishwa kwenye
mafunzo hayo ni Matumizi ya Vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano;
Utunzaji wa siri; Uelewa wa Mpango Mkakati wa Mahakama; Upatikanaji wa Haki na Uaminifu
kwa Umma; Usimamizi Bora wa Mfumo wa Uendeshaji na Usajili wa Mashauri; namna
ya kukabiliana na msongo wa mawazo na zingine nyingi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa
Mahakama hizo 18 kwa mpigo iliyofanyika katika Mahakama ya Wilaya Busega ili
kuwakilisha Mahakama zingine 17, Jaji Mkuu aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kutambua changamoto ya ukosefu na uchakavu wa miundombinu ya Mahakama, hivyo
kuamua kuweka mipango ya ujenzi na ukarabati katika Mpango wake wa Maendeleo wa
Miaka Mitano.
“Serikali ya Tanzania inatambua kuwa
bajeti inayotoa kwa Mahakama isingeweza kuondoa changamoto kubwa ya uhaba na
uchakavu wa majengo. Hali hii iliilazimu Serikali kutafuta fedha za ziada nje
ya nchi ili kuondoa changamoto hizo,” alisema.
Aliishukuru Benki ya Dunia kwa kukubali kutoa mkopo wenye riba nafuu kwa Serikali ya Tanzania ambao umetumiwa na Mahakama ya Tanzania kujenga Mahakama hizo ili kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kupitia Programu ya Maboresho (Tanzania Citizen-Centric Judicial Modernisation and Justice Delivery Project).
Mkurugenzi Msaidizi Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu akifafanua jambo wakati wa mahojiano hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni