Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Mafunzo ya huduma
bora kwa mteja yaliyokuwa yanatolewa kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya
za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika kwenye Kituo cha Kigoma
yamehitimishwa leo tarehe 9 Disemba, 2022, huku Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akiwataka kubadilika na kutoa huduma mpya na bora
kwa wananchi.
Akizungumza wakati
wa kufunga mafunzo hayo, Mhe. Mlacha aliwaeleza washiriki hao kuwa ubora wa
majengo watakayokuwa wanayatumia kuwahudumia wananchi unatakiwa uakisi upya wao
kwa kila kitu, ikiwemo kutumia lugha nzuri, kuvaa vizuri na kutoa huduma bora
kwa ujumla.
“Jengo jipya,
huduma mpya. Kwa kuwa tunaenda kwenye majengo mapya lazima tuonyeshe upya wetu,
vinginevyo majengo hayo hayatakuwa na maana. Sisi tubadilike, tuchukue mtizamo
mpya tuweze kufanya kazi zetu vizuri na mwisho tuwe na Mahakama ya Tanzania
yenye mtizamo mpya, hasa katika kuimarisha imani kwa wananchi,” alisema.
Jaji Mfawidhi huyo
amewasisitiza watumishi hao kuendelea kutumia Teknoljia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zote za kimahakama. Amesema kila mmoja ana
wajibika kutekeleza mwelekeo huo kwa kuwa suala la matumizi ya TEHAMA
mahakamani halina mjadala kwa sasa.
“Sisi hapa Mahakama
Kuu Kigoma tumefikia asilimia 100 na hakuna kurudi nyuma kwa sababu kwa sasa
ndiko dunia inakokwenda. Wenzetu sasa wamefikia hatua ya kuwa na Mahakama
isiyotumia karatasi, hivyo lazima tubadilike na twende na mwelekeo huo,”
alisema.
Kadhalika, Jaji
Mfawidhi huyo amewahimiza watumishi hao kupendana wakiwa kazini, wamalize
tofauti zao na kuishi kama ndugu, kwani kwa kufanya hivyo majukumu yao yatakuwa
mepesi.
Amewapongeza
waandaaji na wawezeshaji wote wa mafunzo hayo kwa kazi nzuri waliyofanya ambayo
anaamini italeta matunda chanya katika utendaji kazi wa atumishi hao.
Naye mtumishi
kutoka Mahakama ya Wilaya Uvinza, Bw. Julius Manyanya, akiongea kwa niaba ya
washiriki wenzake, aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa fursa hiyo waliyopata ambapo
mafunzo waliyopatiwa yatakuwa chachu na hivyo kuboresha utandaji kazi katika
vituo vyao.
Katika kipindi
hicho cha siku tano, watumishi hao walipitishwa kwenye mada mbalimbali, ikiwemo
Maadili na
Kanuni za Maadili katika Mahakama; Huduma kwa Mteja; Wajibu na Majukumu ya
Mahakama za Wilaya; Utamaduni wa Mahakama; Utii na Uvumilivu katika Mahala pa
Kazi; Mabadiliko maeneo ya Kazi na Uboreshaji wa Huduma za Mahakama.
Mada zingine ni
Matumizi ya Vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano; Utunzaji wa siri;
Uelewa wa Mpango Mkakati wa Mahakama; Upatikanaji wa Haki na Uaminifu kwa Umma;
Usimamizi Bora wa Mfumo wa Uendeshaji na Usajili wa Mashauri na Namna ya
kukabiliana na msongo wa mawazo
Mada hizo ziliwasilishwa
na wawezeshaji wabobezi katika maeneo hayo, akiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Sharmillah Sarwatt, Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji wa Mahakama ya
Tanzania, Bw. Erasmus Uisso na Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi cha Mahakama ya
Tanzania, Mhandisi Yohana Mashausi.
Mahakama ya
Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi
watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki
ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo
ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga
kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi
zinazoendana na uzuri wa majengo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni