Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Mkurugenzi
wa Mipango na Ufuatiliaji wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso amewahimiza
watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na
Tanganyika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama kikamilifu katika maeneo yao
ya kazi ili kukidhi matarajio yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Bw. Uisso ametoa
wito huo leo tarehe 9 Disemba, 2022 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Mpango
Mkakati wa Mahakama (2021-2025) katika siku ya tano na ya mwisho ya mafunzo ya
huduma bora kwa mteja kwa watumishi kutoka Mahakama hizo kwenye Kituo cha
Kigoma.
“Kila mtumishi wa
Mahakama ana wajibu wa kutekeleza Mpango Mkakati kuanzia Mlinzi, Dereva, Karani,
Katibu Mahususi, Hakimu au Jaji. Ili kufanikisha mpango mkakati lazima
tufanye kazi kama timu. Mafanikio ya Jaji Kiongozi, Jaji Mfawidhi, Mtendaji
Mkuu yanategemea mchango wa kila mmoja katika Mahakama. Kila mmoja ana nafasi
yake katika utekelezaji wa mpango huo,” amesema.
Amewaeleza
watumishi hao kuwa katika kutekeleza Mpango Mkakati wa pili wanasisitiza zaidi
kwenye tunu za Mahakama hasa kwa kuzingatia uwepo wa maeneo mapya, mfano Buhigwe,
Kakonko, Uvinza, Kaliua, Tanganyika na mengine ambayo hayakuwa na Mahakama za
Wilaya na kwamba wananchi wangependa wapate huduma nzuri.
“Tuna tunu zetu za
Mahakama ambazo zinatuongoza kwenye kufikia maono yetu. Uadilifu, usawa kwa maana
ya kuhudumia wateja wote kwa usawa bila kuangalia kipato cha mtu au hadhi yake
katika jamii, ushirikiano kwetu sisi ndani ya Mahakama na wadau wetu, uwazi na
uwajibikaji,” Mkurugenzi huyo alisema.
Amewakumbusha washiriki
hao wa mafunzo kuwa wanatakiwa kufanya kazi kwa kulinda uhuru wa Mahakama, huku
wakitambua wakati huo huo kwamba wanapaswa kuwajibika kwa umma na kuwa na uwazi
katika kuendesha shughuli za kimahakama.
“Jambo jingine muhimu ni weledi, nisisitize kwenye eneo hili kuwa kuna baadhi ya watu wanafikiri weledi ni watu wa ngazi fulani, lakini weledi maana yake ni taaluma, kila mtu ana weledi katika eneo lake. Tukizingatia haya tutafikia mahitaji ambayo wateja wetu wanatarajia,” alisema.
Kadhalika, Bw. Uisso
alieleza mafaniko mengi yaliyofikiwa wakati wa kutekeleza Mpango Mkakati wa
Mahakama wa kwanza, ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya usikilizaji wa mashauri
ambayo ilipunguza mlundikano na kuongezeka kwa imani ya wananchi kwa Mahakama
kutoka asilimia 61 mwaka 2015 hadi asilimia 78 mwaka 2019 kulingana na utafiti
uliofanyika.
“Pia tumefanikiwa
katika kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kupitia ujenzi wa miundombinu na
ukarabati wa majengo katika ngazi mbalimbali za Mahakama. Moja ya maeneo ambayo
tumejenga ni pamoja na Mahakama Kuu Kigoma na majengo mapya ambayo watumishi
hawa wanaenda kuyatumia,” alisema.
Naye Mhandisi
Yohana Mashausi, akiwasilisha mada kuhusu Matumizi na Utunzaji wa Majengo
Mapya, aliwaomba watumishi hao kuzingatia matumizi bora ya miundombinu iliyopo
kwenye majengo ya Mahakama ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Mfano, watu
wanaweza kutoka kazini wakaacha feni zinawaka, hizo ni gharama zinaedelea
kutumika ukizingatia tuna ukomo wa matumizi ya fedha za umma. Hizi fedha kidogo
tunazotumiwa tunatakiwa kuzitumia vizuri, vinginevyo tunaweza kuyaona majengo haya
ni mzigo,” alisema.
Amewakumbusha kuwa
majengo hayo yamejengwa kwa gharama kubwa, hivyo ni matarajio ya Mahakama kuwa
yatatumika kwa kipindi kirefu kadri iwezekanavyo. Amesema kama majengo hayo
yatatumika vizuri hapatakuwa na ukarabati wa mara kwa mara.
Awali, akiwasilisha
mada kuhusu Msongo wa Mawazo na namna ya Kuzuia Hasira, Mshauli Mtaalam
Binafsi, Bw. Godfrey Wawa aliwaomba watumishi hao kupendana, kuheshimiana na kuzingatia
misingi ya kazi ili waweze kuthibiti na kujiepusha na msongo wa mawazo ambao
unaathari kubwa katika ufanisi kazini.
Alisema kuwa uwepo
wa msongo wa mawazo huathiri mtu binafsi, familia na hata taasisi anayofanyika
kazi, hivyo usipothibitiwa unaweza kuleta athari kubwa, ikiwemo uwezo wa mtu
kufikiri, hivyo kupelekea utendaji wa kazi kushuka.
“Naomba tupendane,
tuheshimiane kila mmoja kwa nafasi yake. Usijione wewe ni kiongozi ukawadharau
wengine. Kumbuka, yule Mfagiaji, Dereva au Mlinzi pale mlangoni anaweza kuwa
ana majibu ya changamoto yako,” Bw. Wawa aliwaambia watumishi hao.
Alisisitiza uvumilivu
mahala pa kazi kwa kuzingatia kuwa kila binadamu ana mapungufu yake na udhaifu
wake. “Kama binadamu, lazima kusameheana. Roho ya kuvumiliana na kusameheana ni
muhimu sana mahala pa kazi. Jifunze kuachilia mambo moyoni mwako, hii
itakusaidia sana kujiepusha na msongo wa mawazo,” alisema.
Kadhalika, Mtaalamu
huyo aliwaomba watumishi hao kuthibiti hasira zao wawapo kazini kwani kwa
kufanya vinginevyo wanaweza kuleta matokeo hasi, hivyo kuathiri mahusiano na
utangamano miongoni mwao na kuathiri utendaji kazi kwa ujumla.
“Hasira ni nzuri
wakati mwingine, kwa sababu inaweza kumfanya mtu kusema ukweli, kuondoa unafiki
na kumfanya yule anayesemwa kuchukua tahadhali au hatua sahihi. Lakini, hasira
isipothibitiwa inaweza kukuletea hasara, maumivu na kukutumbukiza kwenye
matatizo,” alisema.
Mahakama ya
Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma bora kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi
watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki
ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.
Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso akiwasilisha mada kwenye mafunzo yaliyowaleta pamoja watumishi kutoka Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika katika siku ya tano na ya mwisho kwenye Kituo cha Kigoma leo tarehe 9 Disemba, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni