Alhamisi, 8 Desemba 2022

UANGALIFU WASISITIZWA MATUMIZI YA MFUMO WA KUSAJILI, KURATIBU MASHAURI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma

Mkurugenzi Msaidizi katika Kurugenzi ya Kuratibu Mashauri ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Agness Mchome amewasisitiza watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika kuwa makini na waangalifu wanapotumia mfumo wa kuratibu na kusajili mashauri ili kuepuka makosa ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa katika mchakato mzima wa utoaji haki kwa wananchi.

Mhe. Mchome ametoa wito huo leo tarehe 8 Disemba, 2022 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Usimamizi Bora wa Mfumo wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (JSDS2) kwenye mafunzo ya huduma bora kwa mteja yanayotolewa kwenye Kituo cha Kigoma kwa watumishi kutoka Mahakama hizo za Wilaya.

Amebainisha baadhi ya makosa hayo, ikiwemo kukosea kuchagua masijala ya Mahakama, uingizaji usio sahihi wa taarifa muhimu, kuchelewa kulipa ada ya Mahakama, kuingiza tarehe na miaka isiyo sahihi au isiyo halisi kwenye mashauri, makosa ya kuandika isivyo majina ya wahusika, kuchelewa kujibu kwenye uandikishaji au usajili na kutokutembelea mfumo hadi wakati umekumbushwa.

“Nawahimiza muwe makini katika hili, kwani kosa lolote linaweza kusababisha madhara makubwa. Chukueni jitihada binafsi kujua mfumo huu vizuri. Nawaomba msiwe na mazoea ya kutoa haki zenu kwa mtu mwingine. Matumisi mazuri ya mfumo huu unapelekea uamuuzi ambao utatolewa kwa usahihi na wakati,” alisema.

Amewaeleza washiriki hao kuwa haki zilizotolewa kwa mtumiaji ni mahususi kwa ajili ya usimamizi rahisi na uwajibikaji ambapo haki hiyo ikitolewa mara moja haipaswi kushirikishwa kwa mtu mwingine. Amesema inapaswa kuwa tabia kwa watumiaji kutembelea mfumo huo mara kwa mara kwa madhumuni ya kushughulikia kazi zinazowasubiri.

Mhe. Mchome amesema kuwa kwa wasimamizi kutembelea mara kwa mara kutafanya iwe rahisi kwao kufahamu kinachoendelea katika maeneo yao mahususi, inapohitajika kusahihisha matatizo yoyote na usahihishaji wa ripoti hutegemea ufanisi wa kila mtumiaji wa mfumo.

Mwaka 2013 Mahakama ya Tanzania ilianzisha mfumo wa kuratibu na kusajili mashauri (JSDS1) ili kusaidia ukusanyaji wa taarifa za mashauri na utoaji wa takwimu zinazohitajika, ambapo kwa kiwango kikubwa mfumo huo ulikidhi matarajio.

Hata hivyo, mfumo huo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo teknolojia ya kizamani, kushindwa kutoa baadhi ya taarifa na urudufu wa data kwenye mfumo.

Kutoka na hali hiyo, mwaka 2018, Mahakama ya Tanzania ilitumia nguvu kazi ya teknolojia ya habari ya ndani kuboresha JSDS1 hadi JSDS2 ikiwa na vipengele vipya, ikiwemo kusajili mashauri kwa njia ya kielektroniki, malipo ya kielektroniki, uboreshaji wa usajili wa mashauri, mienendo na utoaji wa taarifa kupitia ujumbe mfupi kwenye simua.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.

Mkurugenzi Msaidizi katika Kurugenzi ya Kuratibu Mashauri ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Agness Mchome (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa ana wasilisha mada kwenye mafunzo ya watumishi kutoka Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika leo tarehe 8 Disemba, 2022.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka akitoa maelezo ya nyongeza baada ya Mhe. Mchome kuwasilisha mada yake.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanganyika, Mhe. Glory Mwakihaba akichangia jambo kabla ya Mhe. Mchome kumaliza kuwasilisha mada yake.
Mtumishi kutoka Mahakama za Wilaya Uvinza, Bw. Julius Manyanya akiuliza swali wakati wa uwasilishaji wa mada hiyo.
Baadhi ya watumishi wengine (juu na chini) wakiuliza maswali kwa mwezeshaji kabla ya kuhitimisha mada yake.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni