Alhamisi, 8 Desemba 2022

MHADHIRI CHUO CHA ESAMI AWAASA WATUMISHI KUZINGATIA UTU

Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma

Mafunzo ya siku tano ya huduma bora kwa mteja ambayo yamewaleta pamoja watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika katika Kituo cha Kigoma yameingia siku ya nne leo tarehe 8 Disemba, 2022 ambapo Mhadhiri huria wa Vyuo vya Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), ambaye pia ni Mshauri Mtaalam Binafsi, Bw. Endrew Msami amewaasa kutumia taaluma zao kwa ajili ya manufaa ya umma.

Akiwasilisha mada kuhusu ‘Kutoka kwenye Utu na Utendaji wa Kitaaluma’, Bw. Msami amewasihi watumishi hao kuzingatia utu kwanza wanapotekeleza majukumu yao na kuwatumikia wananchi kwa kutumia taaluma walizonazo kwa uaminifu na usawa huku wakiwajibika kwa Serikali na wananchi ili kuleta thamani iliyokusudiwa.

“Jiulize unataka nini kwenye jamii, ni urithi gani utaiachia jamii baada ya wewe kuondoka duniani, au unataka watu waje kwenye mazishi yako kuhakikisha kama kweli umekufa kutokana na matendo uliyowafanyia? Kama kuna kitu kizuri cha kuwaachia watoto wako ni utu na uaminifu ili mtu akija ofisini kwako aseme umelelewa vizuri na unaitendea haki taaluma yako,” alisema.

Bw. Msami, ambaye pia ni Mhadhiri huria katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, amewaeleza watumishi hao kuwa ni muhimu kutoa huduma ya kitaaluma ambayo imetukuka kwa nafasi ya kila mmoja wao na kwamba ni muhimu kwanza yule mtoa huduma kujitambua kwa kuelewa utu wake ni wa namna gani ili aweze kutumia utu huo uliosahihi kutoa huduma sahihi kwa watu tofauti tofauti anaokutana nao.

“Hili linakuja kwa yeye kutaka kwanza kumwelewa mteja kabla ya mteja kumwelewa mtoa huduma, ndipo hapo huduma itakayotolewa itakuwa sahihi. Hivyo, nawaomba muongeze uadilifu kwa kuwa wa kweli na wenye kutamani kutoa huduma iliyo sawa kwa wateja wenu wote bila kujali nafasi waliyonayo katika jamii kwa sababu katika jamii hakuna binadamu aliye mkubwa kuliko mwenzake,” alisema.

Mhadhiri huyo amewaeleza watumishi hao pia kuwa huduma siku zote inaenda ikitaka mabadiliko, hivyo ili waweze kutoa huduma inayoendana na wakati ni lazima wajifunze kubadilika kulingana na mazingira ya utoaji wa huduma inayobadilika kutokana  na mahitaji.

Amesema mahitaji ya wateja hayabaki vile vile, bali yanaenda yakibadilika kulingana na wakati. Hivyo, amewaomba kuendelea kuboresha taaluma zao ili kwenda na wakati kwa vile kuna mabadiliko mengi ambayo yanatokea duniani.

“Kwa hiyo, mtu wa mahakamani kama mtumishi anatakiwa kujifunza ili kuhakikisha huduma anayoitoa inaenda na wakati. Mara nyingi tunakataa mabadiliko, tusiogope. Ni vema kuwa tayari kukubaliana na mabadiliko ili kwenda na wakati wa dunia ya sasa,” Bw. Msami alisema.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo.

Mhadhiri huria wa Vyuo vya Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), Bw. Endrew Msami akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika katika Kituo cha Kigoma leo tarehe 8 Disemba, 2022.
Sehemu ya watumishi kutoka Mahakama za Wilaya za Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kaliua na Tanganyika (juu na chini) ikifuatilia mada hiyo.

Sehemu nyingine ya watumishi hao (juu na chini) ikimfuatilia kwa makini Bw. Msami alipokuwa anawasilisha mada yake.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni