Jumatatu, 12 Desemba 2022

MABADILIKO KIFIKRA, KIMTAZAMO YATAKIWA MAHAKAMA ZA WILAYA MPYA

Na Faustine Kapama-Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi amewataka watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’ware na Mbogwe kubadilika kifikra, kimtazamo na weledi na kuachana na utendaji kazi wa kimazoea ambao unachangia wananchi kukosa imani dhidi ya huduma zinazotolea na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya huduma bora kwa mteja kwa watumishi wa Mahakama hizo katika Kituo cha Bukoba leo tarehe 12 Disemba, 2022, Mhe. Banzi amewaasa kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wengine wa Mahakama mpya ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kufikia malengo ambayo imejiwekea ya kutoa huduma ya haki sawa kwa wote.

“Itakuwa ni jambo la ajabu mteja anapokuja akiwa na mtazamo chanya katika kupata huduma ikizingatiwa majengo yetu mapya yanavutia na yanapendeza alafu anapata changamoto za kuhudumiwa na watumishi kwa kukatishwa tamaa kwa kauli mbaya na huduma duni. Majengo mapya na bora ya kisasa ya Mahakama hizi hayatakuwa na maana yoyote kama huduma haitakuwa bora,” amesema.

Jaji Mfawidhi huyo amewaeleza washiriki hao kuwa mafunzo hayo ambayo yameandaliwa mahususi kwao ili kujiweka tayari kutoa huduma bora zinazokidhi viwango bora kwa kumlenga mteja ni mwendelezo wa juhudi za makusudi za Mahakama ya Tanzania pindi inapoboresha mazingira ya miundombinu na vitendea kazi, kuwaweka watumishi kuwa tayari kufanya kazi katika Mahakama wakiwa na fikra, maadili na mwanzo mpya katika kuwahudhumia wananchi.

“Ni imani yangu na Mahakama kwa ujumla baada ya mafunzo yanayoanza leo, mtatoka mkiwa watu wapya, ari na nguvu mpya na uwezo mkubwa wa kufanya mambo ambayo yatakuwa tofauti yatakayoiwezesha Mahakama ya Tanzania kuvuka na kufikia malengo ambayo imejiwekea,” amesema.

Mhe. Banzi amewakumbusha watumishi hao kuwa akiwa katika Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa awamu ya pili tarehe 21 Mei, 2021 wa miaka mitano (2020/2021-2024/2025) ambao ndio unatumika kama dira ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama na Programu ya Uboreshaji wa huduma za Mahakama kwa kuwa na umiliki (ownership) na uelewa wa pamoja kuhusu mipango iliyowekwa ili iweze kufikiwa kwa mafanikio na kuleta uboreshaji wa huduma za utoaji haki kwa wananchi.

Amesema kuwa katika nguzo ya tatu inayoelezea kuhusu imani ya wananchi na ushirikishwaji wa wadau (Public Trust and Stakeholder Engagement) ni mambo ambayo wote wanapaswa kuyazingazia kwa kuwahudumia wataja wao, ambao ni wananchi, kwa kufuata misingi ya haki, uwazi na upendo.

“Ni matarajio yangu baada ya mafunzo haya kila mshiriki atakuwa ameiva kwa kubadilika kifikra, kimtazamo na weledi na hivyo kuachana na utendaji wa kimazoea ambao unachangia wananchi kukosa imani dhidi ya huduma zetu. Mtambue kutorudi nyuma katika matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutokana na mabadiliko ya kidunia ambayo yanawalazimu wote kutorudi nyuma.

Jaji Mfawidhi huyo ametumia fursa hiyo adhimu kuishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kupitia mkopo wa Benki ya Dunia ili kugharamia uboreshaji wa huduma za Mahakama, yakiwemo mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi watakaofanya kazi kwenye majengo ya Mahakama mpya za Wilaya.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Amworo Odira, akizungumza katika neno lake la utangulizi aliwaeleza watumishi hao kukumbuka kuwa Mahakama inawekeza fedha nyingi kwenye mafunzo kwa matarajio ya kupata faida kama ambavyo mfanyabiashara hutarajia awekezapo kwenye biashara.

“Faida inayotarajiwa kwenu na Mahakama kwa ujumla ni kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anafanya kazi kwa weledi na kwa ubora tofauti na siyo kuwavunja moyo wananchi wanaofika mahakamani kupata huduma,” alisema.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick, Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jummane Muna aliwaeleza watumishi hao kuwa tarehe 25 Novemba, 2022 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma alizindua Mahakama mpya 18 zilizojengwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Amesema kuwa kufuatia uzinduzi huo, Mahakama imeandaa mafunzo ya huduma kwa mteja kwa lengo la kuwapatia ujuzi na kuwaandaa watumishi katika Mahakama hizo 18 kutoa huduma bora zitakazoendana na uzuri wa majengo yaliyozinduliwa.

“Mafunzo haya yamepangwa kufanyika katika vituo vinne vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma. Kwa kuanzia, mafunzo haya tayari yamefanyika katika Kituo cha Morogoro kuanzia tarehe 28 Novemba, hadi tarehe 02 Disemba, 2022 na kituo cha Kigoma kuanzia tarehe 05 Disemba, 2022 hadi tarehe 09 Disemba, 2022,” alisema.

Bw. Muna amesema kuwa ni matarajio ya Mahakama washiriki wote watakuwa makini kuwasililiza wawezeshaji na kuhakikisha wanaelewa yanayofundishwa ili hatimaye wakayatafsiri kwa vitendo kwa kutoa huduma bora na kwa weledi.

Katika kipindi hicho cha siku tano, watumishi hao watapitishwa kwenye mada mbalimbali, ikiwemo Maadili na Kanuni za Maadili katika Mahakama; Huduma kwa Mteja; Wajibu na Majukumu ya Mahakama za Wilaya; Utamaduni wa Mahakama; Utii na Uvumilivu katika Mahala pa Kazi; Mabadiliko maeneo ya Kazi na Uboreshaji wa Huduma za Mahakama.

Mada zingine ni Matumizi ya Vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano; Utunzaji wa siri; Uelewa wa Mpango Mkakati wa Mahakama; Upatikanaji wa Haki na Uaminifu kwa Umma; Usimamizi Bora wa Mfumo wa Uendeshaji na Usajili wa Mashauri na Namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano ya huduma bora kwa mteja kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’ware na Mbogwe ambayo yameanza leo tarehe 12 Disemba, 2022 katika Kituo cha Bukoba. 
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Amworo Odira akitoa neno la utangulizi wa mafunzo hayo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko akitoa utambulisho wa wageni mbalimbali katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jummane Muna akiwasilisha neno wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati) ikifuatilia mambo mbalimbali wakati wa ufunguzi huo. Wengine ni Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, Mhe. Monica Otaru (kulia) na Mhe. Emmanuel Ngigwana (kushoto).
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nyang'hwale. 
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mbogwe.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kyerwa.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Misenyi.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mahakama kutoka Makao Makuu na Kanda ya Bukoba.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculatha Banzi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo katika Kituo cha Bukoba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni