- Watumishi kutoka Mahakama za Wilaya Kyerwa, Misenyi, Nyang'hware na Mbogwe waanza kupokea 'dozi'
- Naibu Msajili asema maadili ya watoa huduma wa Mahakama huangaliwa popote walipo
Na Faustine Kapama-Mahakama, Kigoma
Mafunzo ya huduma
bora kwa mteja ya siku tano kwa watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa,
Misenyi, Nyangh’ware na Mbogwe yameanza leo tarehe 12 Disemba, 2022 katika
Kituo cha Bukoba huku watumsihi hao wakitakiwa kuzingatia maadili na kanuni zilizowekwa
na Mahakama ya Tanzania wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa
wananchi.
Akiwasilisha mada
ya kwanza kuhusu Maadili, Kanuni za Maadili na Utamaduni katika muktadha wa
Mahakama kwa watumishi hao, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi ya Usimamizi, Ukaguzi
wa shughuli za kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja amewaeleza washiriki
hao wa mafunzo kuwa maadili ni suala muhimu katika taasisi yoyote ili kuweza
kufikia malengo yake iliyojiwekea.
“Maadili
yanatofautiana kutokana na mazingira, au aina ya kazi. Mahakama kama zilivyo
taasisi au mihimili mingine ina maadili na kanuni zinazoongoza mienendo na
tabia za watoa huduma wake. Lengo hapa ni kuongeza kiwango cha kutoa huduma
bora kwa wananchi na yule tunayemhudumia aridhike. Hatuwezi kufanya haya
tusipozingatia maadili na kanuni zilizopo,” alisema.
Amesisitiza kuwa
ni muhimu kwa mtumishi wote wa Mahakama, yaani maafisa wa kimahakama (Judicial
officers) na wasio wa kimahakama (non-Judicial officers) kuwa wadilifu kwa
kuzingatia kanuni zinazoongoza utendaji wao wa kazi wakati wote wakiwa kazini
au nje ya kazi. Amesema kuwa maadili ya watoa huduma wa Mahakama hayaangaliwi
tu wakati wakiwa kazini, bali pia huangaliwa hata wakiwa nje ya kazi.
“Kutokuzingatia
maadili kuna athari sana kwenye huduma tunazozitoa hata kama tukiwa kwenye shughuli
zetu za kawaida. Kwa hiyo ni vizuri kuyazigatia mkiwa kazini na nje ya kazi, hakikisheni
mnalinda taswila nzuri ya Mahakama kwa kadri inavyotakiwa,” alisema Mhe. Minja.
Amesema uwepo wa
maadili mahala pa kazi ni muhimu kwa kuwa huongeza tija na, au ubora wa huduma,
hujenga au kuongeza imani ya Mahakama kwa umma, hulinda taswira ya Mahakama, hujenga
na kuimarisha au kukuza mahusiano miongoni mwa watumishi, huleta amani na
utengamano kwa taifa ili kukuza uchumi endelevu na humfanya mtumishi kutekeleza
vema jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Hivyo, akawasihi maafisa kutoka katika Mahakama hizo mpya za Wilaya kuwa waadilifu wa ghali
ya juu, kusimamia uhuru wa uamuzi wao, kuenenda kulingana na kanuni
zinazokubalika, kuwa na weledi na bidii, au umakini wanapotekeleza majukumu yao,
kuzingatia usawa na kutokuwa na
upendeleo.
“Nafasi ya Hakimu
katika jamii ni nyeti sana na maadili yake hayapaswi kutiliwa mashaka. Hakimu ni kioo cha
jamii, uzingatiaji wake wa miiko na maadili ya kazi yake ni elimu tosha kwa
jamii. Mtoa
haki (Hakimu) anapaswa kuwa na tabia njema mbele ya jamii na hata awapo
mwenyewe, hivyo hatakiwi kuwa na mwenendo au matendo yanayoashiria rushwa na hatafuata
maelekezo au ahadi alizopewa katika utekelezaji wa jukumu la msingi la utoaji
haki,” alisema.
Kadhalika, Mhe.
Minja aliwaeleza washiriki hao wa mafunzo kuwa watumishi wasio maafisa wa
Mahakama wanapaswa kuepuka matendo au mwenendo unaoashiria vitendo vya ukiukaji
maadili, kuwa waadilifu katika kuwahudumia wananchi, kuzingatia miiko na
maadili ya kazi na kuwahudumia wananchi kwa kutumia lugha nzuri na bashasha
(customer care) na pia kuwahudumia wateja wa Mahakama kwa wakati na bila
kupendelea.
“Maadili ni sehemu
ya maisha yetu wakati wote, tukiwa kazini na nje ya kazi. Kwakuwa tumechagua
kuwa katika familia hii ya utoaji haki basi tutekeleze wajibu wetu kwa
kuhakikisha tunatoa huduma bora,” Naibu Msajili huyo aliwaambia watumishi hao.
Mahakama ya
Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi
watakaohudumu katika Mahakama mpya za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa
Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo. Tayari mafunzo hayo yameshatolewa kwenye Vituo vya Morogoro na Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni