·Mwanasaikolojia awasihi
wajibebe kama wanataka kufanikiwa
Na Faustine
Kapama-Mahakama, Bukoba
Mafunzo ya huduma bora ya siku tano kwa
mteja kwa watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa,
Misenyi, Nyangh’ware na Mbogwe yameingia siku ya pili leo tarehe 13
Disemba, 2022 katika Kituo cha Bukoba huku watumsihi hao wakitakiwa kuzingatia kanuni,
taratibu na sheria mbalimbali zinazosimamia utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka
ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania,
Bw. Malimo Manyambula alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Utunzaji
wa Nyaraka na Kumbukumbu katika mafunzo hayo. Alisema utunzaji mbaya wa kumbukumbu
na nyaraka huhatarisha usalama wake.
“Tuna sheria na sera za nchi na taratibu
zetu za ndani ambazo zinatayarishwa na Jaji Mkuu au Mtendaji Mkuu au Msajili
Mkuu kuhusiana na masuala hayo. Watu wanatakiwa wazingatie taratibu hizo kwa
wakati. Inapotokea mtu hatekelezi maana yake anakuwa anaenda kinyume na hizo
taratibu, hivyo kuhatarisha usalama wa kumbukumbu zetu,” amesema.
Katika mada yake, Bw. Manyambula aliwapitisha
washiriki hao wa mafunzo kwenye suala zima la utunzaji wa kumbukumbu kutoka
zinapozalishwa, zinapotumika na wakati zinapotumika zinatunzwaje na mpaka zinapofikia ukomo, yaani jalada
linapokuwa limefungwa.
“Nia kubwa ni kuhakikisha tunakuwa na
utunzaji sahihi wa kumbukumbu ambao utaleta matokeo chanya ya kutoa uamuzi ulio
sahihi na unaopatikana kwa wakati. Kumbukumbu sahihi zinapoenda kwa mtu sahihi,
basi atatoa uamuzi sahihi na kwa wakati kwa sababu hakutakuwa na ucheleweshaji
wowote. Lakini ukipeleka kumbukumbu ambazo siyo sahihi au ni sahihi lakini siyo
kwa mhusika kutakuwa na ucheleweshaji wa kutoa uamuzi,” alisema.
Mkurugenzi huyo aliwakumbusha watumishi
hao utaratibu wa kufungua na utunzaji wa majalada kwa mujibu wa taratibu
zilizoelezwa kwenye Mwongozo wa Masjala katika ofisi za umma na kusisitiza kuwa
ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kila Idara au Kitengo kinatakiwa kuwa
na majalada yanayohusu kazi zao.
Aliwaeleza washiriki hao wa mafunzo baadhi
ya madhara ya kutozingatia mwongozo wa kufungua na kutunza majalada, ikiwemo
kuchelewesha utoaji wa uamuzi au kutoa uamuzi usiosahihi, menejimenti kutokuwa
na ufahamu wa kutosha wa kazi za taasisi na uvujaji wa siri za Serikali.
Naye Mwanasaikolojia, Bi. Sadaka Gandi,
akiwasilisha mada kuhusu Uaminifu, Uvumilivu na Saikolojia mahali pa kazi
katika mafunzo hayo, aliwasihi watumishi katika Mahakama mpya za Wilaya za
Kyerwa, Misenyi, Nyangh’ware na Mbogwe kujitafakari na kujibeba kama wanataka
kufanikiwa wanapotekeleza majukumu yao mbalimbali mahakamani.
“Binadamu anatakiwa kujibeba mwenyewe,
kubeba wengine na kuruhusu wengine wajibebe wenyewe. Hii ina maana kuwa na
uwezo wa kujitambua, kuweza kuwaelewa na kuwavumilia wengine, kuwa na uwezo wa
kuvaa viatu vya wengine na maisha yakaendelea. Jipambanue ili uweze kufurahia
maisha, jua jinsi ya kuthibiti hisia zako na chukua muda kidogo kabla ya kuchua
uamuzi wowote,” alisema.
Mwanasaikolojia huyo amewaomba washiriki
hao wa mafunzo kuwa na mtizamo chanya wanapotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia
kuwa Mahakama ya Tanzania inahitaji watumishi wenye mitizamo iliyopevuka.
“Mtizamo wa mtu mmoja unaweza kuathiri
kila mtu katika taasisi. Ukiwa na mtu mwenye mtizamo mbaya atawavuruga tu
kwenye taasisi yenu na mtapaona mahali pa kazi pabaya. Kuimarisha mitizamo
chanya mahali pa kazi italeta manufaa kwa waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa
ujumla. Hivyo, mtizamo chanya ni muhimu kama tunataka kutekeleza majukumu yetu kwa
matarajio ya taasisi yetu,” amesema.
Bi. Gandi ameeleza faida za mtu mwenye
mtizamo chanya ni kuwa na heshima kwa wengine, kuwa na shauku ya kuambukiza
mambo mema kuhusu maisha, kujitolea kufanya kazi, kuwa na mawazo ya ubunifu na
kuwasaidia wengine. Amesema mambo hayo yote ni muhimu kwa mtumishi kuwanayo
mahali pa kazi.
Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya
huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama mpya za
Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye
vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia
ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa
majengo. Tayari mafunzo hayo yameshatolewa kwenye Vituo vya Morogoro na Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni