Na Faustine Kapama-Mahakama, Bukoba
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah
Sarwatt amewataka watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya
za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe kuwatumikia Watanzania kwa bidii
na weledi wa hali ya juu huku wakitoa kipaumbele kwa mwananchi kwani ndiyo muhimu katika muktadha mzima wa uwepo wa Mahakama ya Tanzania hapa nchini.
Akiwasilisha mada kuhusu Wajibu na
Majukumu ya Watumishi katika Mahakama za Wilaya kwa watumishi wa Mahakama hizo kwenye mafunzo yanayofanyika katika Kituo cha Bukoba, Mhe. Sarwatt alisema kuwa mwananchi
ndiye kipaumbele cha kwanza kwa Mahakama kwa vile ndiye aliyesababisha kuwepo utekelezaji
wa mradi wa maboresho unaoendelea.
“Mwananchi ndiye kipaumbele chetu, ndiye
anayetufanya tuamke asubuhi kwenda kazini. Kila mwananchi anayekuja mahakamani
ndiye anayekusababisha uwepo hapo. Kama wananchi walikuwa hawahitaji huduma
zetu tusingejenga Mahakama hizi zote. Kwa hiyo, mawazo yetu, ubunifu wetu
umlenge huyu mwananchi. Tunataka mwananchi ajione ana bahati kuzaliwa Tanzania,”
alisema.
Msajili wa Mahakama Kuu huyo aliwaeleza watumishi
hao kuwa Mahakama hizo wanazokwenda kufanya kazi hazikujengwa hivyo kwa bahati
mbaya bali zimekuja kwa malengo maalumu, ikiwemo kuwezesha haki kupatikana kwa
wakati na kuongeza ufanisi na huduma bora kwa wananchi.
“Majengo haya yana vipengele vya kipekee
kuwawezesha wadau wengi kukutana katika sehemu moja. Tunataka mwananchi asisumbuke
tena, akihitaji huduma ya mwendesha mashtaka aipate, akihitaji msaada wa
kisheria aupate. Kama nyinyi Mahakimu Wafawidhi hamjawaalika wadau hawa
fanyeni sasa,” alisema.
Mhe. Sarwatt amewaeleza watumishi hao kuwa
majengo hayo pia yamekuja na aina mpya ya utendaji kazi, hivyo wanapaswa kuacha
kufanya kazi kwa mazoea. Amewakumbusha
kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao wakiwa katika Mahakama hizo mpya
kwani hakutakuwepo na kisingizio chochote cha kutoa huduma isiyoridhisha kwa
wananchi.
“Tunategemea uwazi wa hali ya juu
mnapotekeleza majukumu yenu. Haitakiwi kabisa kuonekana kuwa na hata dalili
zozote za tuhuma yoyote. Kipaumbele chetu ni mwananchi, hata kama una matatizo
yako, yule mwananchi yanamhusu nini, kuna uhusiano gani wa changamoto zako na
mwananchi. Tunataka huduma itolewe kwa wakati na bora na hakuna sababu yoyote ya
kutokufanya haya,” alisema.
Naye Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Kitengo
cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Edward Mpabansi, akiwasilisha mada
kuhusu Tathimini ya Mpango Mkakati wa Mradi wa Maboresho wa Mahakama ya
Tanzania kwenye mafunzo hayo, alisema Mahakama ya Tanzania imejiwekea Mpango
Mkakati kama nyenzo ya kuhakikisha inafikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya
Taifa.
Alisema kulikuwepo na Mpango Mkakati wa
kwanza uliotekelezwa kuanzia mwaka 2015/2016 na kukamilishwa mwaka 2019/2020 ukiwa
na nguzo tatu, Utawala, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali; Upatikanaji wa Haki na kwa Haraka
na Kuongeza Imani ya Wananchi kwa Mahakama na Kushirikisha Wadau. Amesema kwa
sasa Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa pili (2020/2021-2024/2025
ukiwa na nguzo hizo tatu.
Mhe. Mpabansi amewaeleza washiriki hao wa
mafunzo kuwa katika kutekeleza mpango mkakati wa kwanza, Mahakama imefanikiwa
katika maeneo mengi, ikiwemo uwepo wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha utoaji wa huduma na jinsi Mahakama
inavyotumia teknolojia hiyo katika utoaji haki kwa wakati.
“Kumekuwepo na ufunguaji wa mashauri
kimtandao, kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao (video conferencing), kupandisha
uamuzi katika mtandao ambapo jumla ya mashauri 3,271 ya Mahakama ya Rufani
yalipandishwa hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2021, huku jumla ya mashauri
12,137 ya Mahakama Kuu, 748 Divisheni ya Biashara, 797 Divisheni ya Kazi, 1,981
Divisheni ya Ardhi na 204 ya Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi yakipandishwa,”
alisema.
Ametaja baadhi ya mafanikio mengine kama kupunguza
mlundikano wa mashauri kutoka asilimia 13 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia tisa
kufikia Septemba 2022, kanzishwa kwa huduma ya Mahakama inayotembea (Dar es
Salaam na Mwanza), kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi wa Mahakama katika
ngazi zote, ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita kwa mikoa ya Arusha,
Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Dodoma, Morogoro na Mwanza, ujenzi wa
Mahakama Kuu mbili za Kigoma na Mara na
ujenzi wa Mahakama mpya 18 katika Wilaya mbalimbali mpya na za zamani.
Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya
huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama mpya za
Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye
vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia
ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa
majengo. Tayari mafunzo hayo yameshatolewa kwenye Vituo vya Morogoro na Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni