Jumatano, 14 Desemba 2022

‘MAHAKAMANI MAHALI SALAMA PAKUPATA HAKI’

Na Faustine Kapama-Mahakama, Bukoba

Mafunzo ya huduma bora kwa mteja ya siku tano kwa watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe yameingia siku ya tatu leo tarehe 14 Disemba, 2022 katika Kituo cha Bukoba huku watumishi hao wakihimizwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuwafanya wananchi waone mahakamani ni mahali salama, hivyo kuondoa dhana kuwa Mahakama kazi yake ni kufunga watu.

Akiwasilisha mada kuhusu Mkataba wa Huduma kwa Mteja (Judiciary Clients Service Charter) katika mafunzo hayo, Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jumanne Muna aliwaambia watumishi kutoka Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe kuwa Mahakama imeweka mkataba na umma na wadau kwa ujumla kwa kujielekeza kupata huduma mbalimbali za Kimahakama na kutambua kwamba Mahakama ndio kimbilio la kupata haki zao na huduma mbalimbali za kisheria, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuutekeleza mkataba huo bila kigugumizi cha aina yoyote.

“Tumeutangazia umma kuwa tunao mkataba wa huduma kwa mteja. Tunataka wananchi watambue kuwa mahakamani ni mahali salama pa kupata haki. Wengi wanajua Mahakama kazi yake ni kufunga watu, lakini kumbe ni sehemu pekee ambayo mwananchi anaweza kupata haki yake. Tunajipambanua kuwa tunatoa haki sawa na kwa wakati, hivyo hatuna budi kutekeleza majukumu yetu kikamilifu,” alisema.

Ametaja baadhi ya madhumuni ya mkataba huo, ikiwemo kuufahamisha umma kuhusu huduma na viwango tarajiwa kutoka kwa Mahakama; kumjali mteja na makundi maalumu kwa kuwapa kipaumbele wakati wa kutoa huduma; kuboresha utoaji huduma kutokana na mrejesho; kuongeza uwajibikaji wa watumishi katika kuwahudumia wananchi kwa viwango vilivyowekwa; kubainisha haki na wajibu wa wateja ili kupata huduma bora kulingana na matarajio na kuweka mfumo wa mawasiliano na kutoa mrejesho.

Bw. Muna amewakumbusha watumishi hao baadhi ya huduma ambazo wanapaswa kuzitoa kwa wateja, ikiwemo kutoa kalenda ya shughuli za Mahakama; kutoa ratiba ya kusikiliza mashauri; kupokea, kusajili na kusikiliza mashauri; kutayarisha na kusoma uamuzi; kutoa nyaraka za Kimahakama na kuthibitisha nyaraka mbalimbali; kutekeleza na kukaza hukumu, amri na uamuzi wa Mahakama na kutoa hati za adhabu.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kutekeleza majukumu ya Mahakama na kuhakikisha kuwa tunazingatia viwango vilivyobainishwa na kutoa huduma kwa ubora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya mteja. Tuna jukumu la kuijenga taswira ya Mahakama na kurudisha imani kwa wananchi,” alisema.

Naye Mhadhiri huria wa Vyuo vya Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), ambaye pia ni Mshauri Mtaalam Binafsi, Dkt. Andrew Msami, akiwasilisha mada kuhusu ‘Kutoka kwenye Utu na Utendaji wa Kitaaluma’, aliwaomba washiriki hao wa mafunzo kubadilika kama watumishi mmoja mmoja ili waweze kuleta mabadiliko mapana katika huduma za kimahakama.

Amewasihi kutokuwa na mitazamo hasi kwa wateja wanaokuja mahakamani na kuchagua aina ya huduma ambazo wanastahili kupata. Dkt. Msami amesema kuwa mtazamo wa aina hiyo huathiri huduma ambayo inatakiwa kutolewa kwa mteja.

“Ukifikiria kwamba huyu mtu ni dhaifu na haelewi anachokitaka tayari inakupa hisia kwamba huduma utakayompa itakuwa imeshuka kwa sababu ya hisia za dharau ambazo umekuwa nazo tayari. Kwa hiyo, natamani kama watumishi wa Mahakama katika ngazi zote muone kwamba huduma haiendani na muonekano wa mtu, bali inaendana na uhitaji alionao na huo uhitaji ndio ambao mtoa huduma anatakiwa kuangalia zaidi ya muonekano wa huyo mtu,” alisema.

Mada nyingine iliyowasilishwa siku ya leo ilihusu Matumizi ya Vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama. Mada hiyo iliwasilshwa na Afisa TEHAMA kutoka Kanda ya Bukoba, Bw. Ahmed Mbilinyi kwa niaba ya Kurugenzi ya TEHAMA ya Mahakama ya Tanzania.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama mpya za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo. Tayari mafunzo hayo yameshatolewa kwenye Vituo vya Morogoro na Kigoma.

Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Jumanne Muna (juu na chini) akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya huduma bora kwa mteja kwa watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa, Missenyi, Nyangh’wale na Mbogwe yanayofanyika katika Kituo cha Bukoba.

Mhadhiri huria wa Vyuo vya Mafunzo ya Utawala Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI), ambaye pia ni Mshauri Mtaalam Binafsi, Dkt. Andrew Msami akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Afisa TEHAMA kutoka Kanda ya Bukoba, Bw. Ahmed Mbilinyi akitoa 'dozi' kwa washiriki wa mafunzo hayo.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni