Alhamisi, 15 Desemba 2022

MKURUGENZI USIMAMIZI MASHAURI AHIMIZA USAHIHI UHUISHAJI WA TAKWIMU KWENYE MFUMO

Na Faustine Kapama-Mahakama, Bukoba

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha amewahimiza watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe kuwa waangalifu wanapoingiza taarifa kwenye mfumo wa menejimenti ya mashauri ili kuwa na takwimu sahihi.

Mhe. Kamugisha ametoa wito huo leo tarehe 15 Disemba, 2022 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Usimamizi Bora wa Mfumo wa Menejimenti ya Mashauri (JSDS2) katika siku ya nne ya mafunzo ya huduma bora kwa mteja yanayotolewa kwa watumishi hao kwenye Kituo cha Bukoba.  

Amesema uhuishaji wa taarifa kwa wakati na usahihi kwenye mfumo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa kumekuwepo na makosa ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakifanywa na watumishi ndani ya Mahakama wakati wa kuhuisha mfumo huo, hivyo kusababisha kuwepo kwa kumbukumbu ambazo siyo sahihi.

“JSDS2 inabaki kuwa mfumo wetu wa usimamizi wa mashauri na chanzo kikuu cha takwimu za taasisi. Ukweli wa taarifa inayotolea na mfumo mzima inategemea usahihi wa kumbukumbu iliyohuishwa. Kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa mfumo huchangia kwa kiasi kikubwa usahihi wa kumbukumbu,” Mkurugenzi huyo alisema.

Amesisitiza usahihi wa uhuishaji wa taarifa kwenye mfumo wa menejimenti ya mashauri kwa sababu kinyume chake hupelekea uwepo wa kumbukumbu ambazo siyo sahihi. Mhe. Kamugisha amesema hakuna kitu kibaya kama kupotosha takwimu kwa sababu JSDS2 ndiyo mfumo mama wa utoaji wa takwimu za mashauri mahakamani.

“Kwa hiyo, kama ule mfumo umeingizwa taarifa ambazo siyo sahihi ina maana hata takwimu utakazozipata zitakuwa siyo sahihi. Takwimu kwa sasa ndiyo zinazotumika katika mipango na ili uweze kupanga vizuri lazima uwe na takwimu. Kwa hiyo, usipokuwa na takwimu sahihi huwezi kupanga sahihi,” alisema.

Kadhalika, Mkurugenzi huyo amewahimiza watumishi kutoka Mahakama hizo kuhuisha taarifa za mashauri kwa wakati kwa kuwa mfumo wa JSDS2 ndiyo unaotoa takwimu zilizopo. “Tunachotaka kwa sasa mahakamani ni kupata takwimu kwa wakati huo huo, kwa hiyo kama shauri likiisha lazima mfumo huo uhuishwe,” amesema.

Mhe. Kamugisha amesisitiza pia kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za Mahakama. Amesema Mahakama inapokwenda kuwa na mifumo mingine, itakuwa vigumu kwa watumishi hao kwenda na mifumo ya kimahakama bila kuwa na ujuzi wa kawaida wa matumizi ya TEHAMA. “Hivyo mnatakiwa kuwa karibu na teknolojia hiyo ambayo ndiyo mwelekeo wa Mahakama kwa sasa,” amesisitiza.

Naye Mshauri Mtaalam Binafsi, Bw. Godfrey Wawa, akiwasilisha mada kuhusu Msongo wa Mawazo na namna ya Kuzuia Hasira katika mafunzo hayo, aliwasihi watumishi hao kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo msongo wa mawazo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amewaeleza kuwa msongo wa mawazo usipothibitiwa huweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kupata shinikizo la damu, shinikizo la moyo na hata kuathiri afya ya akili, hali ambayo inaweza kupunguza uwezo wa kufanya kazi.

Bw. Wawa amewashauri watumishi hao kutafuta mbinu mbalimbali chanya za kukabiliana na msongo wa mawazo, ikiwemo kupata muda wa kupumzika, kujichanganya na marafiki pamoja na familia na pia kufanya mazoezi ili kuburudisha akili ya mwili.

“Katika maisha kuna kitu kinaitwa kiasi. Fanya kazi sana, lakini kumbuka wewe ni binadamu, unahitaji kupumzika. Kuna wakati wa kazi na kuna wakati wa kupumzika. Kumbuka una familia na marafiki, jichanganye ili akili yako ikae sawa. Wewe kama mfanyakazi unatakiwa uwe na afya ya akili ili mwajiri wako aweze kupata matunda anayotarajia kutoka kwako,” aliwaambia watumishi hao.

Ametaja baadhi ya visababishi vya msongo wa mawazo kama mabadiliko ya mazingira, majukumu fulani kazini, mahusiano ya kifamilia au kikazi, shughuli za kila siku, changamoto za kifedha na za kiafya pamoja na hali ngumu ya maisha. Hivyo amewashauri kupambana na msongo wa mawazo ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika maisha.   

Jana jioni tarehe 14 Disemba, 2022, washiriki hao wa mafunzo walipitishwa kwenye mada zingine mbili, ikiwemo Uelewa wa Mpango Mkakati wa pili wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2020/2021-2024/2025) iliyowasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi Bajeti na Mipango katika Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji, Bi. Gladys Qambaita. Mada nyingine ilihusu Matumizi na Utunzaji wa Majengo Mapya iliyowasilishwa na Mhandisi Yohana Mashausi.

Mahakama ya Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi watakaohudumu katika Mahakama mpya za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi zinazoendana na uzuri wa majengo. Tayari mafunzo hayo yameshatolewa kwenye Vituo vya Morogoro na Kigoma.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kwenye mafunzo ambayo yamewaleta pamoja watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe katika Kituo cha Bukoba leo tarehe 15 Disemba, 2022.


Mshauri Mtaalam Binafsi, Bw. Godfrey Wawa, akiwasilisha mada kuhusu Msongo wa Mawazo na namna ya Kuzuia Hasira katika mafunzo hayo.

Mkurugenzi Msaidizi Bajeti na Mipango katika Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji, Bi. Gladys Qambaita akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Mhandisi Yohana Mashausi akifurahia jambo alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Matumizi na Utunzaji wa Majengo Mapya kwenye mafunzo hayo.
Sehemu ya watumishi kutoka Mahakama mpya za Wilaya za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe (juu na chini) ikifuatilia uwasilishaji wa mada hizo.

Sehemu nyingine ya watumishi kutoka Mahakama hizo mpya (juu na chini) ikifuatilia uwasilishaji wa mada kutoka kwa wawezeshaji hao.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni