Na Faustine Kapama-Mahakama, Bukoba
Mafunzo ya huduma
bora kwa mteja yaliyokuwa yanatolewa kwa watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya
za Kyerwa, Misenyi, Nyangh’wale na Mbogwe yamehitimishwa leo tarehe 16 Disemba,
2022, huku Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Emmanuel Ngigwana, akiwataka kutoa huduma bora
kwa wananchi ili kuifanya Mahakama ya Tanzania kufikia malengo ambayo
imejiwekea ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Akizungumza wakati
wa kufunga mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza tarehe 12 Disemba, 2022 katika
Kituo cha Bukoba, Mhe. Ngigwana aliwasihi washiriki hao kuzingatia mambo matatu
muhimu wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kumtanguliza Mungu, kuzingatia maadili
kazini na kuwa na bidii ya kazi.
“Ukimtanguliza
Mungu utakuwa na hofu ya Mungu na utafanya ukijua kwamba kuna siku ukiwa Hakimu
au mtu mwingine yoyote utasimama kutoa hesabu ya kazi uliyofanya duniani. Hivyo
sisi tuchague kuwa na Mungu na tutende mema,” alisisitiza.
Jaji huyo pia
aliwaasa kuzingatia maadili ya kazi kwa kuepuka kufanya mambo ambayo yanaweza
kuleta doa au kusababisha maadili yao kuwekewa maswali, ikiwemo kujihusisha na
vitendo vya rushwa. Amewakumbusha kuwa wao ni kioo cha jamii, hivyo wanapaswa
kuwahudumia wananchi kwa kutumia lugha nzuri na bila kinyongo chochote.
Kadhalika, Mhe. Ngigwana
amewasihi kufanya kazi kwa ushirikiano ili waweze kufanya kazi kama timu moja
ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa. Amesema kuwa wasifanye kazi kwa
kukumbushwa na viongozi wao, bali wajitume kwa kile wanachotakiwa kufanya.
Mhe. Ngigwana
amewasihi watumishi hao kuyatafsiri mafunzo waliyoyapata kwa vitendo ili kuleta
mabadiliko chanya katika Mahakama kwa kuwahudumia wananchi. “Tuepuke utendaji
wa kimazoea ambao tulikotoka ulileta taswira ya kulalamikiwa na wateja,”
alisisitiza.
Alitumie fursa hiyo
kuishukuru Serikali na Mahakama kwa ujumla kwa kuendelea kuwajengea uwezo
watumishi wa Mahakama ili uboreshaji wa huduma unaoendelea katika miundombinu ufanyike
pia katika kuwabadilisha watumishi kimtazamo, kifikra na kiutendaji.
“Tunatamani sana
waandaaji wa mafunzo haya yasiishie kwa watumishi wa Mahakama mpya tu, bali pia
yaendelee hata kwa watumishi wote kadiri mtakayopata fedha,” Mhe. Ngigwana
alisema.
Wakati wa
kumkaribisha Jaji Ngigwana kuzungumza na watumishi hao, Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, Mhe. Amworo Odira aliwaeleza kuwa mafunzo
waliyoyapata ni sawa na kupanda mbegu ambayo baadaye huzaa matunda, hivyo ni
matumaini yake na ya Mahakama kwa ujumla kuwa wataenda kuwatumikia Watanzania
kwa ubora ili kukithi matarajio yanayokusudiwa.
Naye Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Missenyi, Mhe. Yohana Myombo, akizungumza kwa
niaba ya washiriki wenzake ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa fursa hiyo ya
mafunzo waliyopata. Amewaomba washiriki wenzake kuitumia elimu waliyoipata
katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika kipindi hicho cha siku tano, watumishi hao walipitishwa
kwenye mada mbalimbali, ikiwemo Maadili na Kanuni za Maadili katika Mahakama;
Huduma kwa Mteja; Wajibu na Majukumu ya Mahakama za Wilaya; Utamaduni wa
Mahakama; Utii na Uvumilivu katika Mahala pa Kazi; Mabadiliko maeneo ya Kazi na
Uboreshaji wa Huduma za Mahakama.
Mada
zingine ni Matumizi ya Vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano; Utunzaji
wa siri; Uelewa wa Mpango Mkakati wa Mahakama; Upatikanaji wa Haki na Uaminifu
kwa Umma; Usimamizi Bora wa Mfumo wa Uendeshaji na Usajili wa Mashauri na Namna
ya kukabiliana na msongo wa mawazo na hasira.
Mada hizo
ziliwasilishwa na wawezeshaji wabobezi katika maeneo hayo, akiwemo Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Mkurugenzi wa Usimamizi wa
Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha, Mkurugenzi wa
Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula, Mkurugenzi
Msaidizi Bajeti na Mipango katika Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji, Bi.
Gladys Qambaita na Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi cha Mahakama ya Tanzania,
Mhandisi Yohana Mashausi.
Mahakama ya
Tanzania imeandaa mafunzo ya huduma kwa wateja ya siku 20 kwa watumishi
watakaohudumu katika Mahakama mpya za Wilaya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa
Benki ya Dunia na kuzinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022.
Mafunzo hayo
ambayo yatatolewa kwenye vituo vya Morogoro, Kigoma, Bukoba na Musoma yanalenga
kuwaandaa na kuwapatia ujuzi watumishi hao ili watoe huduma bora kwa wananchi
zinazoendana na uzuri wa majengo. Tayari mafunzo hayo yameshatolewa kwenye
Vituo vya Morogoro, Kigoma na Bukoba. Kituo kitakachofuata ni Musoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni