Ijumaa, 16 Desemba 2022

ZINGATIENI UTOAJI TAARIFA SAHIHI ZA KIMAHAKAMA UNAOZINGATIA WELEDI; PROF.OLE GABRIEL

Na Mary Gwera, Mahakama

Mahakama ya Tanzania leo tarehe 16 Desemba, 2022 imekutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari mbalimbali hapa nchini huku Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa rai kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kwa ujumla kuzingatia utoaji habari sahihi unaozingatia vyanzo muhimu vya habari husika ili taarifa sahihi za Mhimili huo ziwafikie vyema wananchi.  

Akizungumza na Wahariri hao kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke-Dar es Salaam, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, mara nyingi kumekuwa na upotoshaji wa taarifa za Mahakama hali inayosababisha sintofahamu au kuwa na mtazamo hasi wa umma dhidi ya Mhimili huo.

“Tuwe na utamaduni wa kusoma na kufuatilia mageuzi yanayofanyika ndani ya Mahakama ili kuhakikisha kuna ‘story balancing’ ya taarifa tunazotoa kwa umma, bora uchelewe ila utoe taarifa sahihi,” amesema Mtendaji Mkuu.

Ameongeza pia, ni muhimu kuwa na mahusiano mazuri baina ya Mahakama na Vyombo vya Habari ili kuweza kuwafikishia wananchi taarifa muhimu za kimaboresho na vilevile amewataka wananchi kuipa ushirikiano Mahakama hususani katika kipindi hiki ambapo huduma mbalimbali zimeboresha zinaendelea kuboreshwa.

“Ni muhimu wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha haki inatendekea kwa wakati, kwa mfano suala la ushahidi ni jukumu pia la mtu ambaye anaitafuta haki yake kwa sababu yeye ndiye anayejua kwamba uhalisia na tuhuma husika hivyo I muhimu kutoa ushahidi ili haki iweze kutendeka,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Aidha, Mtendaji huyo alipata pia fursa wa kuwasilisha Mada ya Mabadiliko ndani ya Mahakama baada ya uhuru hadi sasa’ ambapo amegusia kuhusu historia ya Mahakama pamoja na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama ikiwemo miundombinu ya majengo, matumizi ya TEHAMA, mwenendo wa kiutumishi, Uongozi na rasilimali watu na kadhalika.

Majengo ya Mahakama katika kipindi cha nyuma yalikuwa duni na sasa yameboreshwa, hii inatokana na kuongezeka kwa idadi ya Mahakama katika ngazi zote; idadi ya Mahakama Kuu kuna vituo 19, divisheni nne (4) za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi 30, Mahakama za Wilaya 135 na Mahakama za Mwanzo 960, kuanzishwa kwa dhana ya mfumo Jumuishi wa Utoaji Haki (IJC) katika jengo moja katika Mikoa mitano (5) na vilevile ujenzi wa jengo la makao makuu ya Mahakama ya Tanzania ambalo ni la sita kwa ukubwa duniani,” ameeleza Prof. Ole Gabriel.

Katika wasilisho lake, amebainisha kuwa, Mahakama imepiga hatua katika matumizi ya TEHAMA ambapo kwa sasa mchakato ipo mbioni kupata mfumo wa tafsiri ya Kiswahili na Lugha zingine (hata za asili) kupitia akili bandia (Artificial Intelligence).

 Akizungumza na niaba ya Wahariri hao, naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kufungua milango na kuweza kukutana nao kwani wameweza kufahamu mambo mengi yanayohusu Mahakama ambayo hawakuyajua awali.

“Tunaishukuru Mahakama kwa kutupa nafasi hii ya kukutana maana si mara nyingi Mahakama inakutana na Vyombo vya Habari, la pili tuwapongeze katika mageuzi tuliyoyashuhudia ya kimiundombinu na kimifumo. Vilevile ni ombi langu kwa baadhi ya mashauri muweze kuyaendesha moja moja ‘live’ ili wananchi washuhudie kama ilivyo kwa wenzetu Kenya,” amesema Bw. Balile.

Mada nyingine zilizotolewa katika Mkutano huo ni pamoja na ‘Uendeshaji wa mashauri katika Mahakama ya Tanzania’ iliyowasilishwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda na mada ya Maboresho ya Mahakama ya Tanzania ambayo imewasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.

Katika wasilisho lake, naye, Mhe. Kainda amesisitiza kuhusu matumizi ya TEHAMA kwakuwa yanasaidia katika kuharakisha usikilizaji wa mashauri Mahakamani.

“Sasa hivi Mahakama inauwezo wa kusikiliza mashauri yaliyofunguliwa katika kipindi husika kwa asilimia mia moja. Kutokana na mafanikio hayo Mahakama imeamua kujenga mfumo mpya “Case Management System” ambao hautaruhusu kabisa matumizi ya karatasi,” amesema Mhe. Kainda.

Akiwasilisha Mada ya Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, kwa upande wake, Mhe. Dkt. Rumisha amesema kuwa jamii inatakiwa kubadili mtazamo hasi kwa Mahakama kwa kuwa imejiboresha katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi, hivyo waone kama ni eneo la kukimbilia.

“Kuna uboreshaji wa huduma mbalimbali za Mahakama umefanyika na tunaendelea zote zinalenga kutoa haki bora kwa mwananchi, mfano katika uboreshaji wa huduma hizo mojawapo tumefanikiwa kupunguza idadi ya hatua/vituo vya ufunguaji mashauri kutoka hatua 38 mwaka 2015 hadi hatua 21 kwa mwaka 2021,” amesisitiza Mhe. Dkt. Rumisha.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na takribani Wahariri 25 pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Mahakama kimelenga kuendeleza ushirikiano baina ya Mahakama na Vyombo vya Habari.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.  Aliyeketi kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda na kulia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile. Leo tarehe 16 Desemba, 2022 Mahakama ya Tanzania imefanya mkutano na Wahariri hao kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Temeke-Dar es Salaam.
Meza mkuu ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika mkutano kati ya Mahakama na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa akiwasilisha mada kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini katika mkutano uliofanyika leo tarehe 16 Desemba, 2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyeketi katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Sehemu ya Wakurugenzi na Maafisa wengine wa Mahakama walioshiriki katika Mkutano kati ya Mahakama na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda akiwasilisha mada katika mkutano kati ya Mahakama na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akiwasilisha mada kwenye kikao cha Wahariri na Mahakama kilichofanyika leo tarehe 16 Desemba, 2022 kwenye ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke-Dar es Salaam.



Picha mbalimbali za Wahariri walioshiriki kwenye Mkutano huo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa.







 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni