Na Innocent Kansha, Mahakama
Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank
Mahimbali amewataka watumishi wa Mahakama kutambua dhamana waliyonayo kwa wananchi na Mahakama itawasaidia kuepuka utendaji kazi wa mazoea, na
usio zingatia maadili ya utumishi ikiwemo kutojihusisha na vitendo vya rushwa
na utumiaji wa lugha chafu zisizofaa kwa wateja ambazo zitaifanya Mahakama
kutoaminika na jamii.
Akifunga mafunzo ya watumishi 30 yaliyofanyika kwa muda wa siku tano
katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma kwa Mahakama za
Wilaya za Busega, Itilima, Butiama na Rorya katika hafla ya hiyo, Jaji
Mahimbali alisema, majengo hayo ya kisasa yapo kwa sababu moja kubwa ya kumrahisishia
mwananchi kupata huduma bora zinazozingati maadili na weledi ili mwanachi
azipate kwa ufasaha na kwa wakati.
“Ninawaasa nyote kwa pamoja mkatoe huduma ya haki bila ubaguzi wowote na
kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Mnapaswa kujitafakari katika suala zima la
kutoa huduma bora zinazomlenga mwananchi kwa uadilifu, weledi na uchapakazi ili
haki ionekane ikitendeka kwa vitendo na kuakisi maana halisi ya umuhimu wa
majengo mapya ili kuthibitisha ubora kwa wateja tunaowahudumia”, alisisitiza
Jaji Mahimbali.
Jaji Mahimbali alisema, ni jukumu la kila mtumishi kuifanya Mahakama
kuwa kimbilio la wananchi hasa wanyonge ambao wamekuwa wakipokonywa haki zao na
kuwataka kuwa sehemu muhimu ambayo itachuku sura mpya katika utoaji wa haki na
usawa, huduma bora zinazozingatia kumlenga kila mwananchi.
Mafunzo yakawe nyezo muhimu na yatafsiriwe kwa
vitendo na yawaongoze kutoa huduma bora zinazomlenga mteja. Kipaumbele cha
Mahakama ni kuhakikisha huduma bora zinamfikia mteja ili kujenga imani ya
Mahakama kwa wananchi na kuwafanya wananchi kuwa karibu zaidi na chombo chao.
Mahakama imejiimarisha na kujipambanua kwa huduma
bora ili kurejesha imani kwa wananchi ambayo kwa miaka mingi ilisuasua na
wananchi kukata tamaa kutokana na mwenendo wa huduma zake. Kwa sasa umma umerejesha
imani kubwa na kutambua haki inapatikana Mahakamani, alisema Kaimu Jaji huyo.
“Tuendelee kuijenga taswira chanya ya Mahakama
badala ya kuibomoa ili asije kutokea mtumishi wa kuisaliti huko mbeleni kwa
kufanya vitendo vya kuwakatisha tamaa wananchi. Vitendo hivyo vinaweza kuwa ni
huduma duni, upokeaji wa rushwa na ukosefu wa maadili mbele ya jamii
inayotuamini, wateja wanatambua sasa huduma zipo karibu kwa nia ya kuwapunguzia
gharama, usumbufu na kuwaokolea muda wa kujikita na shughuli za uzalishaji mali
na kukuza uchumi”, alieleza Jaji Mahaimbali.
Aidha, watumishi hao wametakiwa kumtanguliza Mungu katika majukumu yao huku
wakijua watatoa hesabu kutokana na kazi wanayoifanya duniani, hivyo wanatakiwa
kuendelea kuwatumikia wananchi na kukumbuka daima kuwa hakuna mwenye uwezo wa
kujificha mbele za haki kwa kila jambo watakalo litenda.
“Kwa dhamira hii Mahakama inatutaka kubadili fikra
na mtizamo wetu ili kuondokana na kutoa huduma kwa mazoea na badala yake
kupitia mafunzo haya kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anadhamiria kuunga
mkono juhudi za kutoa huduma bora bora zinazoendana na ubora wa wa miundo mbinu
ya majengo katika mazingira tunayofanyia kazi zetu”, aliongeza Jaji Mahimbali.
Kwa upande wake Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Mhe.
Judith Semkiwa kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo alisema, mafunzo hayo
yatachochea utendaji kazi kwa kila mtumishi pia kukabiliana na changamoto
zinazojitokeza, kuchapa kazi kwa weledi, uaminifu na ubunifu ili wateja waweze
kupata huduma zilizobora kwa kufuata msingi na taratibu.
Alisema kufanyika kwa mafunzo hayo kutakuwa ni chachu ya kuboresha
huduma zinazotolewa na mahakama pamoja na wadau ili kuleta maana halisi ya
uanzishwaji wa Mahakama mpya.
Naye, Afisa utumishi mwandamizi Bw. Jumanne Muna kwa niaba ya Mkurugenzi
Msaidizi wa Kitengo cha Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania Bi. Patricia Ngungulu alisema, mafunzo
hayo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi wa kada tofauti tofauti ili waweze
kukabiliana na changamoto za majukumu yao ya kila siku. Ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha watumishi wanafuata kanuni, maadili na kuondoa utamaduni wa
mazoea katika kuwahudumia wananchi kwa kuwakumbusha kuzingatia wajibu na miiko ya
kazi zao, ikiwemo kutunza siri za ofisi na kujenga mahusiano mema baina
miongoni mwa watumishi.
“Tusiishie kuwa wahudhuriaji wa mafunzo na wasikilizaji, tuweke yote
tuliyojifunza katika utendaji ili kuweza kuzifanya Mahakama zetu kuwa
sehemu pekee itakayo toa suluhisho la matatizo ya wateja”, alisema Afisa
utumishi huyo.
Naye, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Bw. Paulo Uromi, alisema
mafunzo hayo yana umuhimu kwao kwani yatawasaidia kutoa huduma nzuri na
kupunguza malalamiko yasoyo na tija kwa kutumia njia ya mtandao katika mfumo wa
kielektoniki.
Pia alisema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi zao kwa kufuata
maadili na kumtanguliza Mungu katika kufanya kazi zao ilikuondoa malalamiko ya
hapa na pale kwa wateja wao.
"Awali wateja walikua wakicheleweshewa huduma kutokana na ukosefu
wa vitendea kazi, huku kesi nyingi zikichukua muda mrefu hadi kupelekea miezi
kadhaa zikiwa Mahakamani, lakini sasa huduma zinatolewa muda huo huo na
kusomewa hukumu zao hii ni kutokana na kuwepo kwa vitendea kazi vya kutosha
katika Mahakama zetu za kisasa" alisema Uromi.
Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Mahimbali akitoa hotuba ya kufunga mafunzo mbele ya washiriki (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo hayo, kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda Maalumu ya Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta na kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Komba
Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Mahimbali akitoa nasaa wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni