Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro imempatia tuzo
maalumu aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama
ya Wilaya Morogoro, Mhe. Maua Hassani Hamduni baada ya kumaliza muda wake wa
kazi/kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa hafla ya kumuaga
Hakimu huyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul
Ngwembe alisema kuwa Hakimu huyo amekuwa ni mfano wa kuigwa kutokana na
kujituma kwa kazi nyakati zote na kuwa, atakumbukwa kwa utendaji kazi wake.
“Ni vyema watumishi wa Kanda hii, kuiga mfano wa Mhe.
Maua, basi ni wakati sasa watumishi wa Mahakama wajifunze kwake ili kuziba
pengo lake katika Mahakama yetu,” alisema Mhe. Ngwembe.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo ya utumishi
bora, Mhe. Maua alitoa shukurani zake za dhati kwa uongozi wa Mahakama Tanzania
na Kanda ya Morogoro kwa kuuthamini mchango wake katika Mahakama na kuomba
ushirikiano waliouonesha kwake udumu.
Mhe. Maua aliongeza kuwa bila kupewa ushirikiano toka
kwa viongozi na watumishi wa kada zote asingeweza kufanya kazi kwa ubora.
Mhe. Maua aliajiriwa tarehe 10 Desemba, 1979 kama
Karani katika Mahakama ya Wilaya Nzega, nafasi ambayo aliitumikia mpaka mwaka
1989 ambapo alipandishwa cheo kuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ulemo hii ikiwa
ni baada ya kujiendeleza na kupata cheti cha sheria katika chuo Kikuu cha
Mzumbe.
Mwaka 1995, Mhe. Maua alihitimu ngazi ya Stashahada ya
Sheria na kupandishwa cheo kuwa Hakimu wa Wilaya katika Kituo cha kazi Morogoro
mpaka mwaka 2008 alipopandishwa cheo kuwa Hakimu Mkazi daraja la II na mwaka
huo huo alijiendeleza katika Shule ya Sheria kwa Vitendo (LST).
Aidha, mnamo mwaka 2015 Mhe. Maua aliteuliwa kuwa
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama na kuhamishiwa Wilaya ya Mufindi Mkoani
Iringa. Mwaka 2020 alihamishiwa Mahakama ya Wilaya Morogoro akiwa kama Hakimu Mkazi
Mfawidhi na mwaka 2022 alipandishwa cheo kuwa Hakimu Mkazi Mkuu nafasi ambayo
amedumu nayo mpaka alipostaafu.
Kadhaika, katika hafla hiyo, Mahakama Kanda ya Morogoro
ilimpokea Naibu Msajili mpya wa Kanda hiyo aliyehamishiwa hapo kutoka Mahakama
Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Augustina Mmbando ambaye aliwataka Watumishi na Wadau
wa Mahakama katika Kanda hiyo kutoa ushirikiano wakati wa kazi ili kuujenga vyema
Mhimili wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni