Na Mwandishi wetu, Musoma.
Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma Mhe. Frank Mahimbali amewaasa watumishi wa Mahakama nchini kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kutimiza wajibu wao, hali ambayo itawasaidia kufanya kazi zao kwa weledi na maadili ili kufikia malengo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama nchini.
Akifungua mafunzo ya huduma kwa wateja kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya za Butiama na Rorya mkoani Mara pamoja na Mahakama za Wilaya Mkoa wa Simiyu za Busega na Itilima leo Jumatatu, Desemba 19, 2022, Jaji Mahimbali amesema kuwa kujituma pamoja na kufanya kazi kwa bidii pia kutasaidia katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi hao na hatimaye kufikia malengo ya mahakama nchini ya kutoa huduma bora kwa wananchi wote.
"Kama mtakumbuka Mahakama zenu ni miongoni mwa mahakama 18 zilizozinduliwa hivi karibuni na kutakuwa hakuna maana kabisa baada ya serikali kutumia fedha nyingi kujenga majengo mazuri na ya kisasa halafu huduma isiwe ya kuridhisha, hebu tuifanye Mahakama kuwa sehemu rafiki kwa wananchi wote " amesema
Ameongeza kuwa itakuwa ni ajabu pale ambapo
mwananchi atapata changamoto ya huduma mbovu ikiwepo kauli mbaya kutoka kwa
watumishi wa mahakma baada ya serikali kufanya uwekezaji huo kwa kujenga
majengo bora na ya kisasa ambapo kuwataka watumishi hao kubadili fikra
iliyojengeka kwa baadhi ya wananchi ya kwamba mahakama ni sehemu ya kufunga
watu badala yake mahakama ziwe sehemu ya kupata huduma ikiwemo ufafanuzi wa
kisheria.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt amesema, kuwa watumishi wa Mahakama
wanatakiwa kutambua kuwa Mahakama ndicho chombo pekee kilichopewa jukumu la
kitoa haki hivyo utendaji kazi wenye kzuingatia maadili na weledi utawezesha mahakama
kufikia malengo hayo.
"Tuna jukumu la kutoa haki kwa wananchi wote
hivyo huduma bora ni muhimu kwa ustawi wa wananchi na nchi yetu kwa ujumla"amesema
Awali Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo kutoka Mahakama ya Tanzania, Patricia Ngungulu alisema kuwa watumishi 140 wa Mahakama za wilaya 18 wamepata mafunzo hayo ya huduma bora kwa wateja, mafunzo yaliyofanyika kwa awamu nne.
Amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa maboresho ya huduma za mahakama huku akiwataka watumishi hao kutimiza wajibu wao licha ya kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa watumishi.
"Tunajua kuna upungufu wa watumishi lakini hiki kisiwe kigezo cha kushindwa kutimiza wajibu wetu, tufanye kazi kwa kujituma, weledi na kujitoa ikiwa ni pamoja na uchache wetu Ili kufikia malengo haya ya kuboresha huduma za mahakama nchini" amesema.
Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya huduma kwa wateja kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya ya Butiama na Rorya mkoani Mara pamoja na Mahakama za Wilaya Mkoa wa Simiyu za Busega na Itilima
Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Mafunzo kutoka Mahakama ya Tanzania, Patricia Ngungulu akitolea ufafanuzi mambo muhimu katika mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakiendelea kupata mada kutoka kwa Wakufunzi wa mafunzo hayo.
Picha na Mwandishi wetu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni