Na Innocent Kansha, Mahakama
Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewataka watumishi wa Mahakama
kuzingatia tunu za Mahakama ili kujenga utamaduni mzuri wa kuwahudumia wananchi
wakati wote bila kujali hali zao, itikadi wala jinsia.
Akitoa mada ya utamaduni na
maadili ya kimahakama kwa watumishi wa Mahakama za Wilaya za Rorya, Butiama,
Itilima na Busenga, Mhe. Chuma alisema kwa kuzingatia tunu hizo kunajenga
utamaduni wa kufanya kazi kwa kuzingatia miiko na kujenga misingi imara ya
mahusiano kazini.
Kwa upande mwingine Msajili
Mkuu alisema, ukizungumzia utamaduni na maadili ya kimahakama ni mambo
yasiyoweza kutenganishwa ikiwa msingi wake mkuu ni uzalendo, uwajibikaji, uadilifu,
uwazi, heshima, utu na ubora wa maamuzi kwa kutenda haki thamani yake ni
utumishi wa umma uliotukuka.
Kufikiwa kwa azma
hiyo kutahitaji mabadiliko ya kifikra, maadili, malengo ya kazi na uwajibikaji
miongoni mwa watumishi wa Mahakama. Ni matumaini ya Mahakama kwamba watumishi
wote wa Mahakama na wadau watashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa tunu na
hatimaye kufikia malengo ya Taasisi iliyojiwekea.
“Uboreshaji wa huduma za
Mahakama unaomlenga mwananchi umechangia mabadiliko ya utamaduni chanya wa
utendaji wa kazi za kila siku kwa kuzingatia vigezo vya upimaji wa kazi na
matokeo halisi kwa kila mtumishi”, alisema Msajili Mkuu
Mahakama ya Tanzania
inaendelea kuboresha huduma zake za utoaji haki kwa wote na kwa wakati. Lengo
kuu la Mahakama kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ya 2020/2021 kuelekea
2024/2025 ni kuhakikisha kuwa azma ya utoaji huduma inayomlenga mwananchi
inafanikiwa.
Aliongeza kuwa, watumishi
wanapaswa kufanya kazi kama timu na bahati njema nyie ni watumishi mlioaminiwa
kuanzisha huduma za Mahakama hizo mpya. Zingatieni maelekezo ya viongozi na
kuheshimu wateja mnaowahudumia bila wao Mahakama haiwezi itwa Mahakama.
“Teknolojia imechangia
kwa kiasi kikubwa kuboresha utamaduni wa utendaji wa watumishi mahali popote
alipo mtumishi ataonekana na kupimwa utendaji kazi wake bila kujali umbali wa
eneo alilopo kijiografia” aliongeza Mhe. Chuma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni