Na Catherine Francis-Mahakama Kuu, Songea
Katika
kuendelea kuadhimisha Wiki ya Sheria nchini watumishi na wadau wa Mahakama
Kanda ya Songea wamefika katika Chuo cha Ualimu Matogoro kutoa elimu kuhusu utatuzi
wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea, Mhe. Michael Manjale aliwaambia wanafunzi
katika Chuo hicho kuwa kauli mbiu ya mwaka 2023 imejikita katika kutatua
migogoro kwa njia ya usuluhishi, hivyo kama walimu watarajiwa hawana budi
kujifunza namna bora ya kutatua migogoro nje ya Mahakama.
Alisisitiza
kuwa walimu ni kundi muhimu kwakuwa wao ndiyo walezi wakubwa wa jamii nzima, hivyo
hawana budi kutumia busara na hekima katika kushughulikia na kutatua matatizo
ya wanafunzi wao ili kuweza kujenga kizazi kilicho bora.
Mhe.
Manjale aliendelea kusema kuwa wanafunzi wamekuwa na migogoro mingi baina ya
wao kwa wao au wao na walimu wao, hivyo wakiwa shuleni walimu ndiyo wasuluhishi
wa matatizo. Aidha, alitumia nafasi hiyo kufundisha sheria ya mtoto pamoja na
wajibu wao kama wazazi nini wanatakiwa kufanya.
Naye
Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mashtaka Ruvuma, Mhe. Hebel Kihaka alisema wapo tayari kuwashauri
wateja wao juu ya umuhimu wa usuluhishi kwa yale makosa ya jinai ambayo yanaweza
kumalizika kwa njia hiyo kulingana na mwongozo wa kisheria wa uendeshaji wa
makosa ya jinai.
Kwa
upande wake, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Songea Mjini, Mhe. Diana Manase
alifafanua maana ya Wiki ya Sheria na kwanini Mahakama inaadhimisha Wiki hiyo ya
utoaji elimu ya sheria kila mwaka nchini.
Katika maelezo yake, Mhe. Manase alisema maadhimisho hayo yapo mahususi kwa ajili ya kutoa elimu na msaada wa kisheria bure na wananchi hupata nafasi ya kujifunza majukumu na utendaji kazi wa kila ofisi.
Wakati wa zoezi hilo la utoaji elimu, Walimu na Wanafunzi walipata nafasi ya kuuliza maswali kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo utaratibu wa kufungua na kusikilza mashauri kwa njia ya kielektroniki, jinsi ya kufungua mashauri yanayohusu matunzo ya mtoto pamoja na utaratibu uliopo kwenye ofisi ya Wakili Serikali kuwatetea wananchi ambao hawana uwezo wa kujigharamia.
Watumishi na Wadau wa Mahakama waliotoa elimu katika Chuo cha Ualimu Matogoro wakiwa katika picha ya pamoja.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni