Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Wakati maadhimisho ya Wiki
ya Sheria yakielekea ukingoni, Timu ya utoaji elimu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kibaha imeshauri mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Bonde la Mto Ruvu utatuliwe
kwa njia ya suluhishi.
Mgogoro huo umebainishwa
baada ya Timu hiyo kufika katika Kijiji cha Ruvu Stesheni kwa lengo la kutoa elimu
na msaada wa kisheria kwenye maeneo mbalimbali.
Akizungumza kwenye mkutano
huo, Hakimu Mkazi kutoka Mahakama ya Mwanzo Magindu, Mhe. Jafari Msisi, ambaye
ni miongoni mwa Timu hiyo, alisisitiza kuwa migogoro kama hiyo ya wakulima na
wafugaji ni bora ikatatuliwa kwa njia ya usuluhishi badala ya kupelekwa mahakamani.
“Ikifanyika vinginevyo Mahakama
itatoa uamuzi na kumpa mmoja ushindi na mwingine akikosa inaweza kukaribisha uhasama
na pengine wadaawa kuzidi kutokuelewana,” alionya.
Awali, Mwenyekiti wa
Kijiji hicho aliyejitabulisha kwa jina moja la Abas aliieleza Timu hiyo kuwa mgogoro
huo ni wa muda mrefu na uamuzi ulishatolewa lakini wafugaji wamekuwa hawako
tayari kuutekeleza.
Mwenyekiti huyo alibainisha
kuwa kuna tamko lilitoka serikalini kuwataka wafugaji wote wahame katika Bonde
la Mto Ruvu, lakini mpaka sasa wapo na wanaingiza mifungo yao mashambani.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
huyo, kutokana na sitofahaiu hiyo wakulima aliamua kufanya maridhiano kwa
kuunda kamati maalumu kushughulikia mgogoro huo lakini wafugaji bado hawako
tayari, suala linaloleta ugumu na uadui.
Katika hatua nyingine, Mahakama
ya Wilaya Mkuranga imetembelea maeneo mbalimbali wilayani humo na kutoa elimu za
kisheria katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.
Hayo yamedhihirika katika
Shule ya Sekondari Mwinyi iliyoko katika Wilaya Mkuranga ambapo jopo la watoa
elimu likiongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Mhe.
Herieth Mwailolo lilitembelea shule hiyo.
Akizungumza katika eneo hilo,
Mhe. Mwailolo amesema Mahakama hiyo imedhamiria kufika maeneo muhimu yenye uhitaji
wa elimu ya kisheria, ikiwemo mashuleni na stendi za mabasi, ambayo yanahitaji
kupewa kipaumbele.
Amesema katika shule
hiyo, wanafunzi wa kike wamekuwa na shauku ya kujua sheria za mirathi na kama
sheria inamruhusu mtoto wa kike kurithi mali.
Naye Mwakilishi wa Taasisi
ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Bi. Euphrazia Kakiko, amesema rushwa
ya ngono huchangia kudidimiza uchumi wa taifa na kusababisha wanafunzi
kutofanya vizuri kwa kutarajia kufaulu kwa kutoa rushwa, hivyo hupelekea kupata
viongozi wabovu baadaye.
Akawataka wanafunzi hao
kusoma kwa bidii na kupinga vikali vitendo vya rushwa na pale wanapoona kuna
viashiria wasisite kutoa taarifa kwenye mamlaka husika ili kukomesha vitendo
hivyo.
Utoaji wa elimu ukiendelea maeneo ya stendi ya Mkuranga.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni