Na Ibrahim Mgallah, Mahakama Kuu Mbeya
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Mbeya, kwa kushirikiana na wadau wake inaendelea na zoezi la utoaji
elimu ya sheria katika maeneo mbalimbali ya jijini hapa ikiwa sehemu ya
maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Zoezi hilo lilianza
tarehe 22 Januari 2023. Utoaji elimu
umejikita kwenye kauli mbiu ya mwaka 2023 inayosema, “Umuhimu wa utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: Wajibu wa
Mahakama na wadau.”
Elimu ya sheria
imeendelea kutolewa katika kituo cha mabasi Kabwe na katika mashule, ikiwemo Shule
za Sekondari Ivumwe, Ikuti, Tulia Ackson na Itende. Vilevile elimu ya sheria
imetolewa kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na kupitia vituo
vya Redio Baraka fm na Rock fm.
Akitoa elimu ya sheria
katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Mbeya, Mhe, Dkt Lilian Mongella ameishauri jamii kutumia njia ya
usuluhishi katika kutatua migogoro yao mbalimbali ili kuokoa muda na gharama.
“Tunawahamasisha zaidi
wadaawa wanaotafuta kutatatua migogoro yao wakimbilie kwanza kwenye
kuisululisha ili kuokoa muda na gharama, jambo litakalopelekea kuokoa uchumi
wao,’’ alisema Jaji Mongella.
Watu wote waliofikiwa na
elimu ya sheria wameipongeza Mahakama kwa mpango huo kwani utasaidia jamii kuwa
na amani, umoja na mshikamano. Zoezi la
utoaji elimu linaendelea hadi ifikapo tarehe 29 Januari, 2023.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni