Na Tiganya Vincent-Mahakama -Dodoma
Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wananchi kutumia njia mbadala katika
utatuzi wa migogoro ili kuwawezesha kuwa na muda mwingi katika utekelezaji wa
shughuli za kujiingizia kipato.
Ametoa kauli hiyo jana tarehe
27 Januari 2023 mjini hapa wakati wa ziara yake ya kutembelea maonesho ya Wiki
ya Sheria yanayoendelea katika Viwanja vya Nyerere Square.
Mhe. Dkt. Ndumbaro
alisema kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema umuhimu wa utatuzi wa migogoro
kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu; wajibu wa Mahakama na
Wadau, Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuhakikisha kuwa inasisitiza
matumizi ya njia mbadala katika kumaliza migogoro kwenye jamii.
Alisema njia mbadala
zinaimarisha urafiki, mashauri humalizika haraka na kutumia gharama nafuu,
hivyo kuwezesha pande zote kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Dkt.Ndumbaro
aliongeza kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha inasajili wasuluhishi wa
migogoro kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili
kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi.
“Hii mtu akitaka kufanya
anaingia katika Tovuti ya Wizara na kujisajili na wakiridhika kama wana sifa
wanasajiliwa kama wasuluhushi na tunawatumia vyeti vyao kwa njia ya mtandao ili
waanze kuwahudumia Watanzania katika suala la usuluhishi,” alisema.
Katika hatua nyingine
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Ndumbaro amemhakikisha mwananchi aliyetaka
vyeti vya kuzaliwa kutoka Wakala wa usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA)
vitolewe karibu na maeneo wanayoishi ili kuwapunguzia mzigo wa nauli ya
kusafiri kutoka vijijini kutafuta huduma hiyo mijini.
Awali Leonard Motto
alisema kuwa amekuwa akitumia kiasi cha shilingi elfu 70 kwa safari na kuja na
kurudi kwake kwa ajili ya nauli kufuatilia cheti cha RITA Dodoma mjini na
anapofika wakati mwingine anaelezwa akifuate cheti ni baada ya siku saba, jambo
ambalo linamsababishia gharama.
Alisema ni vema RITA
wakaweka utaratibu ambao utakuwa rafiki na sio mzigo kwa mwananchi anapotaka cheti
cha kuzaliwa kutoka RITA ili akipate na
kurudi kwake kwa ajili ya kuendelea na majukumu merngine.
(Picha na Tiganya
Vincent)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni