Na Francisca Swai-Mahakama, Musoma
Wananchi wameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa Wiki ya Sheria kwa ajili ya utoaji elimu na
msaada wa kisheria bure na kwa urahisi.
Akitoa shukrani hizo, Mkazi
wa Musoma Mjini, Bi. Veronica John amesema kuwa elimu inatolewa kwa uhuru,
kwani watumishi pamoja na wadau wanakuwa na muda wa kutosha kusikiliza, kutoa
maelezo, ufafanuzi na ushauri wa masuala mbalimbali.
“Hali niliyokuta ni
tofauti kabisa na pale watumishi hawa wakiwa maofisini ambapo wanakuwa na
mizunguko na shughuli nyingi,” alisema baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika
Viwanja vya Mukendo ambayo yameandaliwa na Mahakama na wadau wake.
Naye Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara
kwenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mara, Bw. Francis Ngowi
amesema maonesho hayo kila mwaka yamekuwa na manufaa kwa kuwakutanisha wadau
mbalimbali pamoja, kufahamiana tofauti na kila mmoja akiwa ofisini kwake.
Amesema hatua hiyo inawawezesha
kuwahudumia wananchi kwa pamoja, hivyo mwananchi akitembelea maonesho hayo ya Wiki
ya Sheria anaweza kupata huduma nyingi kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake, Wakili
Christopher Waikama ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutembelea maonesho hayo
ili kupata ushauri wa masuala mbalimbali hasa namna ya kufanya usuluhishi ili
kupunguza migogoro mikubwa hasa iyohusiana na ardhi.
Amesema mwananchi
akitembelea maonesho hayo ataweza pia kujifunza vitu mbalimbali kutoka kwa
wadau wanaoshiriki kama vile Jeshi la Polisi, Mawakili wa Kujitegemea, Afya,
TAKUKURU, Msaada wa Kisheria, RITA, NIDA na wengine wengi.
Naye Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mhe. Bahati Bwire na Hakimu Mkazi, Mhe. Gibson
Ngojo, wanaoshiriki kutoa elimu katika Viwanja hivyo wamesema mwitikio wa
wananchi ni mkubwa na wengi wana matatizo ya ndoa, talaka, mirathi na ardhi.
Maonesho hayo ya Wiki ya
Sheria yanatolewa katika maeneo mbalimbali ikiwemo viwanja vya Mukendo Musoma
Mjini, taasisi za elimu katika shule za Msingi, Sekondari na Vyuo na stendi
mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mara.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja
na wadau kutoka banda la Chemba ya Wafanyabiashara TCCIA. Mwenye fulana ya rangi
ya bluu ni Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara Mara, Bw. Francis Ngowi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni