Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa ushauri kwa Jeshi la Magereza nchini
kuona namna bora ya kufuatilia nyenendo za wafungwa pindi wamalizapo muda wa
vifungo vyao kwa kushirikiana na Halmashauri kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii ili dhana ya
marekebisho ya tabia kwa wafungwa iweze kuonekana kwa vitendo.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari jana tarehe 26 Januari, 2023 jijini Dodoma mara baada ya
kukagua Mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria yanayofanyika
katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini humo, Mhe. Senyamule alisema kuwa,
asilimia kubwa ya wafungwa wanaomaliza vifungo vyao bado wanaendelea na tabia
zisizo na maadili ikiwemo kufanya uhalifu kama wizi na mengineyo.
“Nimepita katika
banda la Magereza nimeona wanafanya kazi nzuri sana, na hususani wajibu wa
marekebisho kwa wafunga, lakini naona mara nyingi baada ya wafungwa
kumaliza vifungo vyao hawafuatiliwi nyenendo na hatimaye wengine kuendelea kufanya uhalifu kama wizi na kadhalika, hivyo, ni muhimu Magereza kuangalia
namna bora ya kuendelea kufuatilia nyenendo za wafungwa hata baada ya kumaliza
vifungo vyao, ni muhimu Magereza kuangalia namna ya kushirikiana pamoja na
Halmashauri na hususani Maafisa Ustawi wa jamii kuangalia namna bora ya
kuwawezesha wananchi hao baada ya kumaliza vifungo ili waweze kuendelea na
maisha yao,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aliongeza kuwa, Mkoa
wake upo tayari kushirikiana na Magereza kwa kuwa mfano (sample area) ambayo
itakuwa eneo kwa ajili ya kuwasaidia wafungwa hao wanaomaliza vifungo hata kwa
kupewa mitaji na elimu zaidi kupitia Halmashauri na Maafisa Ustawi wa Jamii ili
kuendelea na maisha yao bila uhalifu kwa kuwa asilimia kubwa ya wafungwa
waliomaliza kutumikia vifungo vya huendelea na tabia za kihalifu.
Kwa upande
mwingine, Mhe. Senyamule ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi nzuri
inayoendelea kufanya ikiwa ni pamoja na uboreshaji pamoja na mabadiliko katika utoaji
wa huduma zake mbalimbali.
Kadhalika
amepongeza Mhimili huo kwa kuja na Kauli mbiu inayohusu masuala ya Usuluhishi
kwa kuwa njia hii inaleta mshikamano baina ya wananchi.
“Njia hii ya
utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi itaongeza utoaji haki kwa njia ya
mapatano na makubaliano na wananchi watapata muda wa kufanya shughuli nyingine
zitakazowaingizia kipato, hivyo wito wangu kwa wananchi watembelee maonesho
haya kupata elimu zaidi ya usuluhishi,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Miongoni mwa
Mabanda aliyotembelea Mhe. Senyamule ni pamoja na Mahakama Kuu ya
Tanzania-Kituo cha Usuluhishi, Jeshi ya Magereza, Jeshi la Polisi, Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ‘BRELA’, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF), Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) na mengine.
Maonesho haya ya
Wiki ya Sheria yanaendelea kufanyika nchi nzima hadi tarehe 29 Januari, 2023 na
kilele cha Siku ya Sheria nchini itakuwa tarehe 01 Februari, 2023 ambapo
itafanyika Kitaifa jijini humo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.
Kauli mbiu ya Wiki
na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni; Umuhimu
wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi
Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akiwa katika banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni