·
Wanafunzi
Elimu ya Msingi, Sekondari, Vyuo, wafungwa, Askari Polisi, Madaktari na Wauguzi
na wengine wanufaika na elimu hiyo.
Na
Stanslaus Makendi na Arapha Rusheke; Mahakama Kuu Dodoma
Mahakama Kuu
ya Tanzania Kanda ya Dodoma kwa kushirikiana na wadau wake wamewafikia wananchi
wapatao 2000 katika utoaji elimu ya sheria hususani juu ya umuhimu wa kutatua
migogoro kwa njia ya Usuluhishi na masuala mengine muhimu ya kisheria kwa
makundi mbalimbali ndani ya Jiji la Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa Maadhimisho
ya Wiki ya Sheria nchini kwa mwaka 2023.
Elimu hiyo imetolewa tarehe 27 Januari, mwaka huu katika Shule za Msingi Uhuru na Chang’ombe, Shule za Sekondari Msalato na Welaa, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini. Pia, elimu hiyo ilitolewa kwa Maaskari Polisi wa Kituo cha Polisi Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Gereza Kuu Isanga na Vituo vya Mabasi na masoko mbalimbali ndani ya Jiji la Dodoma.
Akitoa elimu ya umuhimu wa kutumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro wakati wa kutoa elimu kwa makundi hayo; Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mhe. Janeth Musaroche amewasisitiza wananchi na wakazi wa Mji wa Dodoma kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro baina yao kuliko kujichukulia sheria mkononi.
“Ninawahakikishia wananchi wenzangu kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi huokoa gharama za kesi na muda, pia hujenga na kuimarisha zaidi ushirikiano na mahusiano baina ya pande zilizokuwa na mgogoro pindi ridhaa ya suluhu inapopatikana kutoka kwa wahusika wa mgogoro huo,’’ alisema Musaroche.
Zoezi la utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii linakadiriwa kuwafikia watu wapatao 2000 katika kipindi cha wiki moja tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho hayo tarehe 22 Januari, 2023. Elimu hiyo imetolewa kupitia mikutano ya hadhara, mazungumzo ya ana kwa ana baina ya makundi pamoja na kutumia vyombo vya Habari ikiwemo Redio na Televisheni.
Wananchi na
makundi hayo muhimu ya jamii yaliyofikiwa na elimu hiyo wameisifu Mahakama ya
Tanzania kwa programu hiyo na kuomba iwe endelevu ili kuwaelimisha wananchi
masuala muhimu yanayohusu haki zao.
Sehemu ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) wakimsikiliza Mhe. Janeth Musaroche (aliyesimama) akitoa elimu ya sheria pindi alipotembelea Chuo hicho kwa ajili ya kutoa mafunzo ya masuala ya Usuluhishi na Sheria wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msalato iliyopo mkoani Dodoma wakisikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa na watoa elimu walioandaliwa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, 2023.
Sehemu ya Wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) wakimsikiliza Mhe. Janeth Musaroche (hayupo pichani) pindi alipotembelea Chuo hicho kwa ajili ya kutoa mafunzo ya masuala ya Usuluhishi na Sheria wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
Afisa wa Jeshi la Polisi akitoa elimu ya kujitambua na makuzi kwa wananfunzi wa Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo na ujasiri wa kutoa taarifa za matukio mbalimbali ya kikatili wanayokumbana nayo katika jamii.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Janeth Musaroche (wa pili kushoto) akiwa na watumishi na Wadau wa Mahakama wakati wa kutoa Elimu kwa Umma kwa njia ya Redio.
Askari wa Jeshi la Polisi akitoa elimu ya masuala ya Ulinzi Shirikishi na umuhimu wa kuzingatia sheria baina ya wananchi ili kupunguza matukio ya kiuhalifu na mauaji yanayotokana na sababu ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni