Na Faustine Kapama-Mahakama, Manyoni
Watumishi na wadau
mbalimbali wa Mahakama katika Wilaya ya Manyoni leo tarehe 29 Januari, 2023
wamehitimisha maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa kufanya matendo ya huruma katika
Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.
Katika kuonyesha upendo
na jinsi wanavyoijali jamii ya Watanzania, watumishi na wadau hao, wakiwemo Maafisa
Ustawi wa Jamii na Mawakili wa Kujitegemea wametoa msaada wa vitu mbalimbali
katika wodi ya wazazi katika hospitali hiyo.
“Sisi ni watumishi wa
Mahakama, tumeungana na wadau wetu kuja kuwaona na kuwapa zawadi kidogo,”
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Manyoni Mjini, Mhe. Masatu Magesa,
aliyeongoza msafara huo aliwaambia wazazi katika wodi hiyo.
Amesema kuwa kwa muda wa wiki nzima Mahakama ya Tanzania ilikuwa
inaadhimisha Wiki ya Sheria kwa kutoa msaada na elimu ya kisheria bure kwa
wananchi katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Manyoni.
“Tumeona tuje
tuwasalimie tunapohitimisha maadhimisho haya. Tumeandaa zawadi kidogo kwa ajili
yenu, tunaomba muipokee. Nyinyi ni watu muhimu sana kwetu, tunaowajibu wa
kuwatumikia. Bila nyinyi Mahakama haiwezi kuwepo,” alisema.
Kwa upande wake, Wakili
wa Kujitegemea, Msomi Keneth Nangawe, akizungumza baada ya kushiriki zoezi hilo alisema
kuwa wao kama wadau wa Mahakama wameungana pamoja kuwatembelea ndugu zao katika
hospitali hiyo.
“Hawa ni Watanzania
wenzetu, kuja kwetu hapa ni ishara kuwa tupo kwa ajili ya kuihudumia jamii,
hivyo tukaona siyo mbaya sisi kushiriki nao na kuwapa chochote ambacho
tumebarikiwa na Mungu ili kuonyesha kuwa sisi hatupo mbali nao, bali tupo
pamoja,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa
Ustawi wa Jamii katika Wilaya ya Manyoni, Bi. Ashura Jumbe, amesema kuwa jambo
walilofanya watumishi na wadau wa Mahakama kutoa kitu chochote katika hospitali
hiyo ni jambo kubwa na wameonyesha kwamba wao hawapo kwa ajili ya kuhukumu kesi
pekee, bali pia kuihudumia jamii.
“Jambo ambalo
wamelifanya kutoa zawadi kwenye wodi ya wazazi ni kubwa na linaleta faraja. Kama
tulivyoona, wazazi wamefurahia, mimi kitu kikubwa cha kusema ni asante, nasema
asanteni sana na tunashukuru kwa moyo ambao mmeuonyesha,” alisema.
Kwa muda wa wiki nzima
kuanzia tarehe 22 Januari, 2023, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki
ya Sheria katika maeneo mbalimbali nchini kwa watumishi na wadau wake kutoa msaada
na elimu ya kisheria bure kwa wananchi. Maadhimisho ya Siku ya Sheria yatafanyika
kitaifa jijini Dodoma tarehe 1 Februari, 2023 na mgeni rasmi atakuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni