Jumamosi, 28 Januari 2023

SHAMRASHAMRA ZATANDA WIKI YA SHERIA; MAHAKAMA ARUSHA YATIKISA JIJI KWA BONANZA MAALUM

·       Majaji wasisimua bonanza hilo kwa ushiriki wa michezo

·       ·       Arusha, Moshi, Manyara na Wadau washiriki pamoja

Na Angel Meela, Mahakama-Arusha

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha leo tarehe 28 Januari, 2023 imeratibu na kushiriki katika bonanza maalum la michezo lililohusisha Kanda tatu za Mahakama ikiwa ni Mahakama Kuu Kanda ya Arusha (waandaaji), Mahakama kuu Kanda ya Moshi na Mahakama kuu kanda ya Manyara ambapo Kanda hizo pamoja na wadau wote wa sheria wameshiriki ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria iliyoanza tarehe 22 Januari mwaka huu.

Mwandishi wetu kutoka Arusha, Bi. Angel Meela anaripoti kuwa Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, riadha, kukimbia kwa magunia, kukimbia kwa yai, kupokezana vijiti, mchezo wa kuzunguka viti pamoja na burudani zingine  lengo likiwa ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kama ilivyo kauli mbiu ya wiki ya sheria ya mwaka huu iliyoanza kuadhimishwa tarehe 22 Januari mwaka huu na inatarajiwa kukamilishwa tarehe 29 Januari mwaka huu.

Mwandishi wetu anaeleza kuwa, Bonanza hilo limefanyika katika Viwanja vya General Tyre-Njiro, huku akieleza kuwa kwa upande wa mpira wa miguu zilikuwepo timu nne nazo ni timu ya Mahakama Arusha, timu ya Mahakama Moshi, timu ya Mahakama Manyara na timu ya Polisi Arusha ambapo timu ya Mahakama Arusha iliibuka kidedea baada ya kuifunga goli 2-1 timu ya Polisi Arusha katika mechi ya fainali iliyochezwa jioni jijini Arusha.

Na kwa upande wa mpira wa pete timu ya Polisi Arusha iliwacharaza timu ya Mahakama Arusha goli 50-15, hata hivyo mwandishi wetu alipopata nafasi ya kuzungumza na moja ya mchezaji wa timu ya Mahakama na kuwauliza ni nini kimewasibu hadi kupata kichapo hicho licha ya mazoezi makali waliyokua wakifanya, walidai timu ya polisi ni timu kubwa inayocheza ligi daraja la kwanza na hivyo wapo daraja la juu.

Sambamba na michezo hiyo ya mpira wa miguu na mpira wa pete kulikua washindi wengine kama ifuatavyo, kuvuta kamba washindi kwa wanaume na wanawake ni Mahakama Arusha, mchezo wa kuzunguka viti mshindi ni Mhe. Jaji Gladys Barthy,  Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Manyara, mchezo wa kukimbia na yai mshindi ni Bw. Chacha Joseph kutoka Mahakama Kanda ya Moshi, riadha mita 100 washindi ni Bw. Anywelsie Joshua kutoka Jeshi la Polisi Arusha na Bi Nelly Kache kutoka Mahakama Arusha, mbio za vijiti mshindi ni timu Arusha na timu ya Polisi.

Kadhalika, mashindano ya kula mshindi ni Wakili wa Serikali kutoka Moshi Bw. Kassim Nassir na mashindano ya kuvuta kwamba Mahakama Arusha waliibuka kidedea kwa upande wa wasichana na wavulana. Washindi wote wamekabidhiwa makombe na medali na Majaji wafawidhi wa Mahakama za kanda zote tatu zilizoshiriki bonanza.

Akizungumza baada ya kutoa zawadi na medali kwa washindi katika Viwanja vya General tyre jijini Arusha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga ameishukuru Kamati ya maandalizi kwa kufanikisha Bonanza hilo na vilevile kuzishukuru Mahakama pamoja na wadau walioshiriki katika Bonanza hilo na kuongeza kuwa wasisite kuialika Mahakama Kanda ya Arusha wakiandaa bonanza au shughuli yeyote.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kushoto) akipokea medali kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Juliana Massabo, anayepiga makofi kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Simfukwe. Bonanza hilo limefayika leo tarehe 28 Januari, 2023 katika Viwanja vya Viwanja vya General Tyre-Njiro jijini Arusha.
Sehemu ya Majaji walioshiriki katika Bonanza (wenye fulana nyeupe)

Wachezaji kutoka Mahakama Kanda ya Arusha wakifurahia kombe la ushindi wa mpira wa miguu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Gladys Barthy akipokea medali ya ushindi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga (kushoto).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akimkabidhi kombe Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Yohane Masara baada ya Timu ya Mahakama Kanda ya Arusha kuibuka mshindi katika mchezo wa mpira wa miguu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganya akimpongeza kwa kumpatia medali Mtendaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Bw. Leonard Maufi kwa uratibu mzuri wa Kamati ya maandalizi ya Bonanza hilo.
Makombe na medali maalum zilizoandaliwa kwa ajili ya washindi wa michezo mbalimbali pamoja Kamati ya Maandalizi ya Bonanza hilo.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni