Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma ametoa rai kwa Wadau wa Mhimili huo na wananchi walioshiriki na kutembelea
maonesho ya Wiki ya Sheria kuwa chachu ya kuhamasisha usuluhishi dhidi ya
migogoro mbalimbali inayojitokeza katika jamii ili kulinda amani na kukuza uchumi.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama, Wadau na
Wananchi walioshiriki katika hafla ya kufunga Maonesho ya Wiki ya utoaji elimu
ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ leo tarehe 29 Januari, 2023, Mhe.
Chuma amesema kuwa, kwa kufanya hivyo watakuwa wanatekeleza kwa vitendo Kaulimbiu ya wiki ya sheria ya mwaka huu
isemayo; “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi katika Kukuza Uchumi
Endelevu: Wajibu wa
Mahakama na
Wadau.”
“Ni imani yangu kwamba kila Taasisi iliyoshiriki maonesho haya
imejipambanua ipasavyo kwenye kauli mbiu hii, kuelimisha wananchi na kuonesha
utayari wao wa kusaidia utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa
maslahi mapana ya kusaidia wananchi kukuza uchumi wao na wa nchi yetu kwa
ujumla,” amesema Mhe.
Chuma.
Mahakama
katika utaratibu wake wa kuelimisha umma itaendelea kuhimiza na kuuelimisha juu
ya faida za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. “Kimsingi, usuluhishi ni takwa la
kikatiba na ni kwa mujibu wa ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,”
amesisitiza Msajili Mkuu.
Mhe. Chuma ameainisha faida za usuluhishi ambazo ni pamoja na kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, kupunguza gharama na kujenga au
kulinda amani na kuongeza kuwa,
usuluhishi ni agizo la maandiko matakatifu huku akitoa mifano wa Waebrania 12:14
inaelekezwa kuwa tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, Mathayo 5:9 inaainisha kuwa heri wapatanishi;
maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Nayo,
Mathayo 5:25-26 inaelekeza kuwa njooni upatane na mshtaki wako wakati unaenda
naye kortini,
asije mshtaki wako akakukabidhi kwa hakimu, na mwamuzi kwa walinzi au kufungwa
gerezani.
Aidha; Msajili Mkuu ameonesha kuridhishwa na idadi ya
Taasisi/Wadau walioshiriki katika Maonesho hayo, ambayo idadi yao ni Taasisi 38
zilizoshiriki katika maonesho hayo
na kueleza kuwa mwitikio huo unatokana na mahusiano mazuri ya
Mahakama na wadau na utayari wa wadau kushirikiana na Mahakama kwa kutoa mchango
wao katika kuelimisha wananchi na kuboresha huduma za upatikanaji haki.
Aliongeza kuwa, anaamini kwamba,
ushirikiano huu utasaidia kuimarisha mahusiano na mazingira mazuri ya utoaji
haki na utoaji huduma kwa ujumla kwa wananchi wanaowahudumia. Vilevile amewaomba Wadau kutenga bajeti za kutosha kwa ajili
ya
kuweka mazingira wezeshi katika matumizi ya TEHAMA kwa lengo la kuendelea na
kasi ya karne ya 21.
Kadhalika, Mhe. Chuma amewashukuru Viongozi waliopata
nafasi ya kushiriki na kutembelea maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika kitaifa
jijini Dodoma, Viongozi hao ni pamoja na; Mhe. Dkt. Philip Isidor
Mpango, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Damasi Ndumbaro (Mbunge) Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Mhe. Salma Maghimbi, Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani,
Prof. Elisante ole Gabriel Mtendaji Mkuu wa Mahakama na wengine.
Mbali na Wadau, Msajili Mkuu amevishukuru pia Vyombo vya
Habari kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuuhabarisha umma katika kipindi chote cha maonesho na kuwaomba kuendelea kutoa
taarifa sahihi za Mhimili huo zinazozingatia usawa wa pande zote muhimu za
taarifa husika.
Wiki ya Sheria nchini ilizinduliwa rasmi tarehe 22
Januari, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Philip Mpango ambaye alizindua kwa ngazi ya kitaifa. Aidha, kilele cha Siku ya
Sheria nchini kwa mwaka huu itakuwa tarehe 01 Februari, 2023 ambapo kitaifa
itafanyikia katika Viwanja vya Chinangali mkoani Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa Wadau walioshiriki katika Maonesho hayo
ni pamoja na Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), Tume ya Haki za Binadamu, Tume ya Kurekebisha
Sheria, Tume ya Utumishi ya Mahakama, Taasisi ya Usuluhishi, Baraza la
Ushindani, Ofisi ya Mkemia Mkuu Wa Serikali, Mamlaka ya Kuthibiti Dawa za Kulevya, Kamisheni ya Usuluhishi na
Uamuzi, Kituo cha Haki za Binadamu, OSHA.
Wengine ni Taasisi ya Mafunzo ya
Sheria kwa Vitendo (LST),
RITA,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, NMB, TAKUKURU, Wakili Mkuu Wa Serikali,
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Chama Cha Majaji Wanawake (TAWJA),
Mahakama ya Afrika Mashariki, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chuo Cha uongozi wa Mahakama Lushoto,
Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi Nyumba Na Maendeleo ya Makazi, Jeshi la
Zimamoto, Jeshi La Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, BRELA na wengine.
Meza kuu wakiwafuatilia wanakwaya (hawapo katika picha) walipokuwa wakitoa burudani wakati wa tukio la kufunga Maonesho ya Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria. Katikati ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, wa pili kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria, Mhe. Sylivester Kainda, wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani (T) na Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki na Siku ya Sheria, Mhe. Charles Magesa na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni