Na Mary Gwera, Mahakama-Msemembo, Manyoni
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani leo tarehe 07 Januari, 2023 ameongoza maelfu ya watu kumzika
aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt.
John Utamwa aliyefariki dunia tarehe 02 Januari, mwaka huu.
Akizungumza na hadhara iliyokuwepo katika ibada ya
kumuaga marehemu Jaji Utamwa katika kijini cha Msemembo Wilaya ya Manyoni
mkoani Singida, Mhe. Siyani amesema kuwa, Mahakama imepoteza mtu makini ambaye
alikuwa na mchango mkubwa kwa Mhimili huo na Taifa kwa ujumla.
“Kwanza napenda kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa
na marafiki kwani tumepata pigo zito na tumempoteza Kiongozi, mwalimu na rafiki
wa wengi ambaye alikuwa akipenda ushirikiano na watu katika masuala mbalimbali,”
amesema Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi ameainisha kuwa, marehemu Jaji Utamwa
alikuwa na mchango mkubwa kwa Mahakama na jamii, huku akieleza kuwa marehemu
alipenda kufanya tafiti za masuala mbalimbali, alikuwa mwanahaki aliyependa
kusimamia haki za watu bila kuwa na chembe ya ubaguzi.
“Marehemu Jaji Utamwa alipenda sana elimu kujiendeleza,
licha ya kukaribia kustaafu mwaka jana alianza kusoma shahada nyingine, hili ni
funzo kwetu kuwa elimu haina umri, mara nyingi alinishauri mimi pia
nijiendeleze zaidi nami nilisikiliza ushauri wake na nimeanza shule na hivi
karibuni alinitumia boksi la vitabu ili kunisaidia katika masomo yangu,” ameeleza
Jaji Kiongozi.
Kiongozi huyo wa Mahakama Kuu ametoa ujumbe kwa Wana-Manyoni
kuwa marehemu alikuwa Mtetezi wao, kwakuwa alipenda ustawi wa Wilaya yake huku
akitoa mfano kuwa, marehemu Jaji Utamwa ndiye aliyejenga hoja zenye mashiko
zilizosababisha kujengwa kwa Mahakama mpya ya Wilaya ya Manyoni ambayo Mhe. Siyani
anabainisha kuwa marehemu Jaji Utamwa alitamani awepo wakati wa uzinduzi wa
jengo hilo la Mahakama. Ameongeza kwa kuwasihi wananchi wa Wilaya hiyo kuyaenzi
mazuri yote aliyokuwa nayo ikiwa ni pamoja na kutunza amani na haki
aliyoidumisha.
Kwa upande wa familia, Mhe. Siyani amewasihi kuwa na
moyo wa ushujaa huku akitoa neno la Faraja kwa familia hiyo kutoka Kumbukumbu
la Torati sura ya 31 mstari wa sita (6) lisemalo; ‘Iweni Hodari na moyo
wa ushujaa, msiogope wala msihofu kwa maana Bwana Mungu wako yeye ndie
anayekwenda pamoja nawe hatakupungukia wala kukuacha’.
Akiongoza misa ya mazishi ya Jaji Utamwa, Askofu wa
Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Bonde la Ufa (Lift Valley), Baba Askofu John
Lupaa ameainisha mambo manne ya kumkumbuka marehemu ambayo ni pamoja na kuwa na
heshima kwa watumishi wenzake wa umma ambapo aliamini kuwa kila mtu ana nafasi
muhimu nkatika kazi, mchapakazi ambapo alitekeleza wajibu wake kwa weledi na
uadilifu mkubwa, kuimarisha uhusiano kati ya Viongozi wa dini na Serikali na
jambo la nne marehemu alikuwa Mkristo halisi aliyeshiriki katika mambo
mbalimbali ya kikanisa.
Akisoma wasifu wa Marehemu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kwamba, marehemu alihudumu
katika vituo mbalimbali vya kazi huku akishika vyeo mbalimbali ikiwemo uhakimu,
usajili na kadhalika na hadi umauti unamfika alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Iringa.
Kadhalika, Prof. Ole Gabriel ametoa shukrani kwa ndugu,
jamaa marafiki, Madaktari, kanisa, watumishi wa Mahakama na wananchi kwa ujumla
kushiriki kwa karibu katika kipindi chote cha kumuuguza marehemu Jaji Utamwa
hadi kuzikwa kwake.
Baadhi ya Viongozi wengine waliotoa salaam za
rambirambi ni pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda, Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba,
Mwakilishi wa TLS na kadhalika ambao kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa
marehemu atakumbukwa kwa mchango wake katika tasnia ya sheria nchini ambapo alisimamia
haki kwa dhati na hata hukumu alizotoa zilikuwa kama mwongozo kwa wanasheria.
Marehemu
amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la Damu ambapo
tarehe 17 Desemba, 2022 alilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Mnamo
tarehe 18 Desemba, 2022 alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
kuendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomfika.
Marehemu
Jaji Dkt. Utamwa alizaliwa tarehe 30 Juni, 1963 na alijiunga na Mahakama ya Tanzania
tarehe 17 Februari, 1992 akianzia ngazi Hakimu
Mkazi. Alipanda ngazi mbali mbali ndani ya Mahakama na
hatimaye aliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 24 Juni, 2010.
Akiwa Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alifanya
kazi katika kanda za Dar es Salaam, Tabora, Mbeya na Iringa. Marehemu
ameacha mjane na Watoto watano (5) na mjukuu mmoja (1).
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda akizungumza jambo katika tuki hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego akitoa neno katika ibada hiyo.
Sehemu mbalimbali ya Viongozi wa Mahakama na Serikali walioshiri katika ibada ya maziko ya Jaji Utamwa kijijini Msemembo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni