Na Tiganya Vincent-Mahakama, Namtumbo
Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma, Kanali
Laban Thomas amewapongeza Mahakimu mkoani kwake kwa kuwatumikia
wananchi kwa uadilifu, jambo ambalo limesaidia kutokuwepo kwa malalamiko dhidi
yao.
Ametoa kauli hiyo tarehe 5 Januari, 2023
wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa majengo manne ya Mahakama za Wilaya ya
Namtumbo, Nanyumbu, Tandahimba na Ngara iliyofanyika katika viwanja vya
Mahakama ya Wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Kanali Thomas alisema katika vikao vya Kamati
ya Maadili ya Mahakimu walivyokaa hakuna lalamiko lolote lililotolewa na wananchi
dhidi ya Mahakimu hao.
Aliwataka kuendelea kuwatumikia wananchi kwa
kufuata haki na maelekezo ya sheria ili waendelee kuwa kioo kwa jamii katika
kuzingatia maadili ya kazi zao.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo alisema kwa
kuzingatia kuwa Mahakama ndio chombo pekee cha utoaji haki hapa nchini,
Serikali ya Mkoa wa Ruvuma itaendeleza ushirikiano uliopo, ikiwemo kuwapatia
maeneo ya ujenzi wa miundombinu ili kuwawezesha wananchi kupata haki katika
mazingira ya karibu.
Kanali Thomas alisema Serikali ya Mkoa kwa
kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa wanaendelea kushughulikia eneo la
ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki katika Manispaa ya Songea.
Alisema zoezi hilo linaendelea vizuri na
baada ya muda mfupi Mahakama ya Tanzania itapatiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa jengo
hilo, hivyo kusogeza huduma ya utoaji haki karibu na wananchi.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose
Mlyambina alisema kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati
ya Serikali na Mahakama, jambo ambalo limesaidia uboreshaji wa utoaji wa huduma
kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni