Alhamisi, 5 Januari 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA KUHAMIA DODOMA NDANI YA MIEZI MITATU IJAYO

Na Tiganya Vincent-Mahakama –Namtumbo

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amesema kuwa katika miezi mitatu ijayo kuanzia sasa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yaliyopo Dodoma yatakuwa tayari yamekamilika kwa ajili ya watumishi wote kuhamia kwenye majengo yake mapya.

Alizungumza hayo leo tarehe 5 Januari, 2023 katika halfa ya uzinduzi wa Mahakama za Wilaya ya Namtumbo, Ngara, Nanyumbu na  Tandahimba ilifanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Mhe. Siyani alisema hatua kubwa imepigwa katika ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Dodoma ambapo ujenzi umefikia asilimia 78.

Aidha Mhe. Siyani alisema uzinduzi wa Mahakama za Namtumbo, Nanyumbu, Tandahimba na Ngara ni matokeo ya uwezeshwaji unaoendelea kufanywa na Serikali pamoja na usimamizi na utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu wa Mahakama ya Tanzania.

Aliishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka misingi mizuri inayoiwezesha Mahakama kujenga miundombinu yake na hivyo kuwa na mazingira mazuri yanayoiwezesha Mahakama kutimiza wajibu wake.

Mhe. Siyani aliwahikikishia wananchi kwamba Mahakama itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu yake katika ngazi zote.

Alisema ujenzi wa majengo hayo na mengine yanayoendelea kujengwa kote nchini, unaenda sambamba na uwekaji wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema tayari timu ya kwanza imeshahamia Dodoma tangu tarehe 29 Desemba 2022 na timu zinatarajiwa kuendelea kuhamia Makao Makuu ya Mahakama hivi karibuni.

Kwa upande wa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Leonard Magacha alisema ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya ya Namtumbo, Nanyumbu, Ngara na Tandahimba umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.9 , fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani ya nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama (kulia) akisalimiana leo tarehe 5 Januari 2023 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto ) alipowasili katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Nanyumbu na Ngara.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe Gloria Lwomile (kulia) akitoa maelezo kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) alipowasili katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo kwa ajili ya hafla ya uzinduzi huo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (mwenye mkasi) akikata utepe leo kuashiria  uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Nanyumbu na Ngara.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akishirikiana na viongozi wengine kuweka jiwe la msingi la uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Tandahimba, Nanyumbu, Namtumbo na Ngara.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas (kulia) wakati hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Namtumbo na Ngara.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwaongoza viongozi wengine kumukumbuka aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa aliyefariki dunia hivi karibuni.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Leonard Magacha akitoa maelezo kuhusu majengo ya Mahakama za Wilaya ya Namtumbo, Nanyumbu, Tandahimba na Ngara wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo hayo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akibadilisha mawazo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo hayo.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Namtumbo wakiwa hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Nanyumbu na Ngara.
Wanakwaya kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Songea wakitumbuiza wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo hayo.

Baadhi ya viongozi wakiwa hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, Tandahimba, Nanyumbu na Ngara. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni