Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 05 Januari, 2023 ameshiriki pamoja na Majaji wengine wa Mahakama ya Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria ndugu jamaa na marafiki katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, marehemu Jaji Dkt. John Utamwa aliyefariki dunia tarehe 02 Januari, 2023.
Akitoa neno mara baada ya ibada hiyo iliyofanyika
katika kanisa ya Mtakatifu Albano Posta jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma amemtaja
marehemu Jaji Utamwa kama Jaji msomi ‘Intellectual Judge’ ambaye alifanya kazi
yake ya ujaji kwa umakini na alitumiwa muda kufanya tafiti za masuala
mbalimbali.
“Kifo cha Jaji Utamwa kilitushtua Mahakama na kimeacha
simanzi kubwa, kwangu mimi Jaji Utamwa nilimchukulia kama Jaji msomi ‘Intellectual
Judge’ ambaye alifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na vilevile alipenda kufanya
utafiti,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu amemtaja pia marehemu kama mtu mwenye utani
na vilevile alikuwa na mchango mkubwa
ndani ya Mahakama kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi mrefu katika Mhimili
huo, ambapo alikuwa mjumbe wa Kamati mbalimbali ikiwemo ya Kamati ya Jaji Mkuu
ya Kanuni ‘Chief Justice Rules Committee’.
Mhe. Prof. Juma alichukua nafasi hiyo pia kutoa
shukrani kwa Madaktari, wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mahakama
familia kwa kutoa msaada wa karibu wakati marehemu Jaji Utamwa akiwa amelazwa
katika hospitali hiyo. Ameongeza kwa kuahidi kuwa, Mahakama itaendelea kushirikiana
kwa karibu na familia ya marehemu Jaji Utamwa.
Akitoa salaam za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan naye Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa, wamesikitishwa na kifo cha Jaji
Utamwa na kueleza kuwa, Taifa limempoteza mtu muhimu kwenye tasnia ya sheria
nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Jaji Mkuu ya
Kanuni ‘CJ’s Rules Committee’, Mhe. Rehema Mkuye amekiri kuwa Kamati hiyo
imestushwa na kifo cha mjumbe wake, huku akitaja kuwa marehemu alikuwa mjumbe makini
ambaye alikuwa akitoa hoja zenye kujenga na hivyo pengo lake halitazibika.
Kadhalika, Mwakilishi wa ‘Summit’ Chama ambacho
marehemu alikuwa moja ya waanzilishi, Mhe. Jacobs Mwambegele amesema kuwa marehemu alikuwa mwanachama hai wa umoja huo ambapo aliweza kuchangia mawazo na hata michango licha ya kuwa mbali na Dar es Salaam. Mhe. Mwambegele ameongeza kuwa kabla ya umauti, takribani siku 12 nyuma marehemu alimpa ujumbe awafikishie wanachama wa chama hicho ambapo kati ya ujumbe aliowatumia ni kupendana na kushiriki.
Naye Mwakilishi wa familia ameishukuru Mahakama ya
Tanzania, MNH, majirani, ndugu, jamaa na marafiki kwa kushirikiana nao kwa
karibu tangu ugonjwa hadi kufariki kwa Jaji Utamwa.
Ibada hiyo iliyoanza mida ya saa 7 mchana imehudhuriwa
na Baadhi ya Viongozi na Watumishi wastaafu wa Mahakama akiwemo, Jaji Mkuu Mstaafu,
Mhe. Barnabas Samatta, baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (T), Majaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Wasajili wa
Mahakama, Watendaji, Mawakili, wake wa Majaji, ndugu jamaa na Marafiki.
Marehemu
amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la Damu ambapo
tarehe 17 Desemba, 2022 alilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa. Mnamo
tarehe 18 Desemba, 2022 alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
kuendelea kupatiwa matibabu hadi mauti yalipomfika.
Marehemu
Jaji Dkt. Utamwa alijiunga na Mahakama ya Tanzania
tarehe 17 Februari, 1992 akianzia ngazi Hakimu
Mkazi. Alipanda ngazi mbali mbali ndani ya Mahakama na
hatimaye aliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 24 Juni, 2010. Akiwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Marehemu Jaji Dkt. Utamwa alifanya
kazi katika kanda za Dar es Salaam, Tabora, Mbeya na Iringa.
Mwili wa Jaji Dkt. Utamwa
unatarajiwa kuzikwa siku ya Jumamosi, tarehe 07 Januari, 2023 katika Kijiji cha
Msemembo kilichopo Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi benchi la mbele kulia) akiwa katika ibada maalum ya kumuaga aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa. Ibada hiyo imefanyika leo tarehe 05 Januari, 2023 katika Kanisa yla Mtakatifu Albano Posta jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiingiza kanisani jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa.
Familia ya marehemu Jaji Utamwa i.e watoto wakiongozwa na mjane wa marehemu (katikati) wakiwa kwenye ibada ya kuaga mwili wa mpendwa wao.
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Barnabas Samatta (wa kwanza kushoto) akiwa katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu Jaji Dkt. Utamwa. Ibada hiyo ilifanyika katika kanisa Mt. Albano Posta jijini Dar es Salaam. wa kwanza kushoto kwa Jaji Samatta ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro. Aliyesimama wa kwanza kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa neno mara baada ya ibada ya kuaga mwili wa marehemu Jaji Utamwa.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akitoa neno mara baada ya ibada hiyo.
SEHEMU YA PICHA ZA VIONGOZI NA WANAFAMILIA WAKITOA NENO LA SHUKRANI KATIKA IBADA YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU JAJI UTAMWA
Zoezi la kuaga mwili wa marehemu Jaji Utamwa likiendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni