Na Faustine Kapama-Mahakama, Arusha
Akizungumza
wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesisitiza kuwa miradi yote inayoenda kutekelezwa kwa awamu ya pili ambayo ni ujenzi wa Vituo Jumusihi vya Utoaji Haki zaidi ya tisa na Mahakama za Mwanzo 60 lazima zikamilike mwezi Juni, 2024.
"Mvua inyeshe, jua liwake, lazima miradi hii ikamilike Juni, 2024 ili tuweze kubaki na mwaka mmoja wa matazamio. Haya tunayofanya tuyafanye wote, tushirikiane, tufanye kazi kwa pamoja kwa kuzingatia uwajibikaji na taaluma zetu," alisema.
Mhe. Dkt. Rumisha aliwaambia wahitimu hao wa mafunzo kuwa watakapokuwa wanatekeleza jukumu lililombele yao wanapaswa kujiuliza kama wale wataalamu watakaowapitisha watafanya kazi zao kwa weledi na kwa wakati.
Katika
kipindi cha siku tatu watumishi hao walipitishwa katika maeneo kadhaa kuhusu ufanyaji wa tathmini za zabuni na
wawezeshaji wabobezi kwenye mada hiyo, akiwemo Mtaalamu wa Manunuzi kutoka Benki ya Dunia, Mhandisi Raymond Mbishi, Mtaalamu wa Manunuzi kutoka Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE), Bw. Jackson Musiba na Mhandisi kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw.
Fredrick Pondamali.
Kwa wakati fulani, wawezeshaji hao walijikuta
katika mazingira ambayo hawakutegemea kufuatia mwitikio mkubwa, michango na
maswali ya “moto” kutoka kwa washiriki hao ambao walidhihirisha wazi kuelewa
mada zilizokuwa zinawasilishwa.
Akizungumza kabla ya kuhitimishwa mafunzo hayo, Bw.
Musiba aliwaomba watumishi hao kuichukulia miradi inayoenda kutekelezwa kama
mafanikio kwa Mahakama, hivyo hawana budi kujiepusha na ubinafsi. Amesisitiza
usimamizi mzuri wa mikataba na uimarishaji wa mahusiano mema na watendaji ili
kufikia mafanikio yanayotarajiwa.
Mahakama ya Tanzania, kupitia Kitengo cha
Maboresho, iliandaa mafunzo maalumu kwa watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo
Wahandisi, Wasanifu majengo, Maafisa Ugavi, Mahakimu, Wasajili, Wahasibu,
Wachumi na Watakwimu kuwajengea uwezo katika masuala yanayohusu ufanyaji wa
tathmini za zabuni.
Hatua hiyo inafuata baada ya kupata maombi 138 kutoka
kwenye makampuni ambayo yanataka kutoa ushauri kuhusu masuala ya usanifu
majengo pamoja na usimamizi wa miradi ya ujenzi.
Baada ya mafunzo hayo, Kamati hiyo ya Tathmini inaenda
kujichimbia kwa siku kadhaa kufanya zoezi la tathmini kujua wazabuni wapi
wanafaa kufanya kazi hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni